May 28, 2019 21:58 UTC
  • Jumatano, Mei 29, 2019

Leo ni Jumatano tarehe 23 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka 1440 Hijria sawa na tarehe 29 Mei mwaka 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 566 iliyopita sawa na tarehe 29 Mei 1453 ilikombolewa bandari ya Constantine iliyokuwa makao makuu ya Mfalme wa Roma ya Mashariki na vikosi vya Sultani Muhammad Fatih, mtawala wa dola ya Othmaniya. Amri ya kwanza iliyotolewa na Muhammad Fatih baada ya kuudhibiti mji huo ilikuwa ni kudhaminiwa usalama na uhuru wa wakaazi wake. Mfalme huyo alitoa amri ya kukarabatiwa mji huo na kujengwa msikiti, ambao leo hii unajulikana kwa jina la Msikiti wa Sultan Ahmed. Ilipofika mwaka 1930 mji wa Constantine ulibadilishwa jina na kuitwa Istanbul, na ni miongoni mwa miji muhimu zaidi ya Uturuki ulioko magharibi mwa nchi hiyo.

Bandari ya Constantine

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita yaani tarehe 23 Ramadhani mwaka 1392 Hijria Qamaria, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani alikamilisha kazi ya uandishi wa tafsiri kubwa na ya aina yake ya Qur’ani ya al Mizan. Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini zaidi za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri aya za Qur’ani kwa msaada wa aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa na Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa katika lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiingereza na Kihispania.

Allamah Muhammad Hussein Tabatabai

Siku kama ya leo miaka 186 iliyopita sawa na tarehe 23 Mwezi wa Ramadahni mwaka 1254 Hijria Qamaria, ilikamilika kazi ya uandishi wa kitabu cha ‘Jawaahirul-Kalaam’ ambacho kimejumuisha masuala muhimu ya sheria za Mwenyezi Mungu juu ya halali na haramu na kadhalika sheria mbalimbali za dini ya Kiislamu. Ni vyema kuashiria kuwa, kitabu cha Jawaahirul-Kalaam kimebainisha kwa undani masuala mengi ya sheria kiasi kwamba hadi sasa hakuna msomi aliyeweza kuandika kitabu kama hicho. Kunukuu kauli za wasomi wakubwa wa sheria za Kiislamu na kuzitolea ushahidi kwa umakini wa hali ya juu, ni kati ya nukta zinazopatikana katika kitabu hicho. Ayatullah Muhammad Hassan Najafi, mtunzi wa kitabu hicho, alianza kazi ya uandishi wa kitabu cha Jawaahirul-Kalaam akiwa na umri wa miaka 25 huku akitumia karibu muda wa miaka 30 katika uandishi wake na kutokea kuitwa kwa lakabu ya ‘Sheikhul-Fuqahaa.’ Katika kipindi cha maisha yake kulitawala hujuma za fikra potofu za genge la Uwahabi na watu wa kundi la Ikhbariyyun suala ambalo lilimfanya Ayatullah Muhammad Hassan Najafi kuelezea umuhimu wa kuwa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu. Ni baada ya hapo ndipo kukazaliwa fikra ya kuwepo waliyyu Faqihi ‘walii kiongozi' anayesimamia masuala ya sheria za Kiislamu.

Ayatullah Muhammad Hassan Najafi

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita muwafaka na tarehe 29 Mei 1953, Edmund Hillary mpanda milima kutoka New Zealand na Tenzing Norgay mpanda milima kutoka Nepal walifanikiwa kufika kilele cha mlima Everest, ambao ni mlima mrefu zaidi duniani. Mlima wa Everest wenye urefu wa mita 8,848, ni kilele kirefu zaidi cha silsila ya milima ya Himalaya nchini Nepal. Baada ya Hillary na Norgay kufanikiwa kupanda mlima huo mwaka 1953, makundi mengine ya wapanda milima kutoka katika nchi nyingine duniani pia yaliweza kukwea kilele cha mlima huo katika miaka iliyofuata.