Aug 15, 2018 22:02 UTC
  • Alkhamisi tarehe 16 Agosti 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Mfunguo Tatu Dhulhija 1439 Hijria sawa na tarehe 16 Agosti 2018.

Siku kama leo miaka 130 iliyopita, alizaliwa Thomas Edward Lawrence, jasusi mkubwa wa Uingereza aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuzidhoofisha nchi za Kiarabu. Kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia Lawrence alikuwa amefanya safari katika nchi kadhaa za Kiarabu, ambapo sanjari na kujifunza lugha ya Kiarabu, alijifunza pia tamaduni na maisha ya Waarabu. Katika vita hivyo vya Kwanza vya Dunia vilivyojiri kati ya mwaka 1914 hadi 1918, na kwa msingi wa siasa za kikoloni za Uingereza, Lawrence alifanya njama kubwa kuyachochea makabila ya Kiarabu kwa kisingizio cha kutaka kujitawala, ili yaweze kujitenga mbali na utawala wa Othmania ambao katika vita hivyo ulikuwa ukikabiliana na Uingereza. Aidha Thomas Edward Lawrence alikuwa na nafasi kubwa pia katika kuuingiza madarakani ukoo wa Aal-Saud nchini Saudia, suala ambalo lilipelekea kupata umashuhuri mkubwa kwa jina la Lawrence of Arabia.

Lawrence of Arabia

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita alifariki dunia Bi Margaret Mitchell mwandishi wa Kimarekani. Bi Mitchell alizaliwa tarehe 8 Novemba huko Atlanta katika jimbo la Georgia. Baba yake Bi Mitchell alikuwa wakili wa mahakama. Kwa muda fulani alisomea taaluma ya udaktari, lakini baadaye alilazimika kukatisha masomo hayo kutokana na majonzi yaliyosababishwa na kifo cha baba yake. Margaret alianza kazi ya uandishi akiwa na miaka 22. Alizidi kupata umashuhuri baada ya kuchapisha riwaya yake aliyoipa jina la "Gone with The Wind."

i Margaret Mitchell

 

Tarehe15 Agosti miaka 58 iliyopita, kisiwa cha Cyprus kilipata uhuru baada ya machafuko ya miaka kadhaa. Kisiwa hicho ambacho hii leo kinaendeshwa chini ya mfumo wa jamhuri, kiko katika bahari ya Mediterranean kusini mwa Uturuki kikiwa na ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 9000. Kwa miaka kadhaa kisiwa cha Cyprus chenye historia kongwe na muhimu katika eneo kilikuwa chini ya falme za Iran, Ugiriki, Misri na utawala wa Othmania. Lakini mwaka 1878, utawala wa  Othmania ulikabidhi usimamizi wa kisiwa hicho kwa Uingereza katika mkutano uliofanyika mjini Berlin Ujerumani na mwaka 1925 kisiwa cha Cyprus kikawa rasmi koloni la Uingereza.

Bendera ya Cyprus

Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 25 Mordad 1372 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 16 Agosti mwaka 1993 Miladia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari mwanachuoni mashuhuri wa nchini Iran. Ayatullah Sabzawari alizaliwa mnamo mwaka 1290 Hijiria Shamsia, sawa na mwaka 1911 Miladia, katika mji huo uliopo kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanachuoni huyo licha ya kujipatia elimu zake za msingi katika mji wa Sabzawar na kisha kusoma elimu ya dini mjini Mash’had, alielekea Najaf nchin Iraq na kujipatia elimu ya juu ya maarifa ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari ameandika vitabu vingi maarufu zaidi ikiwa ni pamoja na tafsiri ya Qur'ani tukufu ya ‘Mawaahibul-Rahman fii Tafsirul-Qur’an’ chenye juzuu 20, ‘Muhadh-Dhibul-Ahkaam fii Bayaanil-Halali wal-Haraam’ chenye juzuu 30 na ‘Tahdhibul-Usuulu’ chenye juzuu mbili.