Sura ya S’aad, aya ya 39-43 (Darsa ya 829)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 829 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 39 na 40 ambazo zinasema:
هَـٰذَا عَطَاؤُنَا فَامْنُنْ أَوْ أَمْسِكْ بِغَيْرِ حِسَابٍ
Huku ndiko kutoa kwetu. Basi toa au zuia, bila ya hisabu.
وَإِنَّ لَهُ عِندَنَا لَزُلْفَىٰ وَحُسْنَ مَآبٍ
Naye kwa hakika anao ukuruba na marejeo mazuri kwetu.
Katika darsa kadhaa zilizopita tumezungumzia habari za Nabii Suleiman (as). Aya hizi zinakamilisha kuzungumzia habari za Mtume huyo kwa kusema: Mwenyezi Mungu alimpa Nabii Suleiman utajiri mkubwa na neema nyingi mno na kumtaka autumie utajiri na neema hizo kadiri ya uwezo wake kuwasaidia wahitaji katika jamii na kujitahidi kuwatatulia matatizo yao. Tab’an kwa kuwa Suleiman (as) alikuwa Mtume wa Allah, alifanya mambo kwa msingi wa uadilifu; na katika ugawaji wa at’ia na neema alizojaaliwa na Allah alikuwa akimpatia kila mtu kiwango kinacholingana na mahitaji yake, na si kugawanya neema hizo kiwango sawa kwa watu wote, kwani kufanya hivyo hakuendani na uadilifu. Kisha aya zinaendelea kuashiria mwisho mwema wa mtukufu huyo kwa kusema: Licha ya madaraka, utajiri na neema zisizohesabika alizojaaliwa, Nabii Suleiman hakupungua hata chembe katika kudhihirisha uja wake kwa Mola wake, na hakuwahi hata mara moja kuwaonea au kuwafanyia dhulma watu waliokuwa chini ya mamlaka na utawala wake. Kwa sababu hiyo, alikuwa na hadhi na daraja ya juu mbele ya Allah SW na akaondoka hapa duniani akiwa na mwisho mwema na wa kheri. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika utawala unaofuata sharia za Allah, mtawala huwa anaitakidi kwamba, kila alichonacho ni at’ia na fadhila za Mola, ambazo inapasa zitumike kuwahudumia wananchi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa na utajiri na madaraka hakukinzani na wala hakumzuii mtu kuwa mchaMungu, na mja halisi na mwenye ukuruba kwa Mola wake. Katika utawala wa kidini ustawi na maendeleo ya kimaada na utumiaji suhula na rasilimali za ardhini hakupingani na mtu kuwa na ukamilifu wa kiroho na kimaanawi.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 41, 42 na 43 ambazo zinasema:
وَاذْكُرْ عَبْدَنَا أَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الشَّيْطَانُ بِنُصْبٍ وَعَذَابٍ
Na mkumbuke mja wetu Ayubu. Alipomwita Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika Shet'ani amenifikishia udhia na adhabu.
ارْكُضْ بِرِجْلِكَ ۖ هَـٰذَا مُغْتَسَلٌ بَارِدٌ وَشَرَابٌ
(Akaambiwa:) Piga-piga ardhi kwa mguu wako! Basi haya maji baridi ya kuogea na ya kunywa.
وَوَهَبْنَا لَهُ أَهْلَهُ وَمِثْلَهُم مَّعَهُمْ رَحْمَةً مِّنَّا وَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ
Na tukampa ahali zake na wengine kama wao pamoja nao, kuwa ni rehema itokayo kwetu, na iwe ukumbusho kwa watu wenye akili.
Baada ya aya kadhaa zilizotangulia za sura hii ya S’aad kuzungumzia habari za Nabii Suleiman (as) ambaye ni mfano wa Mitume wa Allah waliojaaliwa kuwa na nguvu kubwa za mamlaka na madaraka na utajiri usio na mfano, aya tulizosoma hivi punde zinaashiria habari za Nabii Ayoub (as), ambaye ni nembo na ruwaza ya subira na uvumilivu usio na mfano katika kukabiliana na masaibu na matatizo. Kwa mujibu wa aya hizi, Bwana Mtume Muhammad SAW alitakiwa awasimulie watu habari za maisha ya Nabii Ayoub, ili wapate somo la subira na istikama ya kuzikabili tabu, misukosuko na matatizo ya binafsi na ya kijamii. Kwa mujibu wa vitabu vya tafsiri ya Qur’ani na Hadithi, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpa neema nyingi mno Ayoub (as); na Mtume huyo, naye pia alikuwa mja mshukurivu wa kweli wa neema za Mola wake. Pamoja na hayo Allah SW alimtahini mja wake huyo kwa mtihani mgumu na majaribu mazito mno ili kuthibitisha kuwa, Ayoub ni mja mshukurivu katika hali zote, iwe ni katika raha na neema au katika tabu na shida. Kwa hivyo mali na utajiri wa Nabii Ayoub (as), ukiwemo wa mashamba na mifugo ya kondoo ukaanza kidogo kidogo kupukutika na kutoweka; na yeye mwenyewe pia akasibiwa na maradhi thakili, mpaka ikafika hadi wanawe wakaamua kujitenga naye, kwa kuchelea wasije na wao pia wakaugua maradhi hayo, akabakia