Sep 16, 2019 11:11 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Sep 16

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....

Voliboli: Iran yazizaba Sri Lanka na Qatar

Timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesonga mbele katika michuano ya kuwania kufuzu Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020, baada ya kuzisasambua Qatar na Sri Lanka katika Mashindano ya Mabingwa wa Voliboli Asia. Hata hivyo timu hiyo ya Iran ilishindwa kufurukuta mbele ya Australia siku ya Jumapili. Katika mchuano huo wa kusisimua uliopigwa katika ukumbi wa ndani wa Uwanja wa Azadi hapa Tehran, Australia waliibamiza Iran seti 3-1 (25–22, 23–25, 21–25, 21–25).

Mashabiki wa timu ya voliboli ya Iran

 

Kabla ya hapo, Iran ilikuwa imeiadhibu vikali Qatar kwa kuilaza (25-18, 25-15, 25-17). Aidha timu hiyo ya voliboli ya Iran iliinyoa bila maji Sri Lanka katika mechi yake ya kwanza, kwa kuitandika seti 3-0.

Iran ipo katika nafasi ya 2 kwenye Kundi A ikitanguliwa na Australia na sasa timu hizo mbili pamoja na China na India zimesonga mbele katika Michuano ya Kufuzu Olimpiki ya Asia 2020.

Karate ya Kimataifa; Iran yaibuka ya 2

Timu ya taifa ya karate ya Iran imeibuka ya pili katika Ligi ya Kimataifa ya Karate mjini Tokyo, Japan. Wanaume na wanawake wa Kiirani walioshiriki mashindano hayo ya dunia wameshinda medali moja ya dhahabu, mbili za fedha na shaba mbili na kutwaa nafasi ya pili nyuma ya mwenyeji Japan. Medali ya dhahabu ya Iran ilitwaliwa na Sara Bahmanyar katika safu ya makarateka wa kike. Japan imeibuka kidedea kwa kuzoa medali nane za dhahabu, tatu za fedha na shaba tisa.

Makarateka wa Kiirani

Jamhuri ya Azerbaijan imefunga orodha ya tatu bora kwa kuzoa medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na moja ya shaba. Makarateka Zaidi ya 600 kutoka nchi karibu 80 duniani wameshiriki mashindano hayo ya World Karate League mjini Tokyo, Japan. 

Kombe la Shirikisho

Klabu ya Azam ya Tanzania imekubali kichapo hafifu cha bao 1 bila jibu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Triangle United ya Zimbabwe. Bao pekee la Triangel United lilifungwa dakika ya 34 na Ralph Kawondera kutokana na uzembe wa safu ya ulinzi wa Azam FC. Licha ya Azam FC kupewa sapoti kubwa na mashabiki waliojitokeza katika Uwanja wa Azam Complex, lakini hilo halikuwafaa kwani safu ya ulinzi ya Triangle United ilikuwa ngumu na ikajilinda na hatari zote. Sasa Azam ina kazi nzito ya kwenda kutafuta matokeo mazuri ugenini kwenye mchezo wa marudiano unaoatarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 27-29 nchini Zimbabwe.

TFF yashitakiwa FIFA?

Aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars, Emannuel Amunike amelishitaki Shirikisho la Soka Tanzania TFF kwa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, kutokana na malikimbikizi ya deni. Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidao Jumamosi hii amesema kuwa kadhia hiyo sio kubwa kama linavyokuzwa na baadhi ya vyombo vya habari, na kwamba TFF tayari imeshamlipa kocha huyo kwa asilimia kubwa ya deni lake na iliyobakia ni kidogo. Shirikisho la TFF liliamua kumtimua Amunike mwezi Julai mwaka huu, baada ya Taifa Stars kuvurunda katika michuano ya AFCON ya mwaka huu nchini Misri. Kutimuliwa kwa Amunike nusra kuibue mvutano kati ya TFF na serikali. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Tanzania, Dkt. Harrison Mwakyembe alisema kuwa kama TFF wameamua kufuata nyayo za Misri katika kumfuta kazi Amunike basi na wao wanapaswa wakamilishe mchakato kwa kujiuzulu nafasi zao.

 Riadha; Kenya haikamatiki

Mwanariadha nyota kutoka nchini Kenya, Geoffrey Kamworor amevunja rekodi ya dunia katika mbio ndefu za Copenhagen Half Marathon, zilizofanyika Jumapili nchini Denmark. Kwenye mbio hizo za kilomita 21, Kamworor alitumia muda wa dakika 57:01, na kuweka rekodi mpya ya kutumia muda mfupi zaidi wa Half Marathon duniani.

Geoffrey Kamworor

Kamworor ambaye ni bingwa mara tatu wa mbio hizo, amevunja rekodi ya Mkenya mwenziwe, Abraham Kiptum ya kukimbia umbali huo kwa dakika 58.01, Ambayo aliiweka katika mbio za Valencia Half Marathon mwezi Oktoba mwaka jana. Tayari Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) limeiweka rekodi hiyo mpya ambayo ilikuwa inashikiliwa na Abraham Kiptum kwa muda wa dakika 58:18.

 

Ligi ya EPL

Klabu ya Norwich City iliyopanda daraja na kujiunga na Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza iliwaacha wengi vinywa wazi baada ya kuwalemea mabingwa watetezi wa ligi hiyo Manchester City. Norwich ilisitisha msururu wa Man City kucheza mechi 18 bila kushindwa katika mechi ya kusisimua wikendi. Shambulio la Kenny Mclean kutoka katika kona liliwaweka kifua mbele wachezaji hao wa Canary baada ya dakika ya 18 ya mchezo, kabla ya kuongeza uongozi wao baada ya dakika 30 wakati walipovamia lango la Man City huku mchezaji Todd Cantewel akifunga la pili. Teemu Pukki aliifungia Norwich City bao la tatu katika dakika ya 50 na kuihakikishia timu hiyo ushindi wa 3-2 dhidi ya Manchester City.

Mabao ya City yalifungwa na Sergio Aguero dakika ya 45 na Rodri Hernández dakika ya 88. Kwengineko, Bournemouth iliishushia kichapo Everton na kuisasambua mabao 3-1, wakati ambapo Wabeba Bunduki wa Uingereza walikuwa wanalazimishwa sare ya mabao 2-2 na Watford. Mabao ya Arsenal yalifungwa na Pierre-Emerick Aubameyang katika dakika ya 21 na 32, huku ya Watford yakifungwa na Tom Cleverley na Roberto Pereyra.

Liverpool ambayo iliichabanga New Castle mabao 3-1 inasalia kileleni mwa jedwali la ligi kwa sasa ikiwa na alama 15, ikifuatiwa na City pointi 10, huku Tottenham ikifunga orodha ya tatu bora kwa alama 8.

……………………TAMATI………………..