Ijumaa tarehe 17 Agosti 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 5 Dhulhija 1439 Hijria sawa na Agosti 17, 2018.
Miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo, Rudolf Hess makamu wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler alijiua akiwa jela nchini Uingereza. Hess ambaye alizaliwa mwaka 1894, alikuwa mmoja wa waasisi wa chama cha Kinazi na miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali ya Hitler. Rudolf Hess alihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya jinai za kivita ya Nuremberg nchini Ujerumani baada ya nchi hiyo kushindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. Hess alijiua akiwa jela mwaka 1987.
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Gabon iliyoko magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Atlantiki, ilipata uhuru wake. Wareno walifika huko Gabon kwa mara ya kwanza mwishoni mwa karne ya 15 Miladia. Hata hivyo nafasi ya kijiografia ya Gabon ilizuia kugunduliwa nchi hiyo hadi karne ya 19. Katikati ya karne ya 19 Wafaransa waliwasili Gabon na kuidhinishwa kuitawala nchi hiyo katika mkutano uliofanyika huko Berlin Ujerumani. Hatimaye mwaka 1960 Gabon ilipata uhuru. Kijiografia nchi ya Gabon inapakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kongo, Cameroon na Equatorial Guinea.
Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, wananchi wa Indonesia walianzisha mapambano ya kujikomboa kutoka katika makucha ya mkoloni Mholanzi. Mapambano hayo yaliyoongozwa na Ahmad Sukarno yaliendelea kwa miaka minne huko Indonesia. Baada ya kushadidi mapambano hayo ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Indonesia, Umoja wa Mataifa uliiamuru serikali ya Uholanzi kuuasisi utawala kwa jina la " Umoja wa Indonesia na Uholanzi". Jamhuri ya Indonesia ilivunja umoja huo mwaka 1956 na kutangaza uhuru wa nchi hiyo na Sukarno akawa Rais wa kwanza wa taifa hilo.
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita sawa na tarehe 5 Mfunguo Tatu mwaka 1361 Hijiria, Allamah Muhammad Hussein Kampani aliyekuwa mwanafalsafa na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, alifariki dunia katika mji wa Najaf nchini Iraq. Mwanzuoni huyo alibobea katika masuala ya falsafa, Irfani, historia, jiografia, mashairi na fasihi. Allamah Kampani ameandika risala na vitabu vingi katika taaluma za falsafa, irfani, fasihi na fiqhi.