Jan 02, 2019 08:38 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 810, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass’Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 69 hadi 71 ambazo zinasema:

إِنَّهُمْ أَلْفَوْا آبَاءَهُمْ ضَالِّينَ

Hakika waliwakuta baba zao wamepotea.

فَهُمْ عَلَىٰ آثَارِهِمْ يُهْرَعُونَ

Na wao wakifanya haraka kufuata nyayo zao.

وَلَقَدْ ضَلَّ قَبْلَهُمْ أَكْثَرُ الْأَوَّلِينَ

Na hakika walikwishapotea kabla yao wengi wa watu wa zamani.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia hali mbaya ya adhabu na mateso watakayokuwa nayo makafiri na waovu motoni. Aya hizi tulizosoma zinasema, sababu ya watu hao kutiwa motoni ni kwamba: Bila ya kupima na kutafakari, wao walizikubali fikra, imani na itikadi za mababa na mababu zao waliopita na kuamua kufuata kibubusa njia na mwenendo wa wazee wao hao, licha ya kufahamu kuwa fikra zao hazikuwa sahihi wala hazikuwa na misingi ya kukubalika kiakili na kimantiki. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Kwa masikitiko, ufuataji huo usio na nadhari umezoeleka na unashuhudiwa katika kaumu na mataifa mbali mbali katika zama zote za historia. Watu wengi huwa wanadhani kwamba mila na desturi na fikra na itikadi walizokuwa nazo waliowatangulia ni sahihi. Na hata kama watabaini kwamba mila na fikra hizo ni za mambo ya uzushi na khurafa huwa hawana uthubutu wa kuzitolea maoni na kutamka hadharani kuwa si sahihi. Kutunza turathi zilizoachwa na waliotangulia maana yake si kuwafuata wao kibubusa na bila ya mantiki. Kama ambavyo, laiti kama mwanadamu angetosheka na elimu na utaalamu wa waliotangulia tu katika sayansi za jarabati, yasingepatikana maendeleo na ustawi wowote katika maisha yake. Kwa maelezo sahihi zaidi ni kwamba, kutunza na kulinda turathi za waliotangulia maana yake ni kudumisha mila na desturi nzuri na zenye faida walizoziacha wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika mafundisho ya Kiislamu taklidi, kwa maana ya kufuata jambo bila ya kuwa na elimu nalo mwenyewe, haijuzu katika masuala ya imani na itikadi. Iwe anaowafuata mtu ni wazee na mababu zake waliopita au mashekhe na maulamaa wanaoheshimika. Kila mtu anatakiwa yeye mwenyewe afanye uhakiki na utafiti kuhusu misingi ya itikadi za dini, ambayo ni Tauhidi, Utume na Ufufuo na kufikia yakini juu ya mambo hayo kwa hoja na mantiki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kwa kufuata mambo kibubusa na bila hoja, mtu hupatwa na hatima mbaya duniani na akhera. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mila na desturi na fikra na itikadi za waliotutangulia inapasa zipimwe kwa mizani ya akili na mantiki, si kwa hisia za jazba na ukereketwa wa kikabila, rangi, asili yao watu n.k.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 72 hadi 74 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا فِيهِم مُّنذِرِينَ

Na hakika tuliwapelekea waonyaji.

فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُنذَرِينَ

Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale walioonywa.

إِلَّا عِبَادَ اللَّـهِ الْمُخْلَصِينَ

Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu walisafishwa. 

