Sep 01, 2018 04:06 UTC
  • Jumamosi, Septemba Mosi, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Tatu Dhulhija 1439 Hijria mwafaka na tarehe Mosi Septemba mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1312 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Mussa al-Kadhim (AS) ambaye ni mmoja kati ya wajukuu watukufu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alilewa na baba yake Imam Ja'afar bin Muhammad Swadiq (as) na kupata elimu na maarifa ya Kiislamu kutoka kwa mtukufu huyo kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Kadhim (as) alishika hatamu za Uimamu na uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35 na kukabiliana na mashaka mengi. Imam Kadhim (as) alipitisha kipindi kikubwa cha umri wake katika kuwazindua na kuwaelimisha Waislamu maarifa asili ya dini. Suala hili liliwatia hofu kubwa watawala wa Bani Abbas ambao walimkamata na kumfunga jela ili kumuweka mbali na Waislamu waliokuwa na kiu ya maarifa halisi ya dini yao. Imam Kadhim (AS) alisifika kwa ukarimu mkubwa, uvumilivu na usamehevu. Tunatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kuadhimisha siku hii muhimu ya kuzaliwa mtukufu huyo. ***

 

Miaka 844 iliyopita katika siku kama ya leo, ilianza kazi ya kujenga mnara maarufu wa Pisa huko katika mji wa Pisa nchini Italia. Mnara huo ulijengwa kwa ajili ya kuitundika saa juu yake. Hata hivyo mnara huo uliokuwa na urefu wa mita 55 ulipinda kwa karibu mita tano muda mfupi baada ya kuanza kujengwa. Hitilafu hiyo imeufanya mnara huo ujulikane kwa jina la"Mnara Uliopinda wa Pisa." Hadi kufikia sasa mnara huo umefanyiwa marekebisho ya kiwango fulani kufuatia juhudi za wahandisi na wataalamu wa nchi mbalimbali. ***

Mnara wa Pisa

 

Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulioambatana na uharibifu mkubwa na kuua idadi kubwa ya watu, ulitokea nchini Japan. Zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 8.3 kwa kipimo cha Rishta iliua watu zaidi ya laki moja na 40 elfu. Mtetemeko huo uliyakumba hata baadhi ya maeneo ya miji ya Tokyo na Yokohama. Mbali na hasara kubwa zilizosababishwa na mtetemeko huo, idadi kubwa ya Wajapani pia walikosa makazi yao na nyumba nyingi ziliteketea kwa moto.***

Mtetemeko wa ardhi Japana

 

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, Vita vya Pili vya Dunia vilianza baada ya jeshi la Ujerumani ya Kinazi kuanzisha mashambulizo dhidi ya Poland. Adolf Hitler alianza kuliandaa jeshi lenye nguvu wakati akiwa madarakani huko Ujerumani kwa kutumia vibaya hadhi yake na hisia za ubaguzi na utaifa wa wananchi wa nchi hiyo, ambao walikuwa wamefedheheka sana kufuatia kushindwa vibaya katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Katika kipindi kifupi, Hitler alifanikiwa kuikalia kwa mabavu sehemu kubwa ya ardhi za Ulaya na kaskazini mwa Afrika. ***

Kuanza Vita vya Pili vyya Dunia

 

Na miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo, kulifanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Libya yaliyomfikisha madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Kabla ya mapinduzi hayo, Libya ilikuwa ikiongozwa na utawala wa Mfalme Idris wa Kwanza. Wakati mfalme Idris alipoelekea nchini Uturuki kwa ajili ya matibabu, kundi moja la wanajeshi ambalo liliongozwa na Kanali Muammar Gaddafi lilifanya mapinduzi ya kijeshi na kumvua madaraka mfalme huyo sambamba na kutangaza utawala wa kisoshalisti nchini Libya. Hata hivyo katika miaka ya kukaribia kupinduliwa na kuuliwa, Muammar Gaddafi alianza kufuata siasa za Wamagharibi na kuwakabidhi viwanda vya mafuta vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hali inayodaiwa kuchangia hasira za wananchi. Muammar Gaddafi aliondolewa madarakani na kuuawa kufuatia mapinduzi ya tarehe 21 mwezi Agosti 2011.***

Kanali Muammar  Gaddafi