Dec 04, 2018 09:03 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 802. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 36 ya Ya-Sin, katika darsa hii tutaanza kuizungumzia sura ya 37 ya Ass 'Affat. Sura hii iliteremshwa Makka; na kama zilivyo sura nyingine za Makka, badala ya hukumu na maamrisho ya dini, imetilia mkazo zaidi masuala ya kiitikadi na matukio yaliyojiri katika harakati za Mitume waliotangulia za kupambana na shirki na ukafiri hususan kisa cha Nabii Ibrahim (as) cha kuyavunja masanamu ya watu wa kaumu yake. Suratu-Ss 'Affat imekemea pia imani potofu kuhusiana na majini na malaika. Baada ya utangulizi huo mfupi, sasa tunaianza darsa yetu ya leo kwa kutoa tarjumi na maelezo ya aya tano za sura hiyo ambazo zinasema:

وَالصَّافَّاتِ صَفًّا

Naapa kwa wanao jipanga kwa safu.

فَالزَّاجِرَاتِ زَجْرًا

Na kwa wenye kuzuia sana mabaya.

فَالتَّالِيَاتِ ذِكْرًا

Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.

إِنَّ إِلَـٰهَكُمْ لَوَاحِدٌ

Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni (Mungu) Mmoja.

رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَرَبُّ الْمَشَارِقِ

Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote.

Sura hii inaanza kwa viapo kadhaa ili kumfanya mtu awe na mazingatio maalumu. Bila shaka Mwenyezi Mungu SW hana haja ya kuapa; na kimsingi waja wake walio waumini wanayaamini na kuyakubali maneno yake bila ya kufuatanishwa na kiapo chochote kile. Lakini kuapa kwa Allah SW ni kiashiria cha adhama na umuhimu wa maudhui anayoiapia na kutaka ipewe umuhimu na mazingatio maalumu. Katika aya hizi tulizosoma, Mwenyezi Mungu analiapia kundi moja la malaika walio na jukumu la kufikisha wahyi wa mbinguni wa Mola kwa Mitume na kuzuia watu na mashetani wasiingilie kati kutaka kuongeza yao ndani ya wahyi huo wa Allah, ili kuhakikisha Mitume wanaupokea ujumbe huo wa Mola kwa usahihi na kwa ukamilifu na kuwafikishia watu. Sifa maalumu ya kwanza waliyonayo malaika hao ni harakati yao ya kujipanga kwenye safu zenye nidhamu maalumu, kiasi cha Allah SW kuiapia adhama ya nidhamu hiyo ya safu za malaika hao. Ni wazi kwamba sisi wanadamu hatuna tajiriba kuhusiana na malaika hata tuweze kudiriki na kuielewa nidhamu yao hiyo makini; lakini upangaji safu ni jambo linaloashiria nidhamu na utayarifu wa kiwango cha juu kabisa. Kama ambavyo safu za vikosi vya jeshi huwa zinajenga nidhamu maalumu katika harakati ya askari na kuwaweka tayari kutekeleza amri za makamanda wao. Malaika walio kwenye safu zenye nidhamu kamili na waliotayari kutekeleza maamrisho ya Allah, wanaondoa kila kizuizi cha kutaka kukwamisha jambo hilo na kuhakikisha amri waliyopewa na Mola wanaitekeleza. Baada ya viapo hivyo Qur'ani tukufu inasema: Mola wa mbingu na ardhi na viumbe wote ni Mungu mmoja tu, wala hana mshirika yeyote katika ulimwengu. Si yeyote miongoni mwa malaika na majini wala viumbe wengine wa mbinguni na ardhini ambao wana nafasi yoyote ile katika uumbaji, uendelezaji na uendeshaji wa ulimwengu. Yeye Allah si Mola Muumba tu, lakini tadbiri na uendeshaji wa masuala ya viumbe wote na mfumo unaotawala mambo yao uko kwenye mamlaka yake. Nukta nyingine iliyoashiriwa katika aya hizi ni kwamba kuna mashariki au mawio kadhaa katika sayari hii ya dunia kwa jua kuchomoza kila siku katika wakati na mahali tofauti na kwa kipindi maalumu kinachotafautiana na siku ya kabla yake. Mabadiliko haya ya kila siku yanafanyika kwa nidhamu maalumu na kwa mujibu wa mahesabu kamili yaliyoratibiwa. Mabadiliko yote haya yanafanyika kwa tadbiri na uendeshaji wa Allah, ambaye ameziwekea kila moja kati ya sayari ya dunia na jua njia na mzingo wake; na kila moja inazunguka kupitia kwenye mzingo huo kwa kasi maalumu, ambapo matokeo ya harakati hizo zilizonadhimiwa ni kupatikana mashariki na magharibi au mawio na machweo kadhaa ya jua katika pande tofauti za sayari ya dunia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa na nidhamu katika mambo ni moja ya masuala muhimu yanayotiliwa mkazo na dini na ambayo huwezesha kupatikana nguvu na umoja pamoja na kasi ya ufanyaji kazi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa siku zote huwepo na vizuizi katika harakati ya kufikia lengo ambavyo inapasa zifanyike juhudi na bidii bila kuchoka za kuviondoa hadi kufikia lengo lililokusudiwa. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Allah SW ni Muumba wa ulimwengu na pia ni mwendeshaji wa masuala yote ya ulimwengu huo. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba ulimwengu na kila kilichomo ndani yake viko chini ya uendeshaji wa Mungu mmoja tu. Na kwa hakika nidhamu na uratibu uliopo baina ya mbingu na ardhi pamoja na viumbe vingine duniani ni ishara bora na tosha ya kuthibitisha upekee wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 6 ambayo inasema:

إِنَّا زَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِزِينَةٍ الْكَوَاكِبِ

Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota.

Baada ya aya zilizotangulia kutilia mkazo upekee wa Mola, Muumba wa mbingu na ardhi, aya hii inasema: Sisi tumeipamba kwa nyota mbingu iliyoko juu ya vichwa vyenu, ambayo ni mbingu ya karibu zaidi na nyinyi. Ukweli ni kwamba maisha, katika miji yenye pirikapirika na hekaheka kubwa na kufurika idadi kubwa ya watu, yamewafanya wanadamu wa leo wanaoishi kwenye mazingira yaliyotawaliwa na mwanga wa mataa ya mabarabarani, majumbani, madukani na maeneo mengine ya miji katika nyakati za usiku, washindwe kuziona nyota angani. Lakini katika usiku wa giza nene kwenye maeneo ya mashambani na uandani mbingu huwa na mandhari ya kuvutia mno ya kuwaduwaza na kuwastaajabisha watu. Ni mandhari jamili na yenye adhama pia. Ni kama kwamba kupitia aya hii, Mwenyezi Mungu amezifananisha nyota na taa zinazotumika kupamba kwenye mijumuiko ya sherehe. Nyota ambazo, nyingi zao zinameremeta kwa kuwaka na kuzima kutoka masafa ya mbali huku nuru na mwanga wa baadhi ya nyengine ukiwa ni thabiti na wa kuendelea. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kupenda mapambo na jamali ni miongoni mwa hisia za kimaumbile za mwanadamu. Kwa hivyo kuneemeka na mapambo na mandhari jamili za maumbile ni jambo linalokubaliwa na Qur'ani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, uzuri wa kuvutia wa mbingu na nyota ni ishara ya qudra na adhama ya Mola Muumba wa ulimwengu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutafakari juu ya mbingu na nyota na kutafiti na kutalii kwa kina kuhusu maumbo hayo ni moja ya fani za elimu ambazo wanafikra na wanasayansi wa dini ya Uislamu walikuwa daima wakizitilia mkazo maalumu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 802 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuzidishie maarifa ya kumtambua na kuzidi kuzielewa na kuzishukuru neema alizotujaalia, zilizotuzunguka katika maisha yetu ya kila siku. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags