Jun 23, 2019 17:21 UTC
  • Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-15

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 15 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Katika kipindi kilichopita tulizungumzia suala la umuhimu wa uhuru ndani ya nchi inayozingatia misingi ya demokrasia. Tukasema kuwa suala hilo lilipewa umuhimu mkubwa na Imam Khomeini (MA).

Moja ya daghaghada za Imam Homeini (MA) hususan katika kipindi cha uongozi wake, ilikuwa ni kubainisha mipaka ya wigo wa uhuru katika Jamhuri ya Kiislamu. Katika uwanja huo mtukufu huyo alikutaja kulinda matukufu ya jamii na kujiepusha na njama kuwa ni katika masharti ya uhuru wa vyombo vya habari na vyama vya kisiasa. Aidha sambamba na kuashiria tajriba ya mwezi wa kwanza tangu kufikiwa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ambapo katika kipindi hicho baadhi ya makundi ya kisiasa yaliyokuwa yameibuka yalikuwa yakitumia vibaya ustawi, Imam Khomeini alisema: "Tumewapa uhuru, uhuru wa moja kwa moja ambao katika kipindi cha miezi kadhaa tu kuliundwa karibu vyama 200 na makundi, idadi kubwa ya vyombo vya habari, magazeti na majarida ambayo yalianza kuchapishwa na hakuna mtu aliyewazuia kufanya hivyo. Aidha licha ya kukiuka matukufu yote…..bado hakuna aliyewanyooshea kidole, hadi pale tulipofahamu kwamba wanahusika na kuibua fitina na wanafanya njama dhidi ya nchi….Madamu njama zenu zimethibiti, basi hatuwezi kuruhusu muwe na uhuru wa kufanya kila mnachokitaka." Hotuba ya tarehe 2/6/1358.

Waandishi wa habari

 

Kadhalika mtukufu huyo alikuambatanisha kuchungwa masuala ya jamii na matukufu ya wanawake na wanaume na uhuru na kuhusiana na hilo  alisema: "Tumefanikiwa kuunda utawala wa uhuru kamili, utawala ujao ni lazima uzingatie maslahi jumla ya jamii na kadhalika ni lazima ufungamane na masuala ya jamii ya Kiirani kwa kuwa uhuru unapasa kutilia maanani heshima ya jamii fulani na ya wanaume na wanawake wa jamii hiyo." Hotuba ya tarehe 22/7/1357. Katika sehemu nyingine Imam Khomeini (MA) anasema: "Katika utawala wa Kiislamu, kutakuwa na uhuru wa wazi na kamili. Isipokuwa tu wananchi hawatopewa uhuru ambao utaenda kinyume na maslahi ya raia na utakaotoa pigo kwa heshima ya watu binafsi." Hotuba ya tarehe 27/10/1357.

*******

Ndugu wasikilizaji, kuzuia kuenea ufisadi katika jamii ni moja ya mistari miekundu ya uhuru ambapo Imam aliamini kwamba, misingi ya Kiislamu haitoi idhini ya kuenezwa ufisadi. Katika uwanja huo Imam Khomeini alisema: "Uhuru uko katika wigo wa sheria. Uislamu umezuia ufisadi na kuhusu hilo umetoa uhuru ambao utakuwa kinyume na ufisadi." Hotuba ya tarehe 7/4/1357. Aidha katika sehemu nyingine anautaja ufisadi, wala njama na waharibifu kuwa chanzo cha kuzuia uhuru kwa kusema:

Vyombo vya habari vilipewa nafasi katika mtazamo wa Imam Khomeini MA

 

"Tutatoa uhuru wa moja kwa moja, tunatoa na tutaendelea kutoa. Lakini si kwa watu wanaokula njama, si kwa ufisadi wala waharibifu." Hotuba ya tarehe 20/2/1358. Imam Khomeini pia alikutaja kutosababisha madhara kwa wananchi na badala yake kuwa na manufaa na maslahi kwa taifa kuwa miongoni mwa masharti ya uhuru na kuhusiana na hilo alisema: "Uhuru ni kwa ajili ya kila mtu maadamu hautalisababishia madhara taifa la Iran." Hotuba ya tarehe 25/10/1357.