Baada ya aya zilizotangulia kueleza kwamba watu waliofuata upotofu watapata adhabu kali ya moto, aya tulizosoma zinasema: Kupotoka watu hao, sababu yake haikuwa ni kutokuwepo Mitume na Manabii; kwa sababu Allah SW amewatuma waja wake wateule kwa watu wa kaumu mbalimbali ili kuwaelekeza kwenye uongofu na kuwatahadharisha na mwisho mbaya wa duniani na akhera. Ijapokuwa Mitume waliopewa vitabu idadi yao ni ndogo, lakini Mitume waliokuwa wakifanya tablighi na kubainisha hukumu za sharia za Mitume hao wakubwa walikuwa wengi mno, kiasi kwamba kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, idadi yao ilikuwa karibu laki moja na ishirini na nne elfu. Moja ya majukumu muhimu ya Mitume ni kuwaelimisha watu na kuwakomboa kwa kuzikata pingu na minyororo iliyozonga nafsi zao ya mambo ya uzushi na khurafa na kuwaweka mbali na shirki, dhulma na ukafiri. Lakini kwa masikitiko, watu wengi hawaijali miongozo na maonyo ya walimu hao wenye huruma, na hivyo wanafikwa na mwisho mbaya duniani na akhera. Tab’an waja waliotakaswa na Allah kutokana na imani na ikhlasi zao, ambao wanamtanguliza Allah peke yake katika kila jambo la maisha yao na daima huwa na hima ya kupata radhi za Mola, wao watafuzu na hawatakuwa na mwisho mbaya. Kama watu hao wenye ikhlasi watafikia daraja ya ukamilifu wa imani na wa kumjua Allah, watapata tunza maalumu ya kuwafanya waepukane na hatari na vishawishi vya kinafsi na vya kishetani. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuna haja ya kuwapa watu wanaofuata upotofu maonyo na indhari ya kujihadhari na Moto wa Siku ya Kiyama, kama inavyopasa kuwatahadharisha na hatari watu wanaoishi ndani ya nyumba iliyo na hatari ya kuungua moto. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ikiwa akthari ya watu katika jamii watakuwa wamepotoka haifai mtu kufuata mkumbo, bali anatakiwa ajitahidi kuwalingania na kuwapa miongozo ya kufuata njia ya haki. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kusoma historia za kaumu zilizopita na kutafakari juu ya hatima zao humjenga na kumpa ibra na mazingatio mtu na kumsaidia katika kupambanua baina ya haki na batili. Vile vile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba ikhlasi katika ibada na kudhihirisha uja kwa Mola huwa sababu ya mtu kufuzu na kunusurika na mwisho mbaya.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 75 hadi 78 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ نَادَانَا نُوحٌ فَلَنِعْمَ الْمُجِيبُونَ

Na hakika Nuhu alituita, na Sisi ni bora wa waitikiaji.

وَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ مِنَ الْكَرْبِ الْعَظِيمِ

Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa.

وَجَعَلْنَا ذُرِّيَّتَهُ هُمُ الْبَاقِينَ

Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia.

وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ

Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye.

Aya zilizotangulia zilieleza kwamba: Mwenyezi Mungu Mtukufu alituma Mitume kwa kaumu mbalimbali zilizopita. Aya hizi zinamzungumzia mmoja wa Mitume hao, yaani Nabii Nuh (AS) ambaye ni mmoja wa Mitume wakubwa wa Allah kwa kueleza kwamba: Pamoja na Nabii Nuh kufanya kazi ya kutumia miaka na miaka kuwafikishia miongozo ya uongofu watu wa kaumu yake na kuwatahadharisha na ukafiri na shirki kwa huruma na upendo, lakini akthari ya watu hao hawakuyajali maneno yake, wakamkadhibisha Mtume huyo wa Allah. Mwishowe Nabii Nuh akapoteza matumaini ya watu wake kuongoka, hivyo akamwomba Allah awaokoe waumini na kuwaangamiza makafiri. Allah alimtakabalia Mtume wake dua aliyomwomba, na tufani na mafuriko makubwa na ya gharika yalikumba kila mahali; na makafiri wote wakaangamizwa. Ni wale waliomwamini Nabii Nuh tu na kusadikisha ahadi aliyowapa na wakaabiri pamoja naye jahazini ndio waliookoka na adhabu ya gharika. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba dua ni njia ya kupatia msaada wa Allah, tab’an kwa watu ambao, wao wenyewe kwanza wametekeleza wajibu wao kwa njia sahihi. Tuelewe kwamba wakati waja wa kweli wa Mwenyezi Mungu wanapotanzwa na mambo, huyashinda na kujikwamua na matatizo yanayowakabili kwa dua na kutaradhia shida yao kwa Allah na katu hawaishii kwenye mkwamo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kubaki au kutoweka kizazi chochote cha wanadamu kuko mikononi mwa Allah. Yeye Mola alimlinda Nabii Nuh na wale waliomwamini na tufani ya kutisha na kuwaangamiza waliokufuru. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, hatimaye waja wema na wamchao Allah huokoka na balaa na msiba wa kuangamiza na kuwa na mwisho mwema duniani na akhera. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 810 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, azipokee dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags