Rais Pezeshkian: Iran haitaki silaha za nyuklia
-
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza tena kuwa nchi hii haitaki kumiliki silaha za nyuklia kwa aina yoyote ile.
Katika mahojiano siku ya Jumanne, Rais Pezeshkian amesema: “Tumesema mara kwa mara na kwa uwazi kuwa hatutafuti kabisa silaha za nyuklia. Sera zetu, pamoja na fatwa ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, ziko wazi na thabiti kuhusu suala hili."
Amebainisha kuwa tetesi na propaganda zinazodai kuwa Iran inaendeleza mpango wa silaha za nyuklia zina msukumo wa kisiasa, huku akieleza matumaini kwamba jumuiya ya kimataifa, hasa Marekani, itatambua uhalisia huo.
Hata hivyo, rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Iran inahitajia sayansi ya nyuklia ili kukidhi mahitaji yake ya kimaabara, kiteknolojia na kitabibu.
Rais wa Iran ameendelea kusema kuwa: “Hatuwezi kukubali kunyimwa haki ya kutumia sayansi na maarifa ya nyuklia kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wetu, kuendeleza viwanda vyetu, na kukuza kilimo chetu."
Rais Pezeshkian pia amebaini kuwa Iran iko tayari kikamilifu kwa aina yoyote ya ukaguzi wa mpango wake wa nyuklia. Amesema Iran haina hofu juu ya ukaguzi wa kina unaofanywa na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).
Sehemu za mahojiano hayo zilichapishwa na Ofisi ya Rais wa Iran saa chache baada ya wajumbe wa Iran kufanya duru ya pili ya mazungumzo ya nyuklia na wawakilishi wa Marekani katika mji wa Geneva, Uswisi.
Mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja yalianza mapema mwezi huu nchini Oman, baada ya pande zote mbili, Iran na Marekani, kupunguza kauli kali zilizokuwa zikionyesha uwezekano wa mzozo wa kijeshi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, aliyeongoza ujumbe wa Iran mjini Geneva, alisema kuwa mazungumzo hayo na Marekani yamepiga hatua.
Araghchi aliongeza kuwa mazungumzo hayo ya siku ya Jumanne yalihitimishwa kwa makubaliano juu ya misingi elekezi, ambayo yataongoza mazungumzo yajayo kuelekea makubaliano tarajiwa.