Jumapili, 08 Septemba, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 8 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria mwafaka na tarehe 8 Septemba 2019 Miladia.
Siku ya leo tarehe 8 Septemba ilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ujinga. Kujua kusoma na kuandika ni miongoni mwa vielelezo vya ustawi katika jamii ya mwanadamu na ujinga husababisha umaskini na kubakia nyuma kimaendeleo. Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa mkakati wa kupambana na kutokujua kusoma na kuandika haukuwa wa kuridhisha katika baadhi ya nchi na hadi sasa idadi kubwa ya watu hawajapata neema hiyo. Nchini Iran baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu kulifanyika jitihada kubwa za kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika kwa kadiri kwamba Disemba mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuasisiwa Harakati ya Kupambana na Ujinga. Taasisi hiyo imepiga hatua kubwa hapa nchini. ***
Tarehe 8 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1380 iliyopiita, maji yalimalizika kabisa katika mahema ya mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia yake katika jangwa lenye joto kali la Karbala. Kharazmi katika kitabu cha Maqtalul Hussein na Khiyabani katika Waqaiul Ayyam wameandika kwamba: Katika siku ya nane ya mwezi Muharram mwaka 61 Imam Hussein na masahaba zake walikuwa wakisumbuliwa na kiu kali, kwa msingi huo Imam Hussein alichukua sururu na akapiga hatua kama 19 nyuma ya mahema kisha akaelekea kibla na kuanza kuchimba ardhi. Maji matamu ya kunywa yalianza kutoka na watu wote waliokuwa pamoja naye walikunywa na kujaza vyombo vyao kisha maji yakatoweka na hayakuonekana tena. Habari hiyo ilipofika kwa Ubaidullah bin Ziad alimtumia ujumbe kamanda wa jeshi la Yazid mal'uuni, Umar bin Sa'd akimwambia: Nimepata habari kwamba Hussein anachimba kisima na kupata maji ya kutumia, hivyo baada ya kupata risala hii kuwa macho zaidi ili maji yasiwafikie na zidisha mbinyo na mashaka dhidi ya Hussein na masahaba zake."
Miaka 256 iliyopita katika siku kama ya leo, baada ya mapigano ya muda mrefu na kwa mujibu wa makubaliano ya Paris, Canada iliondoka chini ya udhibiti wa Ufaransa na kudhibitiwa rasmi na Uingereza. Hata hivyo mivutano baina ya Wacanada wenye asili ya Ufaransa na Waingereza waliokuwa wakiishi Canada iliendelea kwa muda mrefu. Licha ya Canada kujitangazia uhuru na mamlaka ya kujitawala mwaka 1867 lakini nchi hiyo inafuata Uingereza katika mfumo wake wa kisiasa. ***
Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi waliuzingira mji wa Leningrad, Saint Petersburg ya sasa. Hata hivyo mji huo haukutekwa na jeshi la Kinazi licha ya matarajio ya Adolf Hitler na makamanda wake. Wakazi wa Leningrad waliendeleza mapambano ya ukombozi hadi Januari mwaka 1944 wakati walipofanikiwa kujiondoa katika mzingiro wa wanajeshi wa Ujerumani. ***
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa ulinzi wa mataifa ya Asia ya kusini mashariki (SEATO) katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila. Mkataba huo ulitiwa saini na nchi za Marekani, Uingereza, Australia, Pakistan, Thailand, Ufaransa, New Zealand na Ufilipino. Kwa mujibu wa mkataba huo, nchi mwanachama itakapokabiliwa na mashambulio ya kijeshi kutoka nje, uasi na vitisho vya ndani, basi nchi wanachama zinapaswa kuisaidia nchi hiyo kijeshi au kwa kutumia wenzo wa vikwazo.***
Na miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi wa utawala wa kidikteta wa Pahlavi walishambulia maandamano makubwa ya wananchi wa mji wa Tehran na kuua raia wengi. Wananchi Waislamu wakazi wa Tehran siku hiyo walianza kuandamana tangu asubuhi, hayo yakiwa maandamano ya siku kadhaa mfululizo kuwahi kufanywa na wakazi wa mji wa Tehran dhidi ya utawala wa kibaraka wa Pahlavi. Wakati huo, utawala wa kijeshi ulikuwa umetangazwa katika mji wa Tehran, lakini wananchi Waislamu walipuuza hali hiyo na wakamiminika mitaani wakipiga nara dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo huo, walinzi maalumu wa Shah walifanya mashambulizi na katika muda mfupi wakawaua shahidi wananchi zaidi ya elfu nne wa Tehran waliokuwa wakipigania haki zao.***