Dec 19, 2018 10:15 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 803, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 7 hadi ya 10 ambazo zinasema:

وَحِفْظًا مِّن كُلِّ شَيْطَانٍ مَّارِدٍ

Na kuilinda na kila shet'ani muasi.

لَّا يَسَّمَّعُونَ إِلَى الْمَلَإِ الْأَعْلَىٰ وَيُقْذَفُونَ مِن كُلِّ جَانِبٍ

Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande.

دُحُورًا ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ وَاصِبٌ

Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu.

إِلَّا مَنْ خَطِفَ الْخَطْفَةَ فَأَتْبَعَهُ شِهَابٌ ثَاقِبٌ

Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng'ara.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amezifanya nyota mbinguni kuwa pambo, ambapo wakazi wa sayari ya dunia wanaburudika kuangalia jamali na uzuri wa nyota hizo. Aya hizi zinaangazia upande mwingine wa mbingu ambao si wa kimaada na hali yake ya kidhahiri kwa kueleza kwamba: Mashetani hudhamiria kujipenyeza kwenye eneo la faragha ya malaika wa mbinguni ili kufanya udukuzi wa kusikiliza maneno yao na kutenda kinyume na yaliyokusudiwa. Inapasa tubainishe hapa kwamba taarifa na habari za watu wa ardhini ziko kwenye mamlaka ya malaika wa ulimwengu wa juu wanaojadiliana na kuzizungumzia habari hizo; lakini mashetani huwa wanazifuatilia ili wajaribu kunasa siri za ulimwengu wa ghaibu. Lakini kila wanapokaribia kwenye faragha hiyo hushambuliwa na kutimuliwa. Aya hizi ni kama kwamba zinawapa bishara wanadamu kuwa Allah SW hajaruhusu viumbe walioasi miongoni mwa majini, ambao sisi tunawaita mashetani wathubutu kukaribia mahali inapofanyikia tadbiri na uendeshaji wa ulimwengu, ambako washughulikiaji wake ni malaika na kujaribu kufanya udukuzi wa kunasa yasemwayo au hata kutia doa kwa namna yoyote ile kazi ya malaika hao. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Hata kama baadhi ya mashetani wataweza kuvivuka vizuizi vilivyowekwa na kukaribia kwenye faragha ya malaika na kunasa habari fulani hushambuliwa na kuangamizwa papo hapo. Maelezo yanayofanana na haya yamebainishwa pia katika aya ya 17 na 18 za Suratul-Hijr na pia aya ya 5 ya Suratul-Mulk. Tab'an tunapoona Qur'ani, katika dhahiri ya aya tulizosoma, inazungumzia jambo la kuhisika na kushuhudika au kutumia misamiati ya umithilishaji na ushabihishaji, hili ni jambo lenye mjadala kwa mtazamo wa wafasiri wa Kitabu hicho kitukufu. Kwa sababu kuna mambo mengine kadhaa yaliyotajwa ndani ya Qur'ani yanayofanana na hayo; na wafasiri wote wanaitakidi kuwa madhumuni ya Allah SW si ile dhahiri ya maneno yaliyotumika kubainisha vitu vinavyohisika na kushuhudika. Kwa mujibu wa wafasiri, maneno hayo yanatoa ushabihishaji wa kiakili kwa ajili kuelewa kitu kinachohisika. Ni kama yalivyotumika ndani ya Qur'ani maneno kama loho, kalamu, Arshi na Kursiy, au Kiti cha Enzi. Ni wazi kwamba maneno haya yote hayawezi kutabikishwa na kulinganishwa na maana za vitu vya kimaada na vya kidhahiri. Isitoshe, katika aya ya 43 ya Suratul-'Ankabut, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Na hiyo ni mifano tunawapigia watu, na hawaifahamu ila wenye ilimu." Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika ulimwengu wa juu wa malaika kuna siri mbalimbali ambazo mashetani wanataka kuzitambua, lakini Allah hajaruhusu mashetani hao wafanye jambo kama hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa udukuzi au unasaji sauti za maneno ya watu ni kazi ya shetani ambayo imekemewa na kukaripiwa katika mafundisho ya Qur'ani. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, inapasa kuwachukulia hatua watu wanaopeleleza na kuchunguza siri za watu ili kuzitangaza na kuziweka hadharani kwa ajili ya manufaa yao.

Aya ya 11 ya sura yetu ya Ass 'Affat ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu ya leo. Aya hiyo inasema:

فَاسْتَفْتِهِمْ أَهُمْ أَشَدُّ خَلْقًا أَم مَّنْ خَلَقْنَا ۚ إِنَّا خَلَقْنَاهُم مِّن طِينٍ لَّازِبٍ

Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa katika sura hii ya Ass 'Affat, yametiliwa mkazo sana masuala ya kiitikadi, ikiwemo asili ya uumbwaji na maadi. Aya hii ya 11 inamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW kwa kumtaka awaulize wakanushaji wa maadi na kufufuliwa viumbe, vipi wanatilia shaka na kuikana qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kumuumba tena mwanadamu? Hivi kweli kuwaumba tena wao Siku ya Kiyama itakuwa kazi ngumu zaidi au uumbwaji wa mbingu zenye adhama? Wao wanadamu wameumbwa kutokana na udongo na maji. Awe ni mwanadamu wa awali, ambaye aliumbwa moja kwa moja kutokana na mchanganyiko wa udongo na maji, au wanadamu wengine wote waliofuatia ambao chakula chao kinategemea udongo na maji, wote baada ya kufa waterejea tena kwenye mzunguko huohuo wa udongo na wala hawatatoweka moja kwa moja. Leo hii imethibitishwa kwa mtazamo wa kisayansi kwamba sifa maalumu za kimwili za wanadamu wote zinapatikana kwenye chembe mojamoja ya seli zao na kwamba molekuli ya DNA au vinasaba ya kila mtu ni tofauti kabisa na ya mtu mwengine kama zilivyo alama za vidole. Kama ni hivyo inatosha kubakia chembe moja tu ya athari ya kila mwanadamu, ili Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu aitoe chembe hiyo kutoka kwenye tumbo la ardhi na kumuumba mtu mwingine aliye sawa na yule aliyepo sasa duniani. Katika mfumo wa duniani, spamu mmoja ambaye ni chembe ndogo mno kabisa ya shahawa huwa anatunga kwenye fuko la uzazi la mama, na baada ya miezi tisa anazaliwa kiumbe mwanadamu aliyekamilika kimaumbile. Kwa hivyo Siku ya Kiyama pia, kama zinavyochipua mbegu za mimea ardhini, ndivyo chembe ndogo kabisa za athari za wanadamu zitamea ndani ya fuko la uzazi la ardhi na hatimaye wanadamu kamili watatoka kwenye tumbo la ardhi hiyo. Je, tunadhani kujiri hayo ni jambo muhali na lisilowezekana? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuwatupia masuali wakanushaji ni mbinu nzuri ya kuzindua na kuziamsha dhamiri za nafsi zao zilizolala. Katika mfumo wa usomeshaji na ufundishaji pia, tunaweza mara nyingi kutumia mbinu ya uulizaji masuali na ulinganishaji badala ya usomeshaji wa moja kwa moja wa maudhui inayokusudiwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa baadhi ya shaka na ukanushaji unaofanywa kuhusu mustakabali wa mwanadamu na kufufuliwa kwake tena Siku ya Kiyama chanzo chake ni kusahau jinsi kiumbe huyo alivyoumbwa huko nyuma. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 803 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu imani ya yakini ya Siku ya Kiyama, na kwa imani hiyo tuzifanye njema amali zetu na kuwa sababu ya kuwa mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags