Apr 06, 2019 21:53 UTC
  • Jumapili, tarehe 7 Aprili, 2019

Leo ni Jumapili tarehe Mosi Sha'aban 1440 Hijria ambayo inasadifiana na Aprili 7, 2019 Miladia.

Leo ni tarehe Mosi Sha'aban. Mwezi wa shaabani unaoanza leo ni mwezi wa ibada, kujipinda na kuomba maghufira. Mtume Muhammad (saw) aliutukuza mno mwezi huu na kuuita kuwa ni mwezi wake. Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake waliusia mno kufanya ibada hususan kufunga swaumu katika mwezi huu wa Shaabani kwa sababu ndio unaotayarisha uwanja mzuri wa kuingia kwenye mwezi wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na wenye baraka tele wa Ramadhan. Katika mwezi huu wa Shaabani kumetukia mambo mengi muhimu kama kuzaliwa Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw) na pia tukio la kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.

Mtume SAW amesema: Sha'aban ni mwezi wangu, Mwenyezi Mungu ampe rehma atayesaidiana na mimi katika mwezi wangu

Siku kama ya leo miaka 1044 iliyopita, Khwaja Abdullah Ansari, faqihi, malenga na mwanairfani wa karne ya tano Hijiria, alizaliwa mjini Herat, magharibi mwa Afghanistan. Alianza kujifundisha mashairi akiwa na umri mdogo ambapo alionyesha kipawa chake na akili ya hali ya juu katika uga huo. Baadaye alijifundisha elimu za dini ya Kiislamu kama vile tafsiri ya Qur'an, fiqhi, hadithi na theolojia. Wakati huo alitokea kuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan huku akitambuliwa kwa lakabu ya jina la mzee wa Herat. Khwaja Abdullah Ansar ameacha athari mbalimbali kwa lugha ya Kiarabu na Kifarsi kama vile 'Munaajaat Nomeh' 'Mahabbat Nomeh' na 'Zaadul-Aarifina.' Aidha aliandika tafsiri kwa uga wa fasihi na Irfan iliyopewa jina la 'Kashful-Asraar' ambayo ilikuwa ya mfumo mpya kabisa katika tafsiri. khwaja Abdullah Ansari alifariki dunia mwaka 481 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani Bi Annemarie Schimmel. Bibi Schimmel alipendelea mno kufanya utafiti na kupata maarifa kuhusu ustaarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prf. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki. Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu. Profesa. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu".

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya baraza la kwanza la dunia la afya na kuandika hati ya kwanza ya mkutano wa kimataifa wa afya. Baraza hilo pia lilichukua uamuzi kwamba tangu mwaka 1950 tarehe 7 Aprili itakuwa Siku ya Kimataifa ya Afya. Tangu mwaka huo tarehe 7 Aprili kila mwaka imekuwa ikiadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Afya.

Matibabu vijijini

Na siku kama ya leo miaka 55 iliyopita mwafaka na tarehe 18 mwezi Farvardin mwaka 1343 Hijria Shamsiya, Imam Khomeini (MA) Kiongozi na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliachiwa huru kufuatia malalamiko na mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran. Usiku wa tarehe 15 Khordad mwaka 1342 Hijria Shamsia vikosi vya usalama vya utawala wa Shah vilimtia mbaroni na kumfunga jela Imam Khomeini baada ya kutoa hotuba iliyokuwa ikifichua maovu ya utawala wa Shah. Wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakitaka kuachiwa huru kiongozi wao. Radiamali kali ya wananchi wa Iran iliulazimisha utawala wa Shah kumwachia huru Imam Khomeini na baadae kumpeleka nyumbani kwake, ambako huko aliwekwa chini ya uangalizi maalumu.

Imam Khomeini (MA)