Aug 17, 2018 23:42 UTC
  • Jumamosi, 18 Agosti, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 6 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1439 Hijria mwafaka na tarehe 18 Agosti 2018 Miladia.

Leo ni Jumamosi tarehe 6 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1439 Hijria mwafaka na tarehe 18 Agosti 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1365 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu, waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao. ***

Eneo la Ajnadeen jirani na Palestina

Katika siku kama ya leo miaka 1181 iliyopita, alizaliwa Abu Ali Muhammad ibn Hammam, mmoja wa maulama mashuhuri wa Iran. Ibn Hammam alikuwa akiishi mjini Baghdad, Iraq ambapo alifanikiwa kusoma elimu ya hadithi kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake. Msomi huyo pia alikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walijifunza kwake elimu ya hadithi na elimu nyingine za Kiislamu. Abu Ali Muhammad ibn Hammam,ameacha vitabu kadhaa katika uga wa hadithi. ***

Abu Ali Muhammad ibn Hammam

Miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Muhammad Ghaffari aliyekuwa na lakabu ya Kamal al-Mulk mchoraji mahiri wa Kiirani. Alisoma katika skuli ya Darul Funun ya Tehran na kupata mafanikio makubwa katika fani ya uchoraji aliyokuwa akiipenda. Kipindi fulani Muhammad Ghaffar alifanya kazi katika utawala wa Nasser Deen Shah Qajar na kufanikiwa kutoa athari zenye thamani kubwa za uchoraji.***

Kamal al-Mulk

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, mamia ya mahujaji wa Iran na wengine kutoka nchi tofauti waliokuwa wameenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba mjini Makka na wakiwa katika hali ya kutekeleza ibada ya faradhi ya kujitenga na mushrikina, waliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Saudi Arabia. Ni vyema kukumbusha kuwa, mahujaji wa Iran kwa miaka yote huwa wanatekeleza ibada hiyo kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo mbali na kuwasisitizia Waislamu kuungana, hutangaza kujibari na kujitenga na maadui wa Uislamu hususan Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Kwa hakika ibada hiyo ambayo hufanyika kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, huwa na taathira kubwa katika msimu wa hija. Ni kwa ajili hiyo, ndio maana Imam Khomein Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akasisitizia sana umuhimu wa ibada ya kujitenga na mushrikina na maadui wa dini ya Kiislamu. ***

askari wa utawala wa Aal Saud walivyoua Mahujaji

Na katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, baada ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq, hatimaye Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kusimamishwa vita hivyo kwa mujibu wa moja ya vipengee vya azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la umoja huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, madola yanayopenda kujitanua ambayo yaliona maslahi yao yamo hatarini hapa nchini yalianza kutekeleza njama mbali mbali ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran. Saddam Hussein kibaraka wa madola ya Magharibi na hasa Marekani, wakati huo akiwa Rais wa Iraq alitumiwa na Washington na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya taifa la Iran akitumia visingizo visivyo na msingi wowote. Mwanzoni mwa vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutaka kusimamishwa vita hivyo, ingawa cha kusikitisha katika azimio hilo ni kwamba, baraza hilo halikuashiria hata kidogo uchokozi wa majeshi vamizi ya Iraq dhidi ya taifa la Iran. ***

Azimio nambari 598