May 15, 2019 04:07 UTC
  • Jumatano, tarehe 15 Mei, 2019

Leo ni Jumatano tarehe 9 Ramadhan 1440 Hijria, inayosadifiana na tarehe 15 Mei 2019.

Siku kama ya leo yaani tarehe 25 Odebehesht 1398 Hijiria Shamsia, ni siku ya kumuenzi mtaalamu wa fasihi 'Abulqasim Firdousi' na malenga mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 319 au 320 Hijiria Shamsia mjini Tous, kaskazini mashariki mwa Iran. Kujulikana duniani kwa Firdousi kulitokana na diwani yake ya mashairi. Alianza kusoma mashairi akiwa kijana mdogo ambapo hadi mwishoni mwa umri wake alijikita katika kuboresha fani yake hiyo. Miongoni mwa athari muhimu za malenga huyo wa Kiirani ni kitabu alichokipa jina la "Shahnameh Ferdowsi". Kitabu hicho kilichosheheni historia ya jadi na utamaduni wa Iran kabla ya ujio wa Uislamu, kimefasiriwa katika lugha mbali mbali. Inasemekana kwamba Firdousi alisoma mashairi kwa muda wa miaka 30.

Abulqasim Firdousi

Siku kama ya leo miaka 243 iliyopita ilitengenezwa meli ya kwanza yenye kutumia mvuke. Meli inayotumia nishati ya mvuke ilitengenezwa miaka 70 baada ya kuvumbuliwa nishati ya mvuke na mhandisi wa Kifaransa Denis Papin. Utumiaji wa nishati ya mvuke katika meli ulileta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa baharini.

Meli ya Mvuke

Siku kama ya leo miaka 160 iliyopita alizaliwa Pierre Curie msomi na mwanafizikia wa Ufaransa. Kipaji cha masomo ya hesabati na fizikia alichokuwa nacho kilianza kuonekana tokea ujana wake, na hatimaye kuibuka kuwa mtafiti mkubwa katika nyanja hizo. Mwaka 1898 mwanafizikia huyo wa Kifaransa alifanikiwa kugundua Radium akisaidiana na mkewe Bi. Marie Pierre. Pierre Curie aliaga dunia mwaka 1906.

Pierre Curie

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, alizaliwa Arthur Schnitzler mwandishi wa visa wa nchini Austria. Bibi na babu wa Arthur walikuwa matabibu na kutokana na hali hiyo, yeye pia akasomea taaluma hiyo na kufanikiwa kupata shahada katika uga huo. Hata hivyo aliachana na taaluma hiyo na kujiunga na taaluma nyingine aliyokuwa akiipendelea, yaani ya uandishi. Arthur Schnitzler pia alikuwa na ujuzi katika masuala ya kisaikolojia ambapo aliandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Kasuku wa Kijani' 'Ardhi Pana' na 'Kuruka Kuelekea Kwenye Giza.' Arthur Schnitzler alifariki dunia mwaka 1931 Miladia.

Arthur Schnitzler

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani. Ayatullah Bahari Hamadani alikuwa mmoja wa maulama wakubwa na mtaalamu mashuhuri wa elimu ya Irfan wa karne ya 13 na 14 Hijiria wa nchini Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali, Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani alielekea mjini Najaf, Iraq na baada ya kukamilisha masomo yake alijishughulisha na kazi ya ufundishaji. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Tadhkiratul-Muttaqiina.'

Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1919 mji wa Izmir moja ya miji ya kihistoria na muhimu nchini Uturuki, ulitekwa na wanajeshi wa Mustafa Kamal Pasha, mwasisi wa Jamhuri ya Uturuki, baada ya kujiri mapigano yaliyopelekea kuuawa watu wengi. Izmir iko magharibi mwa Uturuki, na harakati ya Warepublican ya Uturuki ilianzia katika mji huo wa kihistoria.

Mji wa Izmir

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, jeshi la Ujerumani liliivamia na kuikalia kwa mabavu nchi ya Uholanzi baada ya shambulio kubwa lililodumu kwa siku 5 katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani walianza kuzishambulia nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxemburg huko magharibi mwa Ujerumani tangu tarehe 10 Mei na kufanikiwa kuzidhibiti nchi zote hizo. Uholanzi ilijipatia uhuru mwaka 1945.

Uvamizi wa jeshi la Ujerumani dhidi ya Uholanzi