May 11, 2019 22:09 UTC
  • Jumapili, Mei 12, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 6 Ramadhan 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 12 Mei 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 977 iliyopita, yaani tarehe 6 Ramadhan 463 Hijiria, alifariki dunia Allamah Hamza Ibn  Abdul-Aziz Dailami, maarufu kwa jina la Sallar Dailami, mmoja wa wataalamu wa kubwa wa sheria za Kiislamu (fiqhi). Sallar Dailami alifariki dunia mjini Tabriz, moja ya miji ya kaskazini magharibi mwa Iran. Alikuwa ni mkazi wa mji wa Tabaristan, kaskazini mwa Iran huku lakabu yake ikiwa ni Abu Ali. Aidha Sallar alikuwa ni mmoja wa wanafunzi mashuhuri wa Sheikh Mufid na Sayyid Murtadha Alamul-Huda. Athari mashuhuri ya msomi huyo ni kitabu cha 'Al-Maraasimul-Alawiyyah wal-Ahkaamun-Nabawiyyah' pamoja na kitabu kingine kinachoitwa 'jawaamiul-Fiqhi.' Aidha miongoni mwa athri nyingine za Allamah Hamza Ibn  Abdul-Aziz Dailami ni kitabu kinachoitwa 'Al-Abewaab wal-Fusuul' na 'At-Taqriib.'

Kaburi la Allamah Sallar Dailami

Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, alizaliwa Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko Florence nchini Italia. Nightingale aliyejulikana kwa jina mashuhuri la 'mwanamke mwenye taa mkononi' alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya 'mwanamke mwenye taa mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa pia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi za nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka bila shaka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba alikuwa kipofu mwishoni mwa umri wake ambapo hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910 Milaadia.

 

Florence Nightingale

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, Berlin mji mkuu wa Ujerumani iligawanywa katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia kati ya serikali nne zilizoiteka Ujerumani, mji huo uligawanywa na kudhibitiwa na serikali za Russia, Ufaransa, Uingereza na Marekani. Muda mfupi baadaye mji huo ukadhibitiwa na Urusi ya zamani. Harry Truman rais wa wakati huo wa Marekani alichukua uamuzi wa kuvunja mzingiro na udhibiti huo wa Urusi. Katika kutekeleza hatua hiyo Marekani ilikaribia kupigana vita na Urusi. Matokeo mengine ya hali hiyo ilikuwa ni kugawanywa Ujerumani katika sehemu mbili za Ujerumani Magharibi na Mashariki.

Ukuta uliotumika kuugawa miji hiyo

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, na kwa mujibu wa azimio nambari 278 la Umoja wa Mataifa nchi ya Bahrain ilitengwa na ardhi ya Iran. Kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo ndogo iliyo katika Ghuba ya Uajemi ilikuwa katika utawala wa Iran na baada ya kubuniwa utawala wa Kiislamu ikawa inadhibitiwa na makhalifa wa Kiislamu. Mwanzoni mwa karne ya 7 Hijiria kwa mara nyingine tena nchi hiyo iliunganishwa na Iran na baada ya hapo ikawa chini ya himaya ya Uingereza. Licha ya hayo Iran iliendelea kudai udhibiti na utawala wake kwa Bahrain na kulalamikia vikali hatua ya Uingereza ya kuitawala nchi hiyo.

Bendera ya Bahrain

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, yaani tarehe 22, Ordibehesht, mwaka 1364 Hijria Shamsia, makumi ya watu waliuawa shahidi na kujeruhiwa kutokana na shambulizi la bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la Munafiqiin (MKO) mjini Tehran. Mripuko huo mbali na kusababisha uharibifu mkubwa, uliteketeza kikamilifu jengo moja la ghorofa mbili na karakana ya ufumaji nguo katika barabara ya Naser Khosro na kuua watu 9 na kujeruhi wengine 45. Katika hujuma hiyo ya kigaidi, magaidi wa MKO walitumia bomu lililokuwa na mada za milipuko za TNT zilizokuwa na uzito wa pauni 50. Kundi hilo la kigaidi limekuwa likifanya mashambulizi ya aina hii hapa nchini kwa shabaha ya kupiga vita Mfumo wa Kiislamu na kudhoofisha usalama wa taifa. Mauaji hayo ya kinyama kwa mara nyingine tena yaliidhihirishia dunia jinai za kutisha za kundi la kigaidi la MKO, lenye kuungwa mkono na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni.

Baada ya kujiri shambulio hilo

Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, tetemeko kubwa la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.9 kwa kipimo cha rishta, liliukumba mji wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China. Katika tetemeko hilo la kutisha, watu wapatao 87,000 walifariki dunia na wengine laki tatu na 80,000 kujeruhiwa. Aidha tukio hilo la kutisha liliwaacha bila makazi mamilioni ya watu nchini China. Zilzala hiyo inahesabiwa kuwa moja ya mitetemeko mikubwa ya ardhi iliyowahi kuikumba China katika miongo mitatu iliyopita.

Tetemeko la ardhi lililotokea katika eneo la Sichuan kusini magharibi mwa China