Aug 12, 2018 22:15 UTC
  • Jumatatu tarehe 13 Agosti 2018

Leo ni Jumatatu tarehe Mosi Dhulhija 1439 Hijria sawa na Agosti 13, mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita, Bibi Fatima Zahra binti ya Mtume SAW alianza maisha mapya baada ya kufunga ndoa na Imam Ali bin Abi Talib AS. Bibi Fatima alikuwa mwanamke mwema, mtukufu na kigezo bora cha Waislamu. Masahaba mashuhuri walijitokeza kumposa binti huyo wa Mtume. Hata hivyo, Mtume alikuwa akimjibu kila aliyekwenda kumposa binti yake huyo kwamba, suala la ndoa yake liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Baada ya kufunga ndoa, watukufu hao walianza maisha yao ya kawaida kabisa yaliyojaa huruma, upendo na masuala ya kiroho na kimaanawi. Familia hiyo imeitunuku dunia shakhsia adhimu na wa kupigiwa mfano kama Imam Hassan, Imam Hussein na Bibi Zainab (as).

Tarehe Mosi Dhulhija miaka 853 iliyopita alizaliwa msoni na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu, Ibn Abil Hadid katika eneo la Madain, Iraq ya sasa. Abu Hamid Abdul Majiid bin Muhammad Madaini maarufu kama Ibn Abil Hadid Muutazili alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa wa Muutazila, mtaalamu wa elimu za usuli, falsafa, teolojia na malenga. Kitabu chake mashuhuri cha Sherhe ya Nahjul Balagha ni kielelezo cha mapenzi ya Ibnu Abil Hadid kwa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) na familia ya Mtume Muhammad (saw) kwa ujumla. Kitabu hicho ni miongoni mwa vitabu muhimu sana katika nyanja za fasihi, historia na teolojia na kimekuwa marejeo ya wanazuoni wengi kwa miaka mingi. Athari nyingine za Ibn Abil Hadid ni pamoja na Al 'Abqariyul Hisaan, Al Qasaidul Sab'ul 'Alawiyaat (القصائد السبع العلویات) na Sherhul Muhassal. Ibn Abil Hadid alifariki dunia mwaka 656 Hijria akiwa na umri wa miaka 70.

Tarehe 13 Agosti miaka 119 iliyopita alizaliwa Alfred Hitchcock mtengeneza filamu mashuhuri wa Kiingereza. Alionesha kazi yake ya kwanza mwaka 1920 na baadaye akaanza kujihusisha na uongozaji filamu. Filamu zake za kuogopesha na za kusisimua zilikuwa mashuhuri mno katika zama hizo. Filamu hizo zilimfanya awe mashuhuri kwa jina la the Master of Suspense. Miongoni mwa filamu zake ni The Man Who Knew Too Much na Young and Innocent. Alfred Hitchcock aliaga dunia tarehe 28 Aprili 1980.

Alfred Hitchcock

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijikomboa na kupata uhuru toka kwa mkoloni Mfaransa. Ilikuwa katikati ya karne ya 19 wakati nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo kabla kwa jina la Ubangi-Shari, ilipounganishwa na makoloni ya Ufaransa barani Afrika. Hata hivyo mwaka 1958, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijipatia Mamlaka ya Ndani na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1960, ikajikomboa na kupata uhuru kamili.