Oct 28, 2019 06:46 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Okt 28

Karibu mpenzi msikilizaji katika dakika hiki chache za kutupia jicho baadhi ya matukio muhimu yaliyojiri viwanjani ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kitaifa…..

Futsal: Iran yaibanjua Kyrgyzstan

Timu ya taifa ya soka inayopigwa ukumbini (futsal) ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeigaragaza Kyrgyzstan mabao 8-3 katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki Mashindano ya Mabingwa wa Futsal Barani Asia mwaka ujao 2020. Katika mchezo huo wa Ijumaa ulioshuhudiwa na idadi kubwa ya mashabiki katika Ukumbi wa Michezo wa Ghadir katika jiji la Oroumiyeh mkoani Azerbaijan Magharibi hapa nchini, timu hiyo ya Iran ilicheza kwa kasi kubwa labda kutokana na motisha ya mashabiki. Mahdi Javid alifunga mabao matatu ya hattrick, huku Mahdi Karimi akipachika wavuni mawili.

Timu ya taifa ya futsal ya Iran

Mabao mengine yalifungwa na Hamid Ahmadi, Mohammad Shajari na Taha Nematian katika mechi hiyo ya kikanda. Kwa ushindi huo, Iran mbali na kujikatia tiketi ya kushiriki mashindano hayo yanayofahamika kama Futsal Championship Turkmenistan 2020, lakini pia imemaliza mechi zake kwa kuwa kileleni mwa kundi lake. Mashindano hayo ya kibara yanayoandaliwa na Muungano wa Mashirikisho ya Soka Asia AFC yatafanyika mjini Ashgabat, nchini Turkmenistan kuanzia Februari 24 hadi Machi 10 mwakani.

 

Wushu: Iran yashikilia taji lake

Timu ya taifa ya mchezo wa wushu kategoria ya sanda ya Iran ya Kiislamu imetwaa ubingwa wa mchezo huo duniani katika mashindano yaliyofanyika mjini Shanghai, China. Iran imezoa medali 9 za dhahabu katika duru ya 15 ya mashindano hayo ya World Wushu Championships (WWC) iliyofunga pazia lake Jumatano. Katika safu ya wanawake, Hanieh Rajabi ametwaa medali mbili za fedha katika vitengo vya nandao na nangun, huku mwenzake Zahra Kiani ikitia kibindoni shaba katika safu ya changquan. Kwa ujumla China imeibuka kidedea katika safu zote, huku Iran ikiibuka mshindi wa pili katika mashindano hayo ya kikanda.

Wanamichezo wa wushu wa Iran walioshinda medali na wasimamizi

Mbali na hayo, wanamichezo wa Kiirani wametwaa medali nne katika mashindano ya upigaji makasia ya bara Asia yaliyomalizika Jumapili nchini Korea Kusini. Iran imejikusanyia medali mbili za dhahabu na mbili za shaba katika kategoria tofauti ya mashindano hayo.

Soka: Yanga katika njiapanda

Klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania imepoteza mchezo muhimu katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa nyumbani katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kwa kuchapwa magoli 2-1 dhidi ya Pyramids FC kutoka nchini Misri. Magoli ya vijana hao wa Kiarabu yalifungwa na Erick Traory dakika chache kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza, huku Abdallah Saed akifunga la pili katika dakika 62.

Goli pekee la Yanga likifungwa na Papi Tshishimbi katika dakika za lala salama. Kwa kichapo hicho, Yanga imejiweka kwenye mazingira magumu ya kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Yanga ambao ni wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa wana kazi ya kupindua matokeo watakapovaana na Mafarao hao wa Misri kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa baada ya wiki mbili. 

Riadha: Kenya yang'ara tena mbio za Marathon

Bingwa wa mbio za Marathon kutoka Kenya, Valary Aiyabei ameibuka kidedea kwenye mbio za Frankfurt Marathon mwaka huu 2019. Hii ni baada ya kumaliza mbio hizo kwa kutumia saa mbili dakika 19 na sekunde 10 na kuvunja rikodi ya saa 2 dakika 20 na sekunde 36 iliyowekwa na Meskerem Assefa; na kuwa mwanamke wa kwanza kukimbia chini ya saa 2:20 huko Frankfurt. Kasi ya Aiyabei ni kubwa mara tano katika msimu huu. Amewashinda Waethiopia Megertu Alemu (2:21:00) na Meskerem Assefa (2:22:01) waliochukua nafasi ya pili na ya tatu mtawalia. Assefa alirudi kutetea taji lake lakini alishindwa kuifikia kasi ya Aiyabei.

Raga: Kombe la Dunia, Afrika Kusini yating fainali

Timu ya taifa ya raga ya Afrika Kusini imejikatia tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la Dunia la Raga huko Yokohama Japan, baada ya kuifanyia mauaji ya kimbari Wales katika mchuano wa nusu fainali uliopigwa Jumapili. Kiungo Handre Pollard ndiye aliyekuwa nyota wa mechi kwa kufunga pointi 14 kwenye mpambano mkali ulioshia kwa Afrika Kusini kushinda 19-16 dhidi ya Wales.

Wanaraga wa Afrika Kusini wakishangilia ushindi

Mpambano huo uliokuwa wa kukata na shoka umeshuhudia mabingwa hao wa kombe la Dunia mwaka 1995 na 2007 kuwabwaga Wales katika shindano lao la tatu la nusu fainali baada ya huko nyuma kupoteza katika mwaka 2011 na 1987. Afrika Kusini sasa itavaana na Uingereza katika ngoma ya fainali itayopigwa siku ya Jumamosi.

Dondoo za Hapa na Pale

Mwanafunzi wa kike wa shule moja katika jimbo la Ohio nchini Marekani ameondolewa kwenye mashindano ya mbio za nyika kwa kuvaa vazi la stara la hijabu. Noor Alexandria Abukaram mwenye umri wa miaka 16 amelaani vikali udhalilishaji na ubaguzi aliofanyiwa kwa misingi ya dini yake wakati wa mashindano ya mbio za nyika katika mji wa Findlay jimboni Ohio mapema mwezi huu. Mwanafunzi huyo wa shule ya upili ya Sylvania Northview amesema, "Moyo wangu ulivunjika baada ya kuambiwa kuwa nimeondolewa kwenye mashindano hayo muhimu eti kwa kuwa nilikuwa nimevaa hijabu, vazi ambalo eti linakiuka mavazi ya michezo yaliyoanishwa." Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita, binti mwingine wa Kiislamu ambaye anachezea timu ya taifa ya mchezo wa squash ya Marekani aliwafungulia mashitaka wafanyakazi wa shirika la ndege la Air Canada kwa kumlazimisha kuvua hijabu kabla ya kuabiri ndege ya shirika hilo nchini Marekani.

Noor Alexandria Abukaram

Kwengineko, Shirikisho la Kandanda Tanzania TFF limetangaza rasmi kuwa Etienne Ndairagije ndio kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars. TFF imethibitisha  kuwa imeingia mkataba wa mwaka mmoja na kocha Ndairagije, ambaye awali alikuwa akikaimu nafasi ya ukocha mkuu baada ya kufukuzwa Emmanuel Amunike. Maamuzi yamefikiwa baada ya TFF kuridhishwa na kiwango cha Etienne akiiongoza Taifa Stars katika michezo saba kama kaimu kocha mkuu na kushinda mechi 3, sare 3 na kupoteza mchezo mmoja. Kabla ya hapo Ndairagije alikuwa kocha wa Azam FC.

Wakati huohuo, baada ya kuibuka kwa taarifa juu ya Shirikisho la Soka la visiwani Zanzibar (ZFF) kuvunja rasmi mahusiano na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), uongozi wa shirikisho hilo umekuja na kusema kuwa kwa sasa mahusinano yao yako vizuri na wanatarajia kukutana ili kutatua changamoto zilizojitokeza kati yao. Akitoa taarifa hiyo Msemaji wa wa Rais ya ZFF Adam Natepe alisema tarifa zilizoakisiwa na baadhi ya vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii juu ya kusitisha mahusiano yao kati ya ZFF na TFF ni ya kweli ambapo kutokana na jambo hilo TFF imeitaka ZFF kukaa pamoja na kuyamaliza, ilikuondoa mgogoro huo.

Wallace Karia, Rais wa TFF

Na hatimaye Rais wa Shirikisho la Soka nchini Kenya FKF, Nick Mwendwa, amekuwa ni mgombea pekee aliyewasilisha fomu zake kwa bodi inayoandaa uchaguzi wa kiongozi wa soka nchini humo. Wagombea wengine, wakiongozwa na rais wa zamani Sam Nyamweya, Moses Akaranga, Alex Ole Magelo na Steve Mburu hawakujitokeza kwa madai kuwa, bodi itakayosimamia uchaguzi huo, ilibadilisha sheria ili kumpendelea Mwendwa. Hata hivyo, Mwenyekiti wa bodi Edwin Wamukoya amesisitiza kuwa, siku ya Jumatano ilikuwa ya mwisho kwa waliokuwa na nia kuwania nafasi hiyo kurudisha fomu zao na sasa mlango umefungwa.

……………………TAMATI…………….