Mar 30, 2019 21:56 UTC
  • Jumapili, Machi 31, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 24 Rajab 1440 Hijiria, mwafaka na tarehe 31 Machi 2019 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1433 iliyopita, ngome ya Khaibar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwe wa Mtume Mtukufu (saw). Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakiendeshea njama zao huko Khaibar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui. Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaibar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili. Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa benderea mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda pia, na Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake. Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaibar.

Ngome ya Khaibar

Siku kama ya leo miaka 1101 iliyopita, Abunasr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Iran aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ulioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa. Mwanafalsafa huyo mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya  Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu.

Abunasr Muhammad Farabi

Siku kama ya leo miaka 423 iliyopita yaani tarehe 31 Machi mwaka 1596, alizaliwa Rene Descartes mwanafalsafa, mwanahisabati na mwanafizikia wa Kifaransa. Descartes alifikia daraja ya uhadhiri wa Chuo Kikuu baada ya kuhitimu masomo ya falsafa na hisabati. Aidha msomi huyo wa Kifaransa kipindi fulani alifanya safari katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika taaluma nyinginezo. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.

Rene Descartes

Siku kama ya leo miaka 228 iliyopita alifariki dunia Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Uluum, mtaalamu wa elimu ya irfan na msomi mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1155 Hijiria katika mji mtukufu wa Karbala Iraq na kusoma elimu za dini ya Kiislamu katika mji huo kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa zama hizo pamoja pia na wasomi wengine. Aidha akiwa kijana, Allamah Bahrul-Ulum alifanikiwa kukwea daraja za juu za elimu na kufikia ijtihadi na baada ya hapo akaelekea mjini Najaf. Akiwa mjini hapo haraka alifikia daraja ya umarjaa sambamba na kuteuliwa kuwa mkuu wa hauza ya kielimu mjini hapo huku akileta mabadiliko katika hauza hiyo kongwe. Kadhalika msomi huyo alijishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii na ni kwa ajili hiyo ndio maana alipendwa sana na watu. Aidha Sayyid Bahrul-Ulum alipata kuishi miaka saba mjini Mash’had, Iran na miaka miwili huko Hijaz, Saudia ambapo pia aliendelea kujishughulisha na kazi za kielimu kiasi cha kumfanya imam wa msikiti wa Makkah wakati huo, kujiunga na madh’hab ya Kishia. Aidha aliwalea wanafunzi, bila kusahau kazi ya kufafanua vitabu. Maulama kama vile Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa, Mulla Ahmad Naraqi, Muhammad Baqir Shafati, Sayyid Muhammad Jawad Aamili…ni baadhi ya wanafunzi wa Sayyid Bahrul-Ulum. Vitabu vya ‘Al-Maswaabih’ ‘Mishkaatul-Hidaayah’ ‘Fawaaidulr-Rijaaliyah’ na diwani ya mashairi ni miongoni mwa athari za msomi huyo.

Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Uluum

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, garimoshi lililokuwa likitoka Cairo Misri likielekea katika bandari ya Haifa huko Palestina lililipuliwa kwa bomu, ikiwa ni katika kuongezeka mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina yaliyokuwa yakifanywa na Wazayuni maghasibu. Wapalestina 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa na kundi moja la Kizayuni. Siku nne kabla ya mlipuko huo, garimoshi jingine lililipuliwa huko Palestina na Wazayuni wenye silaha, na kuuwa Wapalestina 24 na kuwajeruhi wengine 61.

Na katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisimamisha uanachama wa Misri katika jumuiya hiyo na nchi nyingi wanachama zikakata uhusiano wao na Cairo. Nchi za Kiarabu zilionesha radiamali hiyo kali kwa Misri baada ya rais wa zamani wa nchi hiyo Anwar Sadat kusaini hati ya mapatano ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Januari mwaka 1978.