Jumapili, tarehe Pili Juni, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 27 Ramadhani 1440 Hijria, sawa na Juni 2, 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 880 iliyopita Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arif na msomi mkubwa wa Kiislamu alizaliwa huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".
Siku kama ya leo miaka 330 iliyopita alifariki dunia Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja wa maulama wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Vitabu vya msomi huyo ni kati ya vitabu muhimu vya marejeo vya maulama wa Kiislamu. Allamah Majlisi alikuwa na uhodari mkubwa katika elimu za dini ya Kiislamu ambapo alifanikiwa kuandika vitabu kadhaa. Katika maisha yake alijishughulisha na kazi ya kuswalisha swala ya Ijumaa, swala za jamaa, kufundisha na kuendeza hadithi za Mtume Muhammad (saw). Vitabu alivyoviandika Allamah Muhammad Baqir Majlisi ni zaidi ya 600, muhimu zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Biharul-Anwaar', 'Hayatul-Quluub' na 'Zaadul-Maad.'
Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita, yaani tarehe Pili Juni mwaka 1882 alifariki dunia Giuseppe Garibaldi, kamanda mzalendo na kiongozi wa vita vya umoja wa Italia. Katika kipindi cha ujana wake Garibaldi alijishughulisha na kazi mbalimbali, ambapo baadaye alijiunga na jeshi. Hatimaye Giuseppe Garibaldi alifanikiwa kuwa kamanda wa wapigania uhuru wa Italia. Garibaldi alifanya juhudi kubwa za kuijenga Italia moja; na kwa sababu hiyo akajulikana katika historia ya nchi hiyo kama shujaa wa taifa.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, mnamo tarehe Pili Juni mwaka 1942 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Mjerumani Marshal Erwin Rommel maarufu kwa jina la Mbwa Mwitu wa Jangwani, alianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Uingereza katika maeneo ya kaskazini mwa Afrika. Kabla ya mashambulizi hayo, Waingereza walikuwa wamefanya hujuma nchini Libya na kuitwaa nchi hiyo kutoka mikononi mwa jeshi la Wajerumani wa Kinazi. Hata hivyo mashambulizi ya jeshi la Erwin Rommel ambayo yalidumu kwa kipindi cha mwezi mmoja yaliwawezesha wanajeshi wake kuidhibiti tena Libya na eneo la al Alamein lililoko kaskazini mwa Misri na karibu na bandari muhimu ya Alexandria. Wajerumani walikaribia kuutwaa mfereji wa kistratijia wa Suez lakini mwezi Novemba mwaka 1942 Waingereza wakafanya mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Erwin Rommel na hatimaye kulishinda.
Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Khordad mwaka 1379 Hijiria Shamsia sawa na Juni Mosi 2001 Milaadia, aliaga dunia Hujjatul Islam Seyyid Ali Akbar Abuturabi, mwanzuoni mwenye mwamko na mwanaharakati wa Iran katika ajali ya gari akiwa na baba yake Ayatullah Seyyid Abbas Abuturabi. Hujjatul Islam Seyyid Ali Akbar Abuturabi alizaliwa mnamo mwaka 1318 Hijiria Shamsia sawa na mwaka 1940 Milaadia, katika mji wa kidini wa Qum nchini hapa. Alijifunza elimu ya dini kutoka kwa maulamama wakubwa akiwemo Imam Khomeini (MA). Kwa mara kadhaa msomi huyo alikamatwa na kuteswa na vibaraka wa Shah katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa. Aidha katika vita vya Iran na Iraq mwaka 1359 Hijiria Shamsia 1981 Milaadia, alikamatwa mateka na askari wa utawala wa Baath wa Iraq na kufungwa kwa miaka 10 katika jela zenye mateso makali za Iraq. Lakini alivumilia kiasi cha kuwa mashuhuri miongoni mwa mateka wa Iran kwenye jela hizo. Alipoachiliwa huru aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya mateka na walioachiliwa huru.