Jan 03, 2019 12:04 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 812 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass’Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 93 hadi 96 ambazo zinasema:

فَرَاغَ عَلَيْهِمْ ضَرْبًا بِالْيَمِينِ

Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia.

فَأَقْبَلُوا إِلَيْهِ يَزِفُّونَ

Basi wakamjia upesi upesi.

قَالَ أَتَعْبُدُونَ مَا تَنْحِتُونَ

Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe?

 وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya!

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Ibrahim (as) alikuwa anangojea apate fursa ya kuwazindua na kuwatoa kwenye usingizi wa mghafala waabudu masanamu wa kaumu yake. Alijaribu kuwafahamisha kwamba masanamu wanayo yaabudu hayana uwezo wa kufanya lolote na kwamba maumbo hayo yasiyo na uhai hayana taathira yoyote katika majaaliwa yao. Kwa hivyo ilipofika siku ya Sikukuu, wakati watu wote walipotoka nje ya mji, alitumia kisingizio cha kuumwa ili abaki ndani ya mji. Katika wakati mwafaka alibeba shoka na kuelekea kwenye maabadi ya masanamu, akayavunja vunja masanamu yote isipokuwa lile kubwa lao. Wakati waabudu masanamu waliporudi mjini macho yao hayakuamini yalichokiona. Miungu yao bandia mikubwa na midogo ilikuwa imevunjwa vunjwa ikiwa imekatwa mikono na miguu. Kutokana na rekodi aliyokuwa nayo Nabii Ibrahim ya kuyasema kwa ubaya masanamu na kitendo cha watu wake cha kuiabudu miungu hiyo bandia, na kwa kuwa yeye hakuandamana nao kwenda nje ya mji, wakawa na yakini kwamba ni yeye ndiye aliyeyavunja masanamu yao. Kwa hivyo walimuendea kwa hasira na ghadhabu na kuanza kumsaili. Lakini bila ya kuingiwa na chembe ya hofu kutokana na hasira na ghadhabu za waabudu masanamu, Mtume huyo wa Allah aliyajibu madai na masuali yao kwa hoja wadhiha na za kimnatiki. Aliwauliza: Mtu gani mwenye akili timamu anakiabudu kile anachokitengeza kwa mikono yake mwenyewe? Kama kitengezwacho kinaweza kuwa muabudiwa, basi mtengezaji wake anastahiki zaidi kuwa maabudu. Kwa hivyo badala ya kuyaabudu masanamu, mwabuduni Mungu na Mola pekee wa ulimwengu, ambaye ndiye aliyeyaumba masanamu haya pia kama ambavyo nyinyi ni viumbe vyake Yeye. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ili kuondoa mambo ya upotofu inatakiwa kupanga mikakati sahihi na kuitekeleza pale inapopatikana fursa mwafaka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika kupambana na shirki na kung’oa mizizi ya mambo ya upotofu, mbali na Mitume kuelimisha, kuonya na kukumbusha, walichukua pia hatua za kivitendo kila walipohisi ni maslaha kufanya hivyo. (Mfano wake ni hatua aliyochukua Nabii Ibrahim dhidi ya masanamu). Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba vitengezwavyo na wanadamu, viwe vitu vya kawaida au vya kisasa vilivyoundwa kwa umahiri na ustadi, vyote hivyo kiuhalisia ni viumbe vya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu kila ubunifu, uvumbuzi na ugunduzi anaofanya mwanadamu unatokana na akili, kipawa na uhodari ambao amejaaliwa na Mola. Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 97 na 98 ambazo zinasema:

قَالُوا ابْنُوا لَهُ بُنْيَانًا فَأَلْقُوهُ فِي الْجَحِيمِ

Wakasema: Mjengeeni jengo, kisha mtupeni motoni humo!

فَأَرَادُوا بِهِ كَيْدًا فَجَعَلْنَاهُمُ الْأَسْفَلِينَ

Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini.