*******

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 15 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 Ndugu wasikilizaji moja ya uwepo wa viashiria muhimu vya uhuru wa kisiasa na kijamii katika nadharia ya Imam Khomeini, ni uhuru katika vyuo vikuu na harakati mbalimbali za kiuanafunzi. Itakumbukwa kuwa katika miaka ya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, vyuo vikuu na kwa kuzingatia kuwa vilihesabiwa kuwa moja ya sekta kuu za maandamano na mapambano dhidi ya utawala wa Shah, viliendeshwa kwa ulinzi mkali wa kiusalama na wanafunzi waliokuwa wakishiriki katika maandamano walikuwa wakikabiliwa na adhabu kali na ukatili mkubwa kutoka kwa serikali. Aidha wanafunzi waliokuwa wakipinga siasa za utawala wa Shah, walikuwa wakizuiliwa kuendelea na masomo hata kwa kosa dogo sana sambamba na kutupwa jela huku wakiteswa kwa adhabu mbalimbali ndani ya jela hizo. Kwa hakika hali ya vyuo vikuu ilikuwa ya kutisha na ya kuogofya ambapo hata ukosoaji mdogo wa mwalimu darasani kwa Shah au kwa siasa za utawala wake, ulimpelekea aanze kufuatiliwa, kutiwa mbaroni na kisha kupewa mateso makali. Imam Khomeini sambamba na kukosoa hali hiyo alisisitiza umuhimu wa kuwepo uhuru katika vyuo vikuu, ili heshima ya walimu, wanafunzi na uhuru wa vyuo hivyo iweze kulindwa.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran

 

Akizungumzia hali ya vyuo vikuu katika miaka ya kabla ya Mapinduzi, Imam Khomeini (MA) alisema: “Lau kama vyuo vikuu vingekuwa eneo salama, basi vijana wetu wanaotaka kufanya ukosoaji katika vyuo hivyo wasingekuwa wanazibwa midogo kwa kupigwa wasichana na wavulana sambamba na kuwafunga jela…..Chuo kikuu ambacho kinatawaliwa na mtu mmoja hakiwezi kuwa ni chuo kikuu, bali mazingira ya kielimu ya chuo kikuu yanapasa kuwa huru.” Hotuba ya tarehe 19/10/1356.

*******

Moja ya sifa za tawala za kidemokrasia, ni kuwepo uhuru kwa ajili ya jamii za watu wachache wa kidini, kikaumu (kabila), kilugha sambamba na utawala huo kuzingatia haki za raia wa kawaida. Mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kulitawala swali moja ambalo alikuwa akiulizwa sana Imam kuhusiana na haki ya jamii za walio wachache kidini na kimadhehebu katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Sababu ya kuibuka swali hilo kati ya weledi wa masuala ya kisiasa na waangalizi wa kimataifa, ni kuwepo msingi wa kidini katika mapinduzi hayo huku kiongozi wake akiwa anatokana na marjaa wa Kishia. Licha ya kwamba viongozi wa kidini walikuwa na nafasi kubwa katika jamii na hata ndani ya serikali ya Iran, lakini baada ya kufikiwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ilikuwa ni mara ya kwanza kwao kuongoza nchi katika historia ya uongozi wa kisiasa. Ni kwa msingi huo na kutokana na idolojia ya mapinduzi hayo na pia kukubalika dini ya Uislamu na madhehebu ya Ushia kuwa msingi mkuu wa kifikra na kisiasa wa mfumo unaotawala nchini, ndipo kukazuka wasi wasi mkubwa miongoni mwa weledi wa masuala ya kisiasa kwamba kuingia madarakani viongozi wa kidini nchini Iran, kungehatarisha au kwa uchache kubana uhuru na haki za wafuasi wa dini na madhehebu za waliowachache. Katika kujibu swali kwamba je, jamii za wachache za kidini na kimadhehebu zingepewa nafasi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini alisema: “Utawala wa Shah haukuamiliana vizuri na jamii za dini za walio wachache miongoni mwa Waislamu, sisi bila shaka tutaheshimu zaidi itikadi za wengine. Baada ya kuondolewa madarakani utawala wa kidikteta na kuanzishwa utawala huru nchini, hali ya maisha ya akthari ya Waislamu na jamii za wachache za kidini, itakuwa nzuri.”Hotuba ya tarehe 22/7/1357.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 15 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.