May 31, 2019 03:06 UTC
  • Ijumaa, Mei 31, 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 25 Ramadhani 1440 Hijria inayosadifiana na tarehe Mei 31, 2019 Milaadia

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita yaani katika Ijumaa ya mwisho ya Ramadhani ya mwaka 1399 Hijria, Imam Khomeini, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa ujumbe muhimu sana na kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Imam Khomeini aliita siku hiyo kuwa ni ya kuipa uhai mpya dini tukufu ya Kiislamu. Kuanzia mwaka huo hadi leo hii, Ijumaa ya mwisho ya Ramadhani ya kila mwaka huadhimishwa nchini Iran na katika maeneo mengine mengi duniani kwa maandamano makubwa ya Waislamu ya kulaani jinai za wavamizi wa Quds na kutangaza uungaji mkono wao kwa malengo matukufu ya wananchi wa Palestina. Kila mwaka maandamano na maadhimisho hayo hufanyika kwa kufana zaidi kuliko mwaka uliopita. Siku ya Kimataifa ya Quds imepata uungaji mkono mkubwa wa Waislamu kote ulimwenguni na kuthibitisha kuwa kadhia ya Quds na Palestina haiwezi kuamuliwa kwenye vikao vya faragha vya baadhi ya watu kwani Waislamu hivi sasa wameamka kutokana na dhulma kubwa wanayofanyiwa Wapalestina na wameamua kusimama kidete kupambana na utawala dhalimu wa Israel. Katika ujumbe wake huo wa kuanzisha Siku ya Kimataifa ya Quds, Imam Khomeini MA alisema: “Ninawaomba Waislamu na tawala zote za nchi za Waislamu waungane katika mapambano ya kukata mikono ya dhalimu huyu (Israel) na wasaidizi wake na ninawaomba Waislamu wote duniani kuihesabu Ijumaa ya mwisho ya Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa Quds ili kuonesha uungaji mkono wa kimataifa wa Waislamu katika kulinda haki za kisheria za wananchi Waislamu wa Palestina.”

Siku ya Kimataifa ya Quds

 

Siku kama ya leo miaka 1490 iliyopita, sawa na tarehe 31 Mei 529, dini ya Ukristo ilitambuliwa rasmi huko Roma kwa amri ya Constantine, mfalme wa wakati huo wa Roma. Kabla ya hapo Wakristo walikuwa wakifanya ibada kwa siri huko Roma. Mwaka 324 Miladia Mfalme Constantine aliamua kuhamia mji wa Byzantine, mji ambao alikuwa ameutangaza kama mji mkuu wa ufalme wake na uliojengwa na Wagiriki yapata karne nane kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as). Miaka sita baadaye na baada ya kuhamia huko mfalme huyo, ndipo dini ya Ukristo ikatangazwa na kutambuliwa rasmi huku wafuasi wake wakiruhusiwa kuabudu kwa uhuru. 

Ukristo

 

Siku kama ya leo, miaka 187 iliyopita, yaani tareh 31 Mei mwaka 1832 miladia aliuawa Évariste Galois, mtaalamu mwenye kipawa cha hesabati wa Ufaransa.  Évariste Galois alizaliwa katika mji wa Bourg-la-Reine karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris. Hadi kufikia umri wa miaka 12, Galois hakuwa na mwalimu mwengine zaidi ya mama yake. Kuanzia rika la uchipukizi alianza kusoma vitabu vya kiwango cha juu mno vya hesabati na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha ukweli wa hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa. Galois aliuawa akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 Miladia, baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani.

Évariste Galois

 

Na siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, yaani tarehe 31 Mei mwaka 1910 Miladia, nchi ya Afrika Kusini iliundwa katika eneo la kusini mwa Afrika kwa kuunganishwa makoloni mawili ya Uingereza na kupewa uhuru. Muungano huo ulipata uhuru kamili mwaka 1931. Hata hivyo hatamu za madaraka ya nchi ziliingia mikononi mwa wazungu wachache. Lakini hatimaye baada ya mapambano makali ya waafrika kusini wazalendo wakiongozwa na shujaa Nelson Mandela, mnamo mwaka 1991 wazungu makaburu walilazimika kuhatimisha mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid katika nchi hiyo.

Bendera ya Afrika Kusini