Sep 09, 2018 14:30 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya sita ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tuligusia kwa muhtasari sisitizo la Imam Khomeini juu ya sekta ya ubinafsishaji kuwa inayokamilisha shughuli za kiuchumi nchini, ambapo serikali na sekta za ushirika zimetakiwa kuizingatia na kufanya juhudi  katika uga huo. Pia tukasema kuwa, shakhsia huyo aliwataka matajiri kugawa mali zao kwa watu masikini kwa kuwa jambo hilo ni kwa maslahi yao wenyewe hasa kwa kutilia maanani kwamba, linamaliza malalamiko ya watu masikini katika jamii. Leo tutazungumzia suala lingine ambalo ni uadilifu wa kisiasa katika jamii.

Ndugu wasikilizaji uadilifu wa kisiasa ni miongoni mwa wigo wa uadilifu wa kijamii ambao unajumuisha uga wa utawala, siasa na ushiriki wa wananchi katika serikali. Aidha kwa kuzingatia umuhimu wa suala hilo katika kuainisha mustakabali wa wananchi, tunaweza kusema kuwa, uadilifu wa kisiasa una nafasi ya uundaji na uainishaji katika kufikiwa uadilifu wa kijamii katika umma. Hii ikiwa na maana kwamba, ili kuwawezesha raia wote kushiriki kwa usawa sambamba na kulindwa haki za wananchi ambapo raia wote bila kuzingatia utofauti wao wa kimtazamo kisiasa, kidini, kimadhehebu, rangi, lugha na kabila hawapaswi kunyimwa haki ya ushiriki wa kisiasa, ni kwa watawala kuandaa anga kwa ajili ya raia hao na kwa namna ya usawa, waweze kuunda miungano yao ya kiraia au ya kisiasa na kuendesha harakati zao kwa uhuru. Kwa mujibu wa sheria, raia wote wako sawa na masuala kama hayo ni miongoni mwa mambo muhimu katika uga wa uadilifu wa kisiasa. Mtazamo wa Imam Khomeini (MA) kuhusu uadilifu wa kisiasa umegawanyika katika pande tatu kuu na muhimu. Wa kwanza ni kutambua kuwa ni haki kushiriki raia wote katika masuala ya kisiasa, pili ni kutambua kuwa ni haki kufuatilia utendajikazi wa watawala na tatu ni kutambua kuwa watu wako huru, kuunda vyama na miungano ya kisiasa, kiraia, kimrengo na kuunda mijumuiko ya malalamiko.


************


Msingi wa mtazamo wa kisiasa wa Imam Khomeini katika kuunda utawala wa Kiislamu, unatokana na nadharia ya Walii Faqihi (fakihi mtawala, aliye na ufahamu wa kutosha kuhusu sheria za Kiislamu). Mtukufu huyo alitambua kuwa usimamizi wa kisiasa wa kiongozi huyo aliyetimiza masharti juu ya masuala yote ya jamii, unategemea matakwa na irada ya Mwenyezi Mungu, ingawa pia aliamini kwamba bila kupatikana ridhaa ya walio wengi na kukubaliwa na jamii, suala hilo haliwezi kuthibiti. Sambamba na kukosoa mwenendo wa uteuzi wa kiongozi katika mfumo wa kiutawala wa kurithishana, Imam alitaja aina hiyo ya utawala kuwa chanzo cha udikteta katika jamii na kuhusiana na hilo aliamini kwamba, raia wote wanatakiwa kuwa na nafasi katika kumchagua kiongozi. Kwa ajili hiyo, kuandaa uwanja wa ushiriki wa kweli, wa usawa na mpana zaidi wa wananchi hao katika masuala yote ya nchi yao, ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa maana hiyo, katika fremu ya fikra na idolojia ya Mapinduzi ya Kiislamu, ushiriki wa kiuadilifu na wa usawa wa wananchi wote, umetajwa kuwa moja ya malengo ya uadilifu wa kisiasa. Katika kipengee cha nane cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imeelezwa kwa wazi moja ya nyadhifa za serikali katika kutumia nyenzo zilizopo kwa ajili ya ‘ushiriki wa watu wote katika kuainisha mustakbali wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.’


*******


Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya sita ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ndugu wasikilizaji moja ya malengo muhimu ya uadilifu wa kisiasa katika nadharia ya Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni kuzinufaisha pia jamii za wafuasi wa dini za walio wachache na kuwapa haki ya kisiasa. Umuhimu wa suala hilo unadhihiri pale tunapodiriki kwamba Imam Khomeini (MA) mbali na kuwa kiongozi na marjaa wa kidini ambaye pia aliunda serikali kwa msingi wa dini ya Uislamu na kwa kuzingatia asili ya dini, alisaidia sana kuandaa mazingira ya kuimarishwa nadharia ya upande wa pili kwa wafuasi wa dini nyingine nchini. Katika mtazamo wa kifikra na kisiasa wa Imam Khomeini katika utawala wa Kiislamu, wafuasi wa dini nyingine wanahesabiwa kuwa sawa na raia wengine ambapo wana haki na kutakiwa kuheshimiwa kikamilifu. Mtukufu huyo aliweka wazi kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfumo wa wananchi na kwamba, wafuasi wa dini za walio wachache ni sawa na raia wengine kuhusiana na suala la uhuru wa kushiriki katika masuala ya nchi yao. Alisisitiza kwamba moja ya majukumu ya serikali ya Kiislamu ni kutetea haki na usalama wa watu wa dini za walio wachache kama ambavyo aliwahakikishia watu wote kwamba katika mfumo wa Kiislamu, jamii zote za dini za walio wachache zitapata uhuru na ustawi kamili katika jamii.


*******


Kwa msingi wa mtazamo huo, katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumewekwa wazi na kuzingatiwa suala la kutetea haki na uhuru wa kisiasa na kijamii za wafuasi wa dini za walio wachache katika maisha yao ya kisiasa na kijamii. Mbali na hayo ni kwamba katika baadhi ya mambo watu hao wamependelewa zaidi ili haki zao zisije zikapuuzwa katika jamii. Kwa mfano, kipengee cha 64 cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kunabainisha taratibu za uchaguzi wa wawakilishi wa wananchi katika bunge ambapo wafuasi wa dini za wachache wamepewa haki maalumu ili kuwa na wawakilishi wao katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani bunge. Kwa mujibu wa kipengee hicho, wafuasi wa Uzartoshti na Mayahudi  wana wawakilishi wao bungeni, huku Wakristo wa Ashuri na Wakeldani (Wakaldu) nao wakiwa na mwakilishi mmoja. Aidha Wakristo wa Armenia, kaskazini na kusini mwa nchi kila kundi mojawapo lina mwakilishi mmoja bungeni. Kwa hakika, hatua ya jamii inayoundwa na watu zaidi ya asilimia 95 ambao ni Waislamu, kuwepo wawakilishi watano wa jamii za dini za wachache bungeni ni moja ya madhihirisho ya uhalisia wa uadilifu wa kisiasa ambao unaakisiwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wafuasi wa dini za walio wachache nchini.


Wapenzi wasikilizaji sehemu ya sita ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.  
 

 
 

 

Tags