Ulimwengu wa Spoti
Ulimwengu wa Michezo, Disemba 2
Matukio muhimu ya spoti ndani ya siku saba zilizopita......
Soka Wanawake: Iran yaibuka ya 2
Timu ya taifa ya soka ya wanawake wenye chini ya miaka 23 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili kwenye duru ya kwanza ya Mashindano ya Ubingwa wa Nchi za Asia ya Kati (CAFA). Hii ni baada ya kuigaragaza Afghanistan kwenye mchuano wake wa mwisho wa mashindano hayo ya kikanda Alkhamisi. Timu hiyo ya wanawake wa Iran inayonolewa na Maryam Azmoun alipata ushindi huo wa kishindo kupitia mabao ya Hajar Dabbaghi aliyefunga matatu ya hatrick, huku Fatemeh Geraeli, Fatemeh Shaban, Zahra Masoumi na Fatemeh Amineh Borazjani kila mmoja akifunga bao moja. Iran imezoa alama 12 katika mechi zake tano ilizocheza kwenye michuano hiyo ya Asia ya Kati.

Kiungo Dabbaghi ameteuliwa kuwa mfungaji bora wa mabao kwenye mashindano hayo, baada ya kufanikiwa kucheka na nyavu mara nane. Iran ilianza vizuri mashindano hayo, kwa kuizaba Turkemenistan mabao 5 bila jibu, baada ya kuiukung'uta Kyrgyzstan mabao 6-0; huku mwenyeji Tajikistan ikilambishwa mabao 4-0 kwenye mchezo wa ufunguzi wa mashindano. Uzbekistan imeibuka kidedea kwa kuzoa jumla ya alama 15, ambapo katika mchuano wake wa mwisho iliichachawiza Tajikistan mabao 3-0. Mechi hizo za CAFA zilipigwa katika viwanja vya taifa vya miji ya Dushanbe na Hisor nchini Tajikistan.
Karate: Iran yapeta Uhispania
Timu ya taifa ya karate ya wanaume ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetawazwa kuwa timu bora mwaka huu 2019, katika mashindano ya Ligi Kuu ya Karate 1 mjini Madrid nchini Uhispania. Hii ni baada ya kutwaa medali saba za dhahabu, kumi za fedha na kumi na tatu za shaba. Ligi hiyo ndio bora zaidi duniani katika mashindano ya karate. Kazakhstan imemaliza ya pili kwa kuzoa sita za dhahabu, ikifuatiwa na Japan iliyorudi nyumbani na medali tano za dhahabu. Makarateka zaidi ya 700 kutoka nchi 89 duniani wameshiriki mashindano hayo ya dunia yanayofahamika kama Madrid Karate1 League.

Wakati huohuo, timu ya karate mtindo wa kumite ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili katika mashindano ya Ligi ya Karate 1 mjini Madrid nchini Uhispania siku ya Jumapili. Makarateka wa Iran Amir Mehdizadeh and Sajad Ganjzadeh kila mmoja alijishindia medali ya dhahabu katika mashindano hayo. Ganjzadeh alimchachafya Mfaransa Jacquet Dnylson na kumshinda kwa alama 4-0 katika safu ya makarateka wenye kilo zaidi ya 84. Mehdizadeh alitangazwa mshindi kutoka na ufundi na umbuji wake, licha ya kutoa 0-0 alipovaana na Ozer Omer Abdurrahim wa Ututuki. Saleh Abazari aliipa Iran medali ya shaba katika mashindano hayo ya karate yaliyoanza Novemba 29 na kumalizika Disemba 1. Kazakhstan imeibuka kidedea kwa kutwaa medali mbili za dhahabu na mbili za shaba huku Uturuki ikimaliza ya tatu kwa kutia kibindoni dhahabu moja, fedha moja na shaba moja. Timu ya karate ya wanawake wa Iran iliweza tu kutwaa medali moja ya shaba.
Ndondi: Mwakinyo awajia juu wanaosema kabebwa
Mwanasumbwi nyota wa Tanzania, Hassan Mwakinyo amewajia juu wanaombeza na kusema kuwa alibebwa katika pigano lake na Mfilipino siku chache zilizopita. Bondia huyo wa kulipwa amesema wanaozungumza hivyo hawana ufahamu juu ya masuala ya kiufundi ya masumbwi. Katika pambano hilo la siku chache zilizopita, Hassan Mwakinyo alimpiga mpizani wake, Mfilipino Arnel Tinampay na kutangazwa mshindi kutokana na kile kinachofahamika kama “majority decision’. Amepuuzilia madai kuwa alibebwa na kwamba Mfilipino alimshinda kwa pointi.
Mwakinyo alitangazwa mshindi wa pointi 2-1 za majaji katika pambano hilo la kimataifa lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Waziri wa Michezo nchini Tanzania, Harrison Mwakyembe amempongeza Mwakinyo kwa ushindi huo, akisisitiza kuwa mwanasumbwi huyo anapasa kupewa motisha zaidi. Pambano hilo la uzito wa Super Welter lisilo na ubingwa ni la raundi 10, na ni la kwanza la kimataifa kwa Mwakinyo kucheza katika ardhi ya Tanzania. Pambano lake la mwisho lilikuwa Machi mwaka huu nchini Kenya, ambapo alimshinda kwa Technical Knock Out mpinzani wake Sergio Gonzalez kutoka Argentina.
Riadha: Mganda avunja rekodi
Mwanariadha kutoka Uganda Joshua Cheptegei mwenye asili ya Kenya amevunja rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 10 huko Valencia, nchini Uhispani na kuandikisha muda mpya wa dakika 26 na sekunde 38. Mwanariadha huyo mwenye miaka 23 amevunja rekodi ya zamani kwa sekunde sita, ambayo iliwekwa mwaka 2010 na Mkenya Leonard Komon. Cheptegei anasema alijitahidi kadri ya uwezo wake licha ya kupigwa na mafua na malaria wakati wa kufanya mazoezi kwa ajili yam bio hizo.
Cheptegei amevikwa taji la bingwa wa mita 10,000 huko Doha mwezi Oktoba, na pia mwezi Machi kushinda taji la dunia la mbio za nyika km 10 nchini Denmark. Mwaka 2018 alikimbia kwa dakika 41 sekunde tano huko Nijmegen, Uholanzi, na kuvunja rikodi ya dunia ya mbio za km 15. Kasi ya wastani ya Cheptegei ilikuwa ni dakika mbili na sekunde 40 kwa kilomita huko Valencia, na kukamilisha kilomita 5 kwa kutumia dakika 13 na sekunde 24.
Dondoo za Hapa na Pale
Binti Muislamu mwenye kuvaa Hijabu, Khadijah Mellah, ametangazwa kuwa Mwanamichezo Bora Msichana wa mwaka nchini Uingereza kufuatia ushindi wake katika mashindano ya mbio za farasi ya Kombe la Magnolia. Mellah, alikuwa mshiriki wa kwanza wa kike kushiriki katika mashindano rasmi ya farasi nchini Uingereza akiwa amevalia Hijabu na aligonga vichwa vya habari baada ya kufanikiwa kuendesha farasi Haverland hadi kupata ushindi katika mashindano yaliyofanyika Goