Aug 15, 2018 02:34 UTC
  • Jumatano, 15 Agosti, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 3 Dhulhija 1439 Hijria sawa na Agosti 15, 2018.

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel ulilazimika kuondoka kwenye eneo la Ukanda wa Gaza, magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Eneo hilo lilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na wanajeshi wa Israel kwenye vita vya Waarabu na utawala huo ghasibu mwaka 1967. Licha ya kuwepo mapatano kati ya Tel Aviv na Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) mwaka 1993 na kuundwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambapo Ukanda wa Gaza nao ungepaswa kuwa chini ya mamlaka hiyo, lakini wanajeshi na walowezi wa Kiyahudi walikataa kuondoka katika eneo hilo. Hatimaye kufuatia mapambano ya wananchi wa Palestina na Intifadha ya Msikiti wa al-Aqswa jeshi la Israel na walowezi hao walilazimika kuondoka katika eneo hilo. Hata hivyo utawala huo ghasibu umeendeleza mashambulio ya kijeshi dhidi ya Gaza pamoja na mauaji yake dhidi ya Wapalestina.

Askari wa Israel wakiondoka Gaza kwa madhila

Miaka 28 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 24 Mordad 1369 Hijria Shamsia, Saddam Hussein Rais wa zamani wa Iraq alimtumia barua Hujjatul Islam Walmuslimin Hashemi Rafsanjani aliyekuwa Rais wa Iran wakati huo, akimjulisha kwamba amekubali kikamilifu vipengee vya makubaliano ya mpaka yaliyotiwa saini 1975 nchini Algeria. Hata hivyo, tarehe 27 Shahrivar 1359 Hijria Shamsia, Saddam Hussein baada ya kushawishiwa na madola ya kibeberu ya Magharibi, alijitokeza kwenye televisheni ya Iraq na kuuchanachana mkataba huo, na baada ya siku chache, alianza kuivamia ardhi ya Iran. Saddam Hussein na waitifaki wake walidhani kwamba, muda mfupi tu baada ya kuivamia ardhi ya Iran wangeliweza kuuangusha mfumo mchanga wa Kiislamu hapa nchini. Hata hivyo kusimama kidete wananchi na mapambano ya wapiganaji shupavu wa Kiislamu wa Iran yalibatilisha njama zao na jeshi vamizi la Iraq likalazimika kurejea nje ya mipaka ya Iran baada ya kushindwa mtawalia. 

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita nchi ya Jamhuri ya Congo Brazzaville ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Huko nyuma Congo Brazzaville ilikuwa sehemu ya ardhi ya Congo katika Afrika Magharibi iliyojumuisha Zaire ya zamani na Angola.  Kongo Brazzaville iligunduliwa na Wareno katika karne ya 15 na baadaye ilikaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kifaransa kwa miaka kadhaa mfululizo. Kongo Brazaville iko magharibi mwa Afrika ikipakana na Jamhuuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola. 

Bendera ya Congo Brazzaville

Congo Brazzaville yenye ukubwa wa kilomita mraba 342, 000 inapakana na nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Gabon, Jamhuri ya Kidemokorasia ya Congo na Angola. 

Miaka 70 iliyopita, sawa na tarehe 15 Agosti 1948 nchi ya Korea ya Kusini iliundwa baada ya kujitokeza mgawanyiko wa visiwa vya Korea. Visiwa vya Korea vilikabiliwa na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu wa madola yenye nguvu katika eneo hilo kama vile China na Japan tokea nusu ya kwanza ya karne ya ishirini.

Bendera

Na siku kama ya leo miaka 71 iliyopita India walipata uhuru baada ya mapambano ya miaka kadhaa dhidi ya mkoloni Muingereza. India ni nchi yenye historia kongwe na utamaduni mkubwa na ilitawaliwa na silsila mbalimbali za ndani na nje ya nchi hiyo. Uislamu ulienea katika baadhi ya maeneo ya India katika karne ya 8 Miladia. Ushawishi wa kikoloni ulianza huko India tangu karne ya 16 Miladia ambapo Uingereza ilifanikiwa kuikalia kwa mabavu na kuidhibiti nchi hiyo baada ya kumshinda hasimu wake wa Ulaya yaani Ufaransa na pia Watimori wa India.

Ramani ya India