Badala ya washirikina wale kuzingatia, kutafakari na kuyakubali maneno yenye hoja na mantiki ya Nabii Ibrahim, walidhamiria kumuua Mtume huyo ili liwe funzo la ibra na mazingatio kwa wengine. Kwa hivyo wakatengeza tanuri kubwa na refu ambalo ndani yake walilijaza vigogo na kuni na kuwasha moto mkubwa. Kisha wakamchukua Nabii Ibrahim na kumtupa ndani ya moto huo wakiamini kwamba watamuua na kumwondoa moja kwa moja mbele ya macho yao. Lakini kwa irada ya Allah SW tanuri la moto ule likawa mithili ya bustani kwa Ibrahim (as) kwani badala ya kumuunguza, moto ukawa baridi na salama kwake. Washirikina walistaajabu na kupigwa na butwaa walipomwona Nabii Ibrahim anatoka kwenye macheche ya moto mkali salama u salimini na hivyo kuzima njama na nia yao ovu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba shirki na ukafiri havina misingi na mashiko wala mantiki na hoja sahihi. Na ndiyo maana washirikina hutumia nguvu na mabavu kukabiliana na tauhidi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika kutekeleza jukumu walilopewa na Mola wao la kuondoa dhulma na ukafiri, waja wa kweli wa Allah huwa tayari kuikabili hatari yoyote inayotishia maisha yao, wala hawahofu hata kuunguzwa kwa moto. Vile vile aya hizi zinatufunza kwamba irada ya Allah ndiyo inayotawala kanuni za maumbile. Kwa hivyo wakati wowote atakapo Yeye Mola huweza kubadilisha athari za vitu vya maumbile, kama alivyouondolea moto uwezo wake wa kuunguza katika kadhia ya Nabii Ibrahim(as).

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 99 hadi 101 ambazo zinasema:

وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَىٰ رَبِّي سَيَهْدِينِ

Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; atakayeniongoza.

رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ

Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema.

فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلَامٍ حَلِيمٍ

Basi tukambashiria mwana aliye mpole.

Baada ya Nabii Ibrahim kunusurika na njama za washirikina wa kaumu yake alihitimisha kazi ya kufikisha ujumbe wa Allah katika ardhi ya Babil. Kwa hivyo akaamua kuhajiri na kuelekea Sham, kwa sababu katika zama zote za historia, eneo hilo lilikuwa ardhi ya Mitume na mawalii wa Allah. Ibrahim (as) alimwomba Mola amwongoze katika kutekeleza jukumu lake. Aidha alimwomba Allah amruzuku mtoto mwema na wa heri ili aje aendeleze kazi yake ya Utume; mtoto ambaye atakuwa mwema na mstahiki kwa hali zote. Allah SW alimtakabalia dua yake, akamtunuku wana wema kama Ismail na Is-haq, ambao wote wawili walikuwa waja wema na watakasifu wakafikia daraja teule ya Utume. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, waja wa kweli humkabidhi Allah usukani wa kuwaongozea njia yao; na Yeye ndiye anayekuwa kusudio la kila harakati  na mambo yao. Humwomba Allah awaongoze katika mambo yao yote na hufanya kila jambo lao kwa kutawakali na kumtegemea Mola wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama tunaamua kufuata njia ya Allah tunatakiwa tuwe na yakini ya kupata utatuzi wa mambo yetu kwa rehma na mwongozo wake Yeye Mola. Kadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, kuomba kujaaliwa kuwa na mtoto mwema ni miongoni mwa dua za Mitume. Na hii yenyewe inaonyesha umuhimu wa kizazi chema na safi na taathira yake kubwa kwa usafi, uzima na usalama wa jamii. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 812 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aturuzuku watoto wema ambao watakuwa sababu ya sisi kukumbukwa na kutajwa kwa wema na heri baada ya kuondoka duniani. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags