Ulimwengu wa Michezo, Nov 11
Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu tuzame viwanjani kutupia jicho matukio muhimu ya spoti na wanaspoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa……
Iran yatwaa tena Taji la Soka ya Ufukweni
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Kombe la Soka ya Ufukweni kwa mara ya tatu baada ya kuisasambua Uhispania mabao 6-3 katika mchuano wa fainali uliopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Jumeirah mjini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu. Wachezaji mahiri wa Iran waliotikisa nyavu katika kitimutimu hicho ni Saeid Piramoun, Mohammad Mokhtari, Hamid Behzadpour, Mohammad Ahmadzadeh na Mohammad Masoumizadeh. Kiungo nyota wa Iran Amirhossein Akbari alitajwa kuwa mchezaji aliyefunga mabao kwenye mashindano hayo, kwani alitikisa wavu mara 6.

Umoja wa Falme za Kiarabu umeitandika Russia mabao 2-1 na kuibuka mshindi wa tatu wa mashindano hayo ya dunia. Iran ilikabidhiwa kombe hilo la mabara katika mashindano hayo yanayojulikana kama Intercontinental Beach Soccer Cup yaliyofunga pazia lake Jumamosi katika mji wa Dubai, huko Imarati. Mashindano hayo yalianza Novemba 5. Iran imetwaa taji hilo mwaka 2013, 2018 huku ikitwaa nafsi ya pili katika mashindano ya mwaka 2017. Mwaka jana, Iran ilitwaa taji hilo baada ya kuisasambua Russia mabao 4-2 katika mchuano wa fainali uliopigwa Dubai.
Timu ya kutunisha misuli ya Iran yatwaa taji la dunia
Timu ya taifa ya mchezo wa kutunisha misuli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka mshindi katika Mashindano ya Mabingwa wa Utunishaji Misuli yaliyofanyika mjini Fujaira, huko Imarati. Timu hiyo ya Iran imeibuka kidedea kwa kuzoa jumla ya medali 11 za dhahabu na 3 za fedha., katika kategoria tofauti za kuanzia kilo 70 hadi 100. Waliotwaa dhahabu katika safu ya uzani ni pamoja na Mobin Karimi (70kg), Farshad Ganji (75kg), Mohammad Ebrahim Arzeshmand (85kg), Mahdi Arzeshmand (90kg), Babak Arzeshmand (95kg) na Mazaher Tabani (+ 100kg).

Katika kategoria ya Classic Physique, Muirani Ali Reza Hassanvand aliibuka kidedea na kutwaa dhahabu huku media nyingine ya dhahabu ya Iran ikitiwa kibindoni na Mahmoud Pour Saber kwa upande wa Body Classic. Hossein Karimi aliipa Iran dhahabu nyingine katika safu ya misuli. Mashindano hayo huwa yanasimamiwa na Shirikisho la Kimataifa la Utunishaji Misulu (IFBB) ambalo liliasisiwa na kaka wawili, Ben na Joe Weider mwaka 1946 mjini Montreal, Canada.
Raga: Kenya yatinga Michezo ya Olimpiki 2020
Timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya almaarufu Shujaa imemaliza ukame wa miaka mitatu bila taji la Kombe la Afrika baada ya kupepeta Uganda 33-0 katika fainali ya Jumamosi jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini. Mbali na kuibuka wafalme wapya wa Bara Afrika, vijana wa kocha Paul Feeney pia wamejikatia tiketi ya kushiriki Olimpiki ya mwaka 2020 moja kwa moja. Shujaa, ambayo ilifanya vibaya sana raga hii ilipojumuishwa kwenye Olimpiki mwaka 2016 nchini Brazil, ilikuwa inakutana na Uganda kwa mara ya pili jijini Johannesburg. Ilibwaga majirani hao wake 24-7 katika mechi ya makundi kabla ya kudhirihisha uweledi huo wake katika fainali kupitia miguso ya nahodha Andrew Amonde pamoja Daniel Taabu, Jeff Oluoch na Oscar Dennis aliyefunga miguso miwili.

Kenya, ambayo iliwahi kuwa namba wani Afrika mwaka 2004, 2008, 2013 na 2015, imeungana na Japan (wenyeji), Fiji, Marekani, New Zealand na Afrika Kusini (nambari nne za kwanza kutoka Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019) na mabingwa Argentina (Amerika Kusini), Canada (Amerika Kaskazini), Uingereza (Ulaya) na Australia (Oceania) katika Olimpiki 2020 itakayofanyika jijini Tokyo.
Kikapu: JKT yatwaa ubingwa taifa Tanzania
Klabu ya JKT imetwaa ubingwa wa Ligi Taifa ya Kikapu Tanzania (NBL), baada ya kuichachafya Savio kwa vikapu 62 kwa 51 katika fainali iliyopigwa wikendi hii katika ukumbi wa ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mashindano ya NBL yalishirikisha timu 14 kutoka klabu mbalimbali nchini ambazo zilichuana kusaka ubingwa huku timu ya Rukwa Stars na Deep Sea Queens ya Tanga zikiwa ni klabu pekee kutoka nje ya Dar es Salaam zilizotinga robo na nusu fainali. Mbli na kutwaa ubingwa, nahodha wa JKT ametangazwa kuwa nyota wa mashindano hayo ya basketboli. Nini siri ya ushindi wa timu hii kwa mwaka wa pili mfululizo?

JKT ambayo ni mwakilishi pekee wa Tanzania katika Mashindano ya Ligi ya Afrika yatayoanza kutia mavumbi Novemba 17 katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, ilitinga fainali baada ya kuiadhibu Oilers vikapu 68 kwa 45, huku Savio ikijikatia tiketi ya fainali kwa kuigaragaza Pazi alama 69-45. Oilers imeibuka mshindi wa tatu baada ya kuizaba Pazi vikapu 79-42.
Riadha: Kenya yahifadhi taji
Kenya imehifadhi taji la kinadada la Chama cha Mbio za kimataifa za kilomita 42 na ndefu (AIMS) baada ya Ruth Chepng’etich kutawazwa mshindi Ijumaa usiku jijini Athens nchini Ugiriki. Chepng’etich alipata tuzo hiyo kutokana na mafanikio yake katika kipindi cha miezi 12 iliyopita. Katika kipindi hicho, Chepng’etich alizoa mataji ya mbio za Istanbul Marathon, Dubai Marathon, Istanbul Half Marathon, Seiryu Half Marathon na Bogota Half Marathon pamoja na kushinda marathon kwenye Riadha za Dunia jijini Doha nchini Qatar mnamo Septemba 27. “Ni heshima kubwa kupokea tuzo hii, hasa katika mji huu ambao marathon ilizaliwa,” alisema Chepng’etich, Ijumaa. Kinadada wengine kutoka Kenya waliowahi kubeba tuzo hii ya kifahari ni Tegla Loroupe mwaka 1995, 1997, 1998 na 1999, Catherine Ndereba (2001) na Mary Keitany (2009, 2011 na 2017). Wengine ni Edna Kiplagat (2013), Florence Kiplagat (2014), Jemima Sumgong (2016) na Gladys Cherono (2018). Kabla ya kupoteza taji la wanaume kwa Muethiopia Lelisa Desisa Mwaka huu 2019, Wakenya walikuwa wametwaa tuzo ya AIMS kwa upande wa wanaume kupitia Benson Masya (1992), Paul Tergat (1996 na 2003), Josephat Kiprono (2001), Samuel Wanjiru (2008), Patrick Makau (2010), Geoffrey Mutai (2011 na 2012), Wilson Kipsang (2013), Dennis Kimetto (2014) na Eliud Kipchoge (2015, 2016, 2017 na 2018).

Wakati huohuo, Mwanariadha wa Kenya anayeshika rikodi ya dunia ya marathon Paul Tergat amepokea Tuzo ya Heshima ya Achilles kwenye Tamasha la Filamu la Kimataifa la Riadha (FICA) katika mji wa San Sebastian nchini Hispania. Bingwa huyo mara tano wa mbio za nyika, Juzi Jumanne alikuwa mgeni wa heshima katika sherehe za FICA. Tergat ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki amefuata nyayo za Bob Beamon miezi 12 iliyopita aliyepokea tuzo kwa mchango wake kwenye michezo. Amewashukuru waandaaji wa hafla hizo kwa kuenzi jitihada zao za miaka mingi katika uga wa spoti. Wakati anashiriki riadha mapema miaka ya 1990, Tergat alikuwa bingwa maarufu duniani na kuweza kushinda mbio kadhaa za nyika.
Ligi Kuu ya Uingereza
Klabu ya Liverpool imeendeleza ubabe wake kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, sawia na rekodi yake ya kutokufungwa katika siku 900. Hii ni baada ya kuichapa Manchester City mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Anfield katika kindumbwedumbwe cha Jumapili. Hii ilikuwa mara ya 214 kwa timu hizo kukutana na pia mara ya 17 kwa City kushindwa kutamba mbele ya Liverpool uwanjani Anfield katika Ligi ya EPL. Liverpool ikiwa nyumbani ilipata ushindi huo mnono kupitia mabao yake yaliyofungwa na Fábio Henrique maarufu kama Fabinho katika dakika 6, Mohammad Salah dakika 13 na Sadio Mane dakika 51, huku lile la kufutia machozi kwa mabingwa watetezi Man City likifungwa na Benardo Silva.
Ushindi huo unaifanya Liverpool ituame kileleni mwa jedwali la ligi ikiwa na alama 34, tofauti ya pointi tisa zaidi ya Manchester City inayoshika nafasi ya nne. Nayo klabu ya Manchester United imefanikiwa kupanda hadi nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kuisasambua Brighton mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Old Trafford siku hiyo hiyo ya Jumapili. Mabao ya Mashetani Wekundu yalifungwa na Andreas Pereira (17), kabla ya Davy Propper kujifunga bao la kisigino dakika 2 baadaye. Marcus Rashford alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la wageni na kuvuruga kabisa mahesabu yao, katika dakika ya 68.

Katika mchezo mwingine Wolverhamton Wanderers iliutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani baada ya kuifunga Aston Villa kwa mabao 2-1 na kuwafanya wapande kutoka nafasi ya 15 hadi ya 8, wakati Villa ikibaki nafasi ya 17, ikiwa juu kwa tofauti ya pointi tatu kwa timu zinazoshuka daraja. Siku ya Jumamosi, klabu ya Chelsea ilifanikiwa kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kuipiga Crystal Palace mabao 2-0 kwenye mchezo uliochezwa Stamford Bridge. Magoli ya The Blues wa Uingereza wakiwa nyumbani yaliwekwa kambani na Tammy Abraham dakika ya 52 na jingine likifungwa na Christian Pulisic dakika ya 79. Arsenal waligaragazwa mabao 2-0 na Leicester City katika Uwanja wa King Power na kulazimika kuondoka uwanjani vichwa chini. Mabao ya wenyeji yalifungwa na Jamie Vardy na James Maddison.
Flying Foxes wapo katika nafasi ya pili wakiwa na alama 26, alama sawa na Chelsea, huku City ikifuatia ikiwa na alama 25. Gunners wenye alama 17, hawana budi kutosheka na nafasi ya 6 kwenye msimamo wa Ligi.
................................MUZIKI...............................