naye mkewe tu aliyeendelea kumthamini kwa kumtunza na kumuuguza. Ilipofika hatua hiyo, shetani akaanza kueneza uvumi kwa watu, kwamba Ayoub (as) amesibiwa na maradhi na kufikwa na mabalaa na misukosuko hiyo kwa sababu ya kumwasi Mwenyezi Mungu; kwani kama angekuwa mja mwema, asingepatwa na mabalaa hayo, mpaka kufika hadi wanawe waamue kumwacha peke yake. Mambo hayo yaliyojiri nyumbani kwa Nabii Ayoub na maneno makali na ya maudhi waliyokuwa wakiyasema watu kutokana na kuchochewa na wasiwasi wa shetani, vilimweka Mtume huyo kwenye hali ngumu mno na kumsababishia machungu na majonzi makubwa. Mtukufu huyo, ambaye katika muda wote wa tabu na misukosuko iliyomfika, hakuwahi kulalama na kusikitika hata mara moja, bali muda wote aliendelea kumshukuru Allah SW, siku moja alimuelekea Mola wake kumshtakia hali ya dhana mbaya iliyokuwa imejengeka ndani ya nafsi za watu juu yake kutokana na kuathiriwa na wasiwasi wa shetani. Lakini katika kufanya hivyo, hakumwomba moja kwa moja Mola wake, jambo lolote lile. Ili kumuokoa Mtume wake na maudhi ya kusemwa vibaya na watu, Allah SW alimwafu na kumpa shifaa ya kimiujiza Ayoub (as), ili watu wote wajue kwamba, mja huyo mteule ni mwenye kurehemewa na Mola wake, na wala hakuwa ameghadhibikwa. Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwamuru Nabii Ayoub pale pale alipokuwa amekaa, apige pige miguu yake juu ya ardhi mpaka ikachimbuka chemchemi ya maji safi na matamu kabisa. Tab’an utokeaji wa chemchemi hiyo ya maji ulifanana na wa kisa cha Ismail, mwana wa Nabii Ibrahim (as). Kwani wakati mke wa Nabii Ibrahim, Hajar alipokuwa amekata tamaa ya kupata maji kwa ajili ya mwanawe mdogo, kwa qudra na uwezo wa Allah, chini ya miguu ya Ismail, aliyekuwa akipiga piga miguu yake ardhini kwa sababu ya kiu kali kando ya Nyumba Tukufu ya Allah ya Al-Kaaba huko Makka, ilichimbuka chemchemi ya maji safi, yaliyokuja kupewa jina la Zamzam, na ambayo yanaendelea kutiririka hadi leo hii. Tukirejea kwenye kisa cha Nabii Ayoub (as), baada ya kuchimbuka chemchemi ya maji, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimtaka Mtume wake huyo akoge kwa maji hayo na kunywa pia ili apate shifaa ya maradhi yake. Ala kulli hal, kutokana na Ayoub kufuzu mtihani aliopewa, alipona kikamilifu maradhi yaliyomsibu. Allah SW alimrejeshea tena neema zake, wanawe wakarudi nyumbani kwake na maisha yake yakanawiri tena kama yalivyokuwa mwanzo. Si hayo tu, Mola Muweza wa kila kitu, alimruzuku watoto wengine pia ili kumkamilishia rehma na fadhila zake. Ni wazi kwamba, kisa cha mchanganyiko wa neema na misukosuko, cha Nabii Ayoub (as) ni somo lenye kutoa ibra na mazingatio kwa wenye busara ili wasiingiwe na ghururi na majivuno kwa neema walizonazo, kwani si hasha zikawaondokea zote ghafla moja. Kisa hiki kinatufunza pia kwamba, tusikate tamaa abadani ya kupata rehma na uraufu wa Allah kutokana na matatizo, shida na maradhi yanayotupata, kwani kuyaondoa yote hayo ni jambo rahisi na jepesi kabisa kwake Yeye Mola. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuelewa historia ya waliotangulia, hasa ya Mitume wa Allah, kuna faida na mafunzo makubwa. Kwa sababu kutambua matatizo na masaibu yaliyowapata watu wengine, huimarisha hali ya subira na uvumilivu ndani ya nafsi ya mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, machungu na masaibu ni uwanja wa kuchezewa na wasiwasi wa shetani. Baadhi ya wakati, shetani huzitumia shida na dhiki ili kumpotosha na kumtoa mtu kwenye njia iliyonyooka. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, kuomba dua ni sira ya mawalii wa Allah na dhihirisho la mtu kuthibitisha ibada na uja halisi mbele ya Muumba wa ulimwengu. Kwa hivyo tuombeni dua kwa ajili ya kuondokewa na masaibu na matatizo tuliyonayo. Vile vile aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kuwa na watoto wengi na ukoo mkubwa ni miongoni mwa neema za Allah SW. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 829 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu subira na azilinde na shari ya wasiwasi wa shetani, pale anapotupa majaribu na kututahini. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/