Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-12
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 12 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Katika kipindi kilichopita tulizungumzia nafasi ya vyombo vya mahakama na majaji wake kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA) na tukasema kuwa, kutekelezwa uadilifu na usalama wa kimahakama kwa mujibu wa misingi na vigezo vya Uislamu, ni mambo yaliyosisitizwa sana na mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo karibuni.
Ndugu wasikilizaji mtakumbuka kuwa katika vipindi vilivyopita, tuliashiria uadilifu wa kimahakama yaani kuandaliwa mazingira ya kuwadhaminia watu haki zao na kuwakinga waliodhulumiwa dhidi ya uwezekano wa kupoteza haki zao yalikuwa moja ya malengo na kaulimbiu ya raia wa Iran katika kipindi cha mapinduzi ya Kiislamu na ambayo yaliashiria na kusisitizwa kwa nyakati tofauti na Imam Khomeini (MA). Ni kwa msingi huo ndipo katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kukatengwa kipengee maalumu cha vyombo vya mahakama ambapo ndani yake kumefafanuliwa misingi tofauti inayohusiana na suala hilo kupitia nyenzo za kufikiwa uadilifu wa kimahakama. Zaidi ya hayo ni kwamba katika vipengee vingine pia kumewekwa wazi umuhimu wa kusimamiwa haki na kuainishwa mihimili ya serikali hususan vyombo vya mahakama sambamba na kuhimizwa kutekelezwa suala hilo. Misingi hiyo kwa pamoja ndiyo iliyofanikisha kupatikana kwa hati ambayo kupitia vyombo vya mahakama, uadilifu na usalama wa kimahakama unaweza kudhaminiwa kwa ajili ya wananchi. Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeviarifisha vyombo vya mahakama vya nchi hii kuwa wenzo muhimu wa kufikiwa uadilifu wa Kiislamu ambapo katika kipengee cha tatu cha katiba hiyo kumebainishwa wazi moja ya nyadhifa za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni kufikiwa uadilifu wa kimahakama. Kadhalika kwa mujibu wa katiba ya Iran, uadilifu ni moja ya misingi mikuu ya mfumo ambapo watunga sheria wote wanatakiwa kuzingatia msingi huo muhimu katika shughuli yao hiyo.
********
Katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jukumu kuu la kufikiwa uadilifu na usalama wa kimahakama limekabidhiwa vyombo vya mahakama. Kwa mujibu wa kipengee cha 156, vyombo vya mahakama ni vyenye kujitegemea ambapo vinatakiwa kulinda haki za mtu binafsi na za jamii nzima kwa ujumla. Na ili kufikia lengo hilo, vinatakiwa kuchunguza madai ya uonevu, ukiukaji wa haki na mashitaka ambapo ili kutatuliwa madai na mizozo, vinatakiwa kutoa maamuzi na hukumu stahiki. Moja ya daghadagha ya Imam Khomeini kwa ajili ya kufikiwa uadilifu wa kimahakama katika jamii ilikuwa ni kuwateua watu wema na wenye vigezo na wanaofahamu sheria za Kiislamu kwa ajili ya kutoa hukumu kati ya watu. Kwa nyakati tofauti na ikiwemo usia wake, alilitaja suala hilo kuwa muhimu katika kufikiwa uadilifu wa kimahakama katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kusema: "Moja ya masuala muhimu ni kadhia ya kutoa hukumu ambayo italinda kazi, nafsi, mali na heshima za watu. Ushauri wangu ni kwa Kiongozi Muadhamu au Baraza la Uongozi kufanya bidii na kuwa na uangalifu mkubwa katika uteuzi wa kiongozi wa juu zaidi katika vyombo vya mahakama. Wanapasa kuwateua watu waaminifu walio na uzoefu wa kutosha na wenye uelewa katika masuala ya sheria za Kiislamu." Mwisho wa kunukuu. Kwa msingi huo, katika kipengee cha 57 cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumebainishwa kwamba, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anatakiwa kumteua shakhsia aliyefikia kiwango cha ijtihadi, mwadilifu, mwenye ufahamu wa masuala ya kimahakama, msimamizi bora na mwenye tadbiri kuwa mkuu wa vyombo vya mahakama. Kadhalika kutokana na udharura wa kuwepo majaji wenye sifa zinazofaa kwa ajili ya kusimamia uadilifu wa kimahakama, katika kipengee cha 158 cha katiba, moja ya nyadhifa za mkuu wa vyombo vya mahakama, ni kuwaajiri majaji waadilifu na wenye sifa zinazofaa kwa jili ya kusimamia suala hilo.
*********
Kama kwanza ndio unafungua redio yako kilipindi kilicho hewani ni Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hii ikiwa ni sehemu ya 12 ya makala hizi.
Ndugu wasikilizaji, falsafa ya elimu ya sheria ambayo inalenga kudhamini usalama wa kimahakama kwa ajili ya raia wote, na ambayo inamzuia mtu kutumia ubaguzi, jinsia, dini na kadhalika, kuwafanyia ukatili au mienendo mibaya watu wengine, imetajwa kuwa falsafa ya utungaji sheria. Suala hilo limepewa umuhimu na kusisitizwa na Imam Khomein na ni kwa ajili hiyo ndio maana katika katiba ya Iran, usalama wa kimahakama wa raia umepewa umuhimu na watunga sheria, ambapo kudhaminiwa kwake ni jukumu la vyombo vya mahakama. Kwa ibara nyingine ni kwamba, usalama wa kimahakama wa raia ni moja ya haki muhimu za kiraia ambazo serikali imeahidi kuzitekeleza na ndio maana katika katiba kukatengwa faslu maalumu kwa anwani ya 'Haki za Raia' ili kupitia faslu hiyo mihimili yote iweze kuzingatia haki hizo kama ambavyo vyombo vya mahakama navyo vinatakiwa kuzisimamia. Katika faslu hiyo ya 'Haki za Raia', kumebainishwa wazi kwamba raia wote wa Iran bila kujali kaumu na makabila yao, wako sawa katika ugawaji wa haki bila kuzingatia rangi, kizazi, lugha na mfano wa hayo. Kipengee cha baada ya hapo kinaashiria kwamba, watu wote wa taifa hili kuanzia wanawake na wanaume wako sawa mbele ya sheria. Kadhalika kipengee cha 22 kinabainisha kwamba, heshima, mali, nafsi, haki, makazi na kazi za watu zinapaswa kulindwa, isipokuwa pale sheria itakavyoainisha vinginevyo.
**********
Moja ya maudhui ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na wa karibu na haki na usalama wa kimahakama wa wananchi, na ambayo inatambuliwa rasmi na daima kufuatiliwa na wapigania uhuru duniani, ni suala la kutofuatilia na kudadisidadisi itikadi za watu. Kwa bahati mbaya, katika historia ya mwanadamu kumeripotiwa matukio mengi ambayo yanaonyesha mienendo iliyo kinyume cha haki za kimsingi za mwanadamu sambamba na kukanyaga thamani zote za kimaadili na kibinaadamu za watu wasio na hatia kwa kosa tu la wao kuwa na itikadi fulani. Katika uwanja huo wahanga hukamatwa na kuteswa kidhalimu sambamba na kutolewa hukumu kandamizi dhidi yao. Kipengee cha 23 cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunabainisha kwamba ni marufuku kudadisi na kufuatilia itikadi ya mtu na kwamba hakuna mtu anayepasa kunyanyaswa, kushambuliwa au kutuhumiwa kutokana na itikadi yake.
Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 12 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.