Oct 07, 2019 07:56 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Oktoba 7

Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....

Debi la Esfahan; Sepahan yainyuka Zob Ahan

Klabu ya Sepahan imeigaragaza Zob Ahan mabao 2-0 katika Debi la Esfahan kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Iran IPL. Watani hawa wa jadi walibanana katika kipindi cha kwanza cha mchezo, na hakuna aliyefanikiwa kuona lango la mwenzake. Hata hivyo mambo yaligeuka katika kipindi cha pili, labda baada ya wakufunzi kuwapa somo vijana wao. Sepahan ilirejea uwanjani kwa kasi na ari isiyo ya kawaida, na wakafanikiwa kutikisa nyavu za Zob Ahan mara mbili. Magoli ya klabu hiyo yalitiwa kimyani na Giorgi Gvelesiani na Kiros Stanlley.

Klabu ya Zob Ahan iliyolishwa mawili bila jibu

Wakati Sepahan ikiinyoa bila maji Zob Ahan, Persepolis (Wekundu wa Tehran) walikuwa wanatandikwa bao moja bila jibu na Shahr Khodro katika Uwanja wa Imam Reza mjini Mashhad siku ya Ijumaa.

Nao Esteqlal au ukipenda waite The Blues wa Tehran, walikuwa wanapata ushindi wa kwanza msimu huu wa mabao 2-1 waliposhuka dimbani kuvaana na Gol Gohar Sirjan katika Uwanja wa Azadi hapa Tehran. Ushindi huu unakuja baada ya kupita wiki sita za kupoteza na kutoa sare. Kwa sasa Sepahan inacheka kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Soka ya Iran ikiwa na alama 14, pointi sawa na Teraktor Sazi ambao waliibamiza Pars Jonoubi bao 1-0 katika mchezo wao. Shahr Khodro ambao waliitandika Persepolis bao 1-0 wanafunga orodha ya tatu bora wakiwa na alama 13.

Iran bingwa Karate

Timu ya taifa ya karate ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kidedea katika mashindano ya Karate 1 - Premier League yaliyofanyika mjini Moscow, Russia. Makarateka wa Iran ya Kiislamu wametwaa ubingwa baada ya kuzoa medali 3 za dhahabu, moja ya fedha na moja ya shaba.

Makarateka wa kike wa Iran wakifanya mazoezi

Dhahabu mbili za kwanza za Iran zilitwaliwa na Sara Bahmanyar and Rozita Alipour katika safu ya makarateka wanawake, huku Zabihollah Poorship akiipa Iran dhahabu ya tatu katika kategoria ya wanaume. Makarateka zaidi ya 600 kutoka nchi 85 duniani wameshiriki mashindano hayo ya kimataifa mjini Moscow.

Iran ya 2 Soka ya Vipofu

Timu ya taifa ya soka ya vipofu ya Jamhuri ya Kiislamu imeibuka ya pili katika Mashindano ya Ubingwa wa Asia baada ya kunyukwa bao 1-0 na China katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo uliopigwa Jumapili. Iran iliingia uwanjani ikifahamu fika kuwa ina kibarua cha ziada kwa kuzingatia kuwa, China ni mshindi mara tano wa mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama Blind Football Asian Championships.

Licha ya kuzabwa bao 1 bila jibu, lakini timu hiyo taifa ya soka ya vipofu ya Iran imejikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Tokyo mwakani. Mbali na Iran na China, timu nyingine ambazo kufikia sasa zimetinga mashindano hayo ya dunia ya Paralimpiki ya Tokyo 2020 ni Brazil, Argentina, Hispania, Ufaransa na Japan.

Ngorongoro ya Tz watwa Cecafa U-20

Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania wenye umri wa miaka 20 almaarufu Ngorongoro Heroes imetwaa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri wa miaka 20 na kwenda chini (CECAFA Challenge U20) baada kuizaba Kenya bao bila jibu katika mechi iliyopigwa Jumapili nchini Uganda. Bao hilo la pekee lilipatikana kunako dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza baada ya mchezaji wa Kenya Otieno Onyango kujifunga. Ushindi huo unaipa rasmi Tanzania kikombe hicho ambacho mashindano yake yalikuwa yanafanyika nchini Uganda. Kocha wa Heroes anakiri kuwa walikuwa na kibarua cha ziada kuibuka na ushindi huo. Ngorongoro Heroes ilifanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya kuifunga Sudan mabao 2-1.

Wachezaji wa Ngorongoro ya Tanzania baada ya kuibuka washindi

Magoli ya Tanzania yalifungwa na Patrick Mwenda dakika ya 39 na Kelvin John dakika ya 45. Kenya nayo iliting fainali baada ya kuizaba Eritrea bao bila jibu. Bao hilo la pekee la Kenya lilikuwa alilojifunga mchezaji wa Eritrea, Yosief Mebrahtu katika dakika ya 84. Kenya na Tanzania ambazo zilikuwa kundi B zilikutana katika mechi ya ufunguzi iliyoishia kwa sare ya mabao 2-2. Wakati huohuo, mchezaji wa Tanzania Bara Kelvin John ameibuka na tuzo ya mchezaji Bora wa Mashindano na Mfungaji bora katika mashindano ya CECAFA U20 yaliyomalizika Jumapili kwa kuzikutanisha Tanzania Bara dhidi ya Kenya kwenye fainali.

Riadha; Kenya yaibuka ya Pili Doha

Kenya imemaliza nafasi ya pili katika msimamo wa medali wa Mashindano Riadha ya IAAF ya mabingwa wa riadha duniani yaliyoanza Septemba 27 na kumalizika jana Oktoba 6 huko Doha, Qatar. Kenya imemaliza mashindano hayo ikiwa na jumla ya medali 11, 5 za dhahabu, 2 za fedha na 4 za shaba. Nafasi ya kwanza imetwaliwa na Marekani huku China ikiondoka katika nafasi ya nne. Katika hatua ya fainali ya michuano hiyo iliyowakusanya wakimbiaji bora zaidi duniani, Timothy Cheruiyot wa Kenya ameshinda taji la dunia la mbio za wanaume mita 1,500, akiongoza kutoka mwanzo hadi mwisho na kutumia dakika 3 sekunde 29 na nukta 26.

Naye Mganda Joshua Cheptegei pia akiondoka kifua mbele na kushinda mbio za wanaume mita 10,000 akitumia muda mzuri kabisa katika historia ya michezo hiyo wa dakika 26 sekunde 48 na nukta 36. Mkimbiaji huyo mwenye miaka 23 ambaye mwaka 2017 alipata medali ya fedha ni Mganda wa kwanza kushinda taji hilo. Wakati huohuo, mwanariadha mwingine wa Kenya Conselsius Kipruto alimshinda Lamecha Girma wa Ethiopia katika fainali ya kusisimua ya mbio za mita 3,000 kuruka vizuizi na maji katika mashindano ya Dunia ya riadha huko mjini Doha Qatar. Girma aliongoza mbio hizo hadi sekunde ya mwisho lakini Kipruto, ambaye alionekana kama alifanikiwa kumfikia na na kunyakua ushindi uliosaidia kuhifadhi taji la dunia la mbio hizo. Alifahamu ushindi wake sekunde 30 baada ya wasimamizi wa mashindani hayo kuthibitisha ushindi wake. Kipruto, mwenye umri wa miaka 24 alimaliza mbio hizo kwa muda wa dakika 8:01.35. Mwanariadha huyo wa miaka 18 wa Ethiopia aliweka rekodi mpya ya kitaifa ya mbio hizo kwa muda wa dakika 8:01.36. Mwanariadha wa Morocco Soufiane el Bakkali aliibuka wa tatu kwa kumaliza mbio hizo kwa 8:03.76. Kenya imetawala mbio hizi tangu mwaka wa 1991 Moses Kiptanui aliposhinda dhahabu katika mbio za dunia mjini Tokyo na kuhifadhi ubingwa huo mwaka wa 1993 na 1995. Kwa jumla Kenya imeshinda mbio hizo mara 12 kwenye mashindano ya dunia.

Dondoo za Hapa na Pale

Bondia namba moja wa uzito wa juu Tanzania, Alphonce Mchumiatumbo amepigwa na Mrusi, Arstan Yellev kwa Technical Knock Out (TKO) nchini Urusi usiku wa kuamkia Jumapili Oktoba 6, 2019. Katika mpambano huo wa raundi 8, Mchumiatumbo alipigwa TKO kwenye raundi ya kwanza, Ambapo bondia Arslan Yallyev alimsokomezea masumbwi mawili mazito yaliyomwangusha chini Mchumitumbo mara mbili na kujikuta akisalimu amri. Kocha Mtanzania aliyeambatana na bondia huyo, Anthony Rutha amesema refa alilazimika kumaliza pambano baada ya Mtanzania huyo kupelekwa chini mara mbili mfululizo.

Kwengineko, kanali ya michezo ya Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG, imetoa taarifa kuwa inapinga vikali kauli isiyofaa ya mkuu wa timu ya The Houston Rockets ya Marekani Daryl Morey, na kuamua kusimamisha ushirikiano na uenezi wa michezo yote inayohusisha timu hiyo.

Novak Djokovic uwanjani akipambana

Na mchezaji tenisi namba moja duniani Novak Djokovic ametwaa Kombe la Michuano ya Wazi ya Tenisi ya Japan siku ya Jumapili na kuondoa wasiwasi kuhusu jeraha lake la bega lililomlazimisha kutoka kwenye michauno ya wazi ya Marekani. Nyota huyo kutoka Serbia limtoa kijasho chembamba Muaustralia John Millman kwa seti 6-3, 6-2 na kusherehekea ushindi wake wa 10 kwenye mashindano hayo makubwa. Djokovic, akicheza kwa mara ya kwanza kwenye mashindano hayi, aliwatambia wapinzani wake wiki nzima, bila kupoteza mchezo hata mmoja na hatimaye kujinyakulia kombe katika uwanja wa Ariake Colosseum ambao upo mahsusi kwa ajili ya Olimpiki ya Tokyo mwaka 2020. Djokovic, ambaye ni mshindi wa Grand Slams mara 16, sasa anakwenda kushiriki mashindano ya Shanghai Masters.

………………………….TAMATI……….………….