May 16, 2019 21:58 UTC
  • Ijumaa, Mei 17, 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 11 Ramadhani, mwaka 1440 Hijria, inayosadifiana na tarehe 17 Mei, mwaka 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 587 iliyopita, yaani tarehe 11 Ramadhani mwaka 853 Hijria Qamaria, aliaga dunia mjini Cairo Misri, Ibrahim Karaki, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na hadithi wa Kiislamu. Baada ya kusoma Qur'an na masomo ya awali ya kidini Ibrahim Karaki alianza kufanya safari mbalimbali katika vituo vya elimu ya kidini kwa lengo la kukamilisha masomo yake ya juu kama vile fiqihi na fasihi ya lugha ambapo alifanikiwa kufikia daraja ya juu katika uwanja huo. Kitabu cha I'rabul-Mufasil ni moja ya athari zilizoachwa na msomi huyo.

Ibrahim Karaki

&&&&&&&&&&

Miaka 270 katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 17 Mei mwaka 1749 Miladia, alizaliwa nchini Uingereza Edward Jenner. Tabibu huyo Muingereza alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Kuanzia hapo ugonjwa huo wa ndui uliweza kutibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. Na ilipofika mwaka 1979 maradhi hayo yaliweza kutokomezwa kabisa duniani. 

Edward Jenner

&&&&&&&&&&

Miaka 80 iliyopita katika siku kama ya leo, dola la Uingereza ambalo Palestina ilikuwa chini ya mamlaka yake, lilitoa kitabu kwa jina la "Kitabu Cheupe" na hivyo kukawa kumepigwa hatua nyingine katika njia ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel. Wapalestina ambao walikuwa wakifahamu vyema himaya ya Uingereza kwa Wazayuni, waliukataa mpango uliokuwa umependekezwa katika kitabu hicho kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.

&&&&&&&&&&

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, yaani tarehe 17 Mei mwaka 1865, mkataba wa kwanza wa kimataifa kuhusiana na mawasiliano ulitiwa saini mjini Paris na wawakilishi wa nchi 20 duniani na kuasisiwa Taasisi ya Kimataifa ya Telegrafu. Kwa sababu hiyo siku ya leo imepewa jina la 'Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano.'

Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano

&&&&&&&&&&

Na siku kama ya leo miaka 10 iliyopita mwafaka na tarehe 27 Ordibehesht mwaka 1388 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Muhammad Taqi Bahjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.

Ayatullah Muhammad Taqi Bahjat Foumani