Alkhamisi, tarehe 6 Juni, 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Juni mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita tarehe 16 Khordad 1368 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 6 Jui mwaka 1989 mamilioni ya wananchi wa Iran waliojawa na huzuni waliuzika mwili wa Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, karibu na makaburi ya mashahidi wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran ya Behesht az-Zahra (as), pambizoni mwa mji wa Tehran. Zaidi ya wananchi milioni kumi kutoka miji mbalimbali hapa nchini pamoja na nje ya nchi walishiriki kwenye mazishi hayo ya kihistoria. Kabla ya hapo wananchi wa Iran, waliuaga mwili wa Imam Khomein, katika eneo la Musalla hapa mjini Tehran, na baadaye kuelekea eneo la Behesht az-Zahra kwa ajili ya mazishi.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi dhidi ya ardhi ya Lebanon. Katika uvamizi huo, jeshi la Israel liliuvamia na kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Bairut. Aidha askari hao wa utawala haramu wa Kizayuni, waliharibu miundombinu, viwanda na viunga vya mji huo, sanjari na kufanyya jinai za aina mbalimbali dhidi ya wakazi wake. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa Wazayuni huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Mwezi Septemba mwaka huo huo, jeshi hilo lilifanya mauaji ya umati dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina katika kambi mbili za Sabra na Shatila karibu na mji mkuu wa Lebanona, Bairut. Hata hivyo mwezi Mei mwaka 2000, kufuatia ushindi wa wanamapamgano wa Hizbullah, wanajeshi vamizi wa Israel walilazimika kuondoka kwa madhila katika maeneo yote ya Lebanon waliyokuwa wameyakalia kwa mabavu.
Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita alizaliwa Dakta Ahmed Sukarno mpigania uhuru wa Indonesia. Sukarno alizaliwa mwaka 1901, na alikuwa mstari wa mbele katika mapambano yake dhidi ya mkoloni Mholanzi nchini humo. Kwa minajili hiyo, Sukarno aliwahi kufungwa jela miaka minne na utawala wa kikoloni wa Uholanzi. Baada ya kifungo hicho alitiwa tena mbaroni na kubaidishwa. Mnamo mwaka 1949 alichaguliwa kuwa Rais wa Indonesia na ilipofika mwaka 1965 Ahmed Sukarno aliondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Janerali Suharto.
Siku kama ya leo, miaka 220 iliyopita, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow. Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake. Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru.