Jumapili, 12 Agosti, 2018
Leo ni Jumapili tarehe 29 Dhul-Qaadah, 1439 Hijiria sawa na tarehe 12 Agosti, 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1219 iliyopita, yaani siku ya mwisho ya mwezi Dhulqaada mwaka 220 Hijria Imam Muhammad Taqi (as) mmoja kati ya wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Mtukufu huyo alipewa jina la 'Jawad' likiwa na maana ya mtu mkarimu sana kutokana na ukarimu wake mkubwa. Imam Jawad alizaliwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka 195 Hijria na kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ridha (as). Kipindi cha maisha ya Imam Jawad kilikuwa kipindi cha kuchanua utamaduni wa Kiislamu na kuenea kwa fikra, itikadi na falsafa na kujitokeza mifumo ya fikra za Kimagharibi za Wagiriki na Warumi katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam alifanya juhudi kubwa kulea kizazi chenye maarifa na kueneza elimu na mafundisho sahihi ya Uislamu kama njia ya kukabiliana na fikra za kigeni sambamba na kufichua siri na maovu ya watawala wa Bani Abbas. Suala hilo liliwakasirisha mno watawala hao ambao hatimaye waliamua kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (SAW) katika siku kama hii ya leo.
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, alifariki dunia faqihi mkubwa wa Waislamu wa Shia na ustadhi mkubwa wa hauza ya kielimu ya mjini Najaf, Iraq, Agha Zia Addin Aragi. Agha Zia Addin Aragi alikuwa ni mmoja wa maulama wakubwa wa Waislamu wa Shia katika karne ya 14 Hijiria, ambaye alizaliwa mwaka 1278 Hijiria katika moja ya vijiji vya mkoa wa Arak, nchini Iran. Alihitimu masomo ya msingi mjini Arak, na kisha akaelekea mjini Najaf na kujiunga kwa maulama wakubwa wa enzi hizo kwa ajili ya elimu ya juu. Muda punde alipanda daraja na kufikia ngazi ya juu katika elimu ya fiqhi na elimu ya wapokezi wa hadithi, huku akiwa marjaa wa nafasi ya kwanza katika zama zake. Baada ya kufariki dunia allamah Akhond Khorasani, Agha Zia Addin Aragi aliasisi hauza kwa ajili ya masomo ya juu ambapo hata wanafunzi wengi wa allamah Akhondi walijiunga na hauza yake. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na 'Maqaalaatul-Usuul' na Tabswiratul-Allamah. Allamah Agha Zia Addin Aragi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 83.
Tarehe 12 Agosti mwaka 1949 yaani miaka 70 iliyopita, hati ya makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda majeruhi na mateka wa kivita ilipasishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi. Hati hiyo ilibuniwa kufuatia miamala isiyo ya kibinadamu na jinai zilizokuwa zikifanywa dhidi ya majeruhi na mateka wa kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi zenye mateka zilitakiwa kuwasilisha orodha ya majina ya mateka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani. Hata hivyo licha kuweko makubaliano hayo, lakini madola mengi duniani yamekuwa yakipuuza na kutojali haki za mateka na majeruhi wa kivita.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita sawa na tarehe 12 Agosti 1976, kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Tel al Zaatar iliyoko karibu na Beirut mji mkuu wa Lebanon, ilitekwa baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu na wanamgambo wa Kimaroni wa nchi hiyo na wakazi wake wakauawa kwa umati. Kambi hiyo ilikuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Palestina na ilianza kuzingirwa mwanzoni mwa mwaka 1976 kwa uungaji mkono na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulifanya hivyo kwa lengo la kushadidisha vita vya ndani huko Lebanon.
Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, Umoja wa Mataifa uliitangaza Agosti 12 kila mwaka, kuwa ‘Siku ya Vijana Duniani’ ili kueleza umuhimu wa vijana katika dunia ya sasa. Tabaka hili lenye utanashati la jamii ndiyo sababu ya maendeleo ya kila nchi kwa msingi huo vijana katika kila nchi wanapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Kutokana na umuhimu wao, vijana wanapaswa kulindwa na kusaidiwa na serikali hususan katika masuala ya ajira, makazi na kujenga familia. Katika upande mwingine kizazi cha leo cha vijana kinakabiliwa na changamoto nyingi za kimwili na kiroho ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na virusi vya HIV, intaneti na michezo ya computa ambayo inawatumbukzia vijana wengi katika ufuska na utovu wa maadili. Kutangazwa Siku ya Vijana Duniani kunaweza kusaidia juhudi za kuwakumbusha vijana umuhimu wao na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazolikabili tabaka hilo muhimu.