Nov 03, 2018 13:05 UTC
  • Ruwaza Njema (8)

(Kumfuata al-Mustafa (saw) katika maneno na kimya chake)

Assalaama Aeikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni tuwe pamoja katika sehemu nyingine ya kipindi cha hiki ambapo kwa leo tutazungumzia Hadithi zinazotusihi tuige mfano bora wa Mtume Mtukufu (saw) katika ukweli, kutekeleza ahadi, kulinda amana kutamka maneno mazuri na kuwa wavumilivu.

********

Imam Ja'ffar (as) anasema katika Hadithi iliyopokelewa kutoka kwake katika kitabu cha Ilal as-Sharai': 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimuahidi mtu mmoja pembeni ya mwamba na kumwambia: Mimi nitakusubiri hapa hadi uje. Jua lilikuwa kali na likimchoma Mtume. Masahaba zake wakamwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Itakuwa vizuri iwapo utaenda kwenye kivuli. Mtume akasema: Mimi nimewekeana naye ahadi hapa na iwapo hatakuja hadi Siku ya Kiama, nitamsubiri hapa hapa.'

 

Naye Qutb ad-Deen ar Rawandi amemnukuu Ammar bin Yassir (MA) katika kitabu chake cha Qisas al-Anbiyaa akizungumzia uhusiano wake wa karibu na Mtume kabla ya kubaathiwa kuwa Mtume (saw) kwa kusema: 'Nilikuwa nikilisha kondoo wa familia yangu naye Mtume (saw) pia akilisha kondoo. Nilimwambia: Ewe Muhammad! Je utakuja twende kulisha kondoo katika eneo la malisho ambalo ninajua lina malisho mengi mazuri na yanayonawiri? Akasema: Sawa. Nilipokwenda katika eneo hilo (Fakh) kesho yake, nilimkuta Muhammad (saw) akiwa tayari amefika hapo kabla yangu huku akiwa amesimama na kuwazuia kondoo wake kuingia katika malisho hayo. Alisema: Sikutaka kuanza kulisha kondoo wangu kabla hujafika kwa sababu tulikuwa tumeahidiana.'

*********

Na katika mifano ya tabia njema ya Mtume Mtukufu (saw) katika kulinda amana, tunasoma Hadithi iliyonukuliwa na mwanazuoni mcha-Mungu na mwenye takwa Abul Hussein Waram bin Abi Faras (MA) katika kitabu chake cha Tanbihul Khawatir akimnukuu Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) ambaye aliwaambia masahaba zake: 'Rudisheni amana, hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa akirudisha amana hata kama ulikuwa ni uzi na sindano.' Imam Swadiq (as) anakusudia kwamba Bwana wa Walinda-amana (saw) alikuwa akichunga sana amana na kuwarejeshea watu amana zao, ziwe ni za thamani kubwa au ndogo.

Mnaendelea kutegea sikio kipindi hiki cha Ruwaza Njema kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Tunasoma Hadithi ifuatayo ambayo imenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi kutoka kwa Imam Muhammad al-Baqir (as) ambaye anasema: 'Yahudi mmoja alifika mbele ya Mtume (saw), Bibi Aisha akiwa pembeni yake na kusema: Sam iwe juu yako. Mtume (saw) akamjibu kwa kusema: (Na) juu yenu.' Na kabla ya kuendelea na Hadithi hii wapenzi wasikilizaji, tunaashiria hapa nukta hii kwamba neno 'sam' ni katika maneno yaliyo na maana ya mauti na makusudio ya Yahudi yule yako wazi hapa. Imam Baqir (as) anaendelea kusema: 'Kisha Yahudi mwingine aliingia mahala pale na kusema vilevile alivyosema mwenzake. Mtume (saw) alimjibu vilevile alivyomjibu yule Yahudi wa kwaza. Yahudi mwingine wa tatu akaingia na kusema vilevile walivyosema wenzake. Mtume alimjibi kama alivyowajibu wenzake waliomtangulia. Aisha alikasirika na kusema: 'Sam, ghadhabu na laana iwe juu yenu enyi kundi la Mayahudi, enyi ndugu wa nyani na nguruwe!' Mtume (saw) akamwambia: 'Ewe Aisha! Lau kama matusi yangekuwa umbo na kuoneka nje kwa macho, yangelidhihiri kwa sura mbaya na ya kuchukiza sana. Hakika urafiki na uvumilivu haukuwekwa juu ya kitu ila ulikipendeza na haukutolewa juu ya kitu ila uliharibu sura yake.' Aisha akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je haukusikia wakisema: Sam (mauti) iwe juu yako? Akajibu: Bila shaka nilisikia, lakini je, haukusikia nililowajibu? Nilisema: Juu yenu (pia). Iwapo Mwislamu atakusalimuni, mjibuni kwa kusema: Assalaam Aleikum na akikusalimuni kafiri, mjibuni kwa kusema: Juu yako.'

 

Na tunasoma katika kitabu cha az-Zuhd cha Sheikh al-Hussein bin Said ambaye ni mmoja wa masahaba wa Imam Hadi (as) ambaye anamnukuu Imam Swadiq (as) akisema: 'Mwanamke mmoja asiye na murua na mwenye matusi, alipita karibu na Mtume (saw) akiwa ameketi chini huku akila chakula na kumwambia: Ewe Muhammad! Unakula chakula na kuketi kama mtumwa?! Mtume (saw) akamjibu: Mimi ni mtumwa na je, kuna mtumwa mwingine yupi ambaye ni mtumwa zaidi kuniliko mimi mbele ya Mwenyezi Mungu?' Akasema mwanamke yule: Je, utanipa tonge katika chakula chako hiki? Baada ya Mtume (saw) kumpa tonge, alisema mwanamke yule: 'Si tonge hili, bali tonge lililo kwenye mdomo wako.' Mtume alitoa tonge lililokuwa kwenye mdomo wake na kumpa mwanamke huyo. Baada ya kula tonge hilo kutoka kwenye mdomo wa Mtume (saw) mwanamke yule hakutamka tena maneno machafu hadi alipoaga dunia.'

***********

Na kwa Hadithi hiyo tukufu wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi wakati huu. Basi hadi tutakapojaaliwa kujiunga nanyi tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

 

Tags