Sep 18, 2019 10:55 UTC
  • Ruwaza Njema (17)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na Karibuni kusikiliza sehemu ya 17 ya kipindi hiki cha Riwaza Njema ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuriya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka Tehran. Kipindi hiki kama mnavyojua huzungumzia maandiko na Hadithi tofauti ambazo huguzia visa mbalimbali vinavyohusiana na tabia njema na ya kuvutia ya Bwana Mtume (saw) ambapo sisi wafausi wake tunapasa kuiga na kuifuata katika maisha yetu ya kila siku.

Katika kipindi cha leo tutazungumzia moja ya mazoea ya Bwana Mtume (saw) ya kumkimbilia Mwenyezi Mungu na kutafuta msaada wake kupitia swala na dua, wakati balaa na mikasa inapotufika na kufanya uadilifu na insafu katika utekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu, karibuni.

***********

Ndugu wasikilizaji, Sayyid Qutub ad-Deen ar-Rawandi amenukuu katika kitabu chake cha ad-Da'waat Hadithi kutoka kwa Maulana al-Imam as-Sajjad Zeinul Abedeen (as) kwamba alisema: 'Msiba ulipompata Amir al-Mu'mineen Ali (as) alikuwa akiswali siku hiyo rakaa elfu moja, kutoa sadaka kwa masikini sitini na kufunga siku tatu. Aliwaambia wanawe: Mnapopatwa na msiba fanyeni kama ninavyofanya mimi, kwa sababu nilimwona Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akifanya hivyo. Basi fuateni athari za Nabii wenu msije mkafanya kinyume na alivyokuwa akifanya, Mwenyezi Mungu akakugeuzieni uso (akakunyimeni baraka zake)….. Imam Zeinul Abideen (as) akasema: Hivyo mimi ninanendelea kufanya kama alivyofanya Amir al-Mu'mineen (as).'

 

Shahidi wa Pili Zein ad-Deen al-Aamili anasema katika kitabu chake cha Musakkin al-Fuad: Mtume (saw) alipofikwa na msiba alikuwa akisimama na kutawadha na kisha kuswali rakaa mbili na kusema: Allahumma! Nimefanya ulichotuamrisha, hivyo tutekelezee ulichotuahidi.'

Na Sheikh Warram al-Maliki al-Ashtari anasema katika kitabu chake cha akhlaki: 'Mtume (saw) alipokuwa akihuzunishwa na jambo lolote, alikuwa akijifariji kwa Swala na Swaumu; na imepokelewa kutoka kwake (saw) kwamba aali zake walipokuwa na haja fulani, aliwaambia: Simameni kwa ajili ya Swala…… Mwenyezi Mungu ameniamuru nifanye hivyo. Amesema: Na waamrishe watu wako kuswali, na uwe na subra nayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni wa mwenye takua.

**********

Tunaashiria hapa Riwaya nyingine inayobainisha wazi huruma kubwa aliyokuwa nayo Mtume (saw) hata kwa wale waliuomsababishia balaa na mashaka. Kwa mfano tunasoma katika kitabu cha as-Shifaa Bitaarif Huquuq al-Mustafa: 'Imepokelewa kwamba moja ya meno ya mbele ya Mtume (saw) lilipovunjwa na uso wake kujeruhiwa katika Vita vya Uhud, aliwalalamikia masahaba zake nao wakasema: Waombee dua ili wafikwe na mabaya. Mtume (saw) akasema: Sikubaathiwa (sikutumwa) kwa ajili ya kulaani bali nilibaathiwa kwa ajili ya kufikisha ujumbe (kuwaita watu kwenye heri) na rehema (kwa walimwengu). Allahumma! Iongoze kaumu yangu kwa sababu hawajui wanalofanya.'

***********

Wapenzi wasikilizaji, tunakunukulieni Hadithi ifuatayo kutoka kitabu cha al-Mahasin cha al-Barqi cha Thiqatul Islam al-Kuleini akimnukuu al-Hussein bin Khalid ambaye anasema: 'Nilimwambia Abal Hassan Musa al-Kadhim (as): Niambie hukumu ya mzinifu ambaye ameoa anayekimbia kutoka kwenye shimo wakati wa kufanyiwa haddi (kurujumiwa). Je, anapaswa kurudishwa ili afanyiwe haddi au la? Imam (as) akasema: 'Anarudishwa na harudishwi. Mpokezi wa Hadithi akauliza: Itawezekanaje hivyo ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu?! Imam Kadhim (as) akajibu: Iwapo atakuwa amekiri kosa mwenyewe - (yaani kuwa amezini –Mwenyezi Mungu atuepushie mbali hilo) – kisha akatoroka baada ya kumsibu (kumpiga) mawe kadhaa, harudishwi. Lakini iwapo ushahidi (kuwa amefanya zina) utakuwa umethibiti dhidi yake naye akawa anakana na kisha kutoroka, atarudishwa hali ya kuwa amedhalilika na kufanyiwa haddi (kurujumiwa).

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Allah kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Allah sana.

 

Ndugu wasikilizaji, kuna maelezo ya kuvutia mwishoni mwa Hadithi hii kuhusiana na umakini na uzingatiaji mkubwa wa Bwana Mtume (saw) kuhusiana na suala zima la uadilifu na insafu. Imam Kadhim (as) anazungumzia uadilifu na insafu ya babu yake Mtume (saw) kupitia kisa kifuatacho: 'Ma'iz bin Malik alikiri mbele ya Mtume (saw) kuwa alifanya zina (hali ya kuwa alikuwa ameoa). Mtume (saw) akaamuru arujumiwe, naye akawa amekimbia kutoka kwenye shimo la kufanyiwa rajm. Hapo Zubeir bin al-Awaam akamrushia muundi wa ngamia uliomtega na kumuangusha chini, na kisha watu wakamkamata na kumuua. Mtume (saw) alipofahamishwa habari hiyo alisema: Ni kwa nini hamukumuacha aende zake alipokimbia?! Hii ni kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa amekiri makosa yake. Hakika kama ningekuwa pamoja na nyinyi singekuacheni mumuue. Imam Kadhim (as) akasema: Hatimaye Mtume (saw) alimlipia fidia kwa familia yake kutoka katika mali ya Waislamu, kwa sababu aliuawa kimakosa.'

***********

Na tunahitimisha kipindi hiki cha juma hili kwa kukunukulieni Hadithi ifuatayo kuhusiana na upole na unyenyekevu wa kuvutia wa Mtume Mtukufu (saw) kwa wanadamu. Imepokelewa katika kitabu cha Makarim al-Alhlaq kutoka kwa Ibn Masoud kwamba alisema: 'Mtu mmoja alifika mbele ya Mtume Mtukufu (saw) na kuanza kuzungumza naye huku akiwa na woga na kutetemeka. Mtume (saw) akamwambia: Tulia! Mimi si mfalme bali ni mwana wa mwanamke ambaye alikuwa akila nyama iliyokaushwa kwa chumvi.'

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema kilichokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayoikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena wiki ijayo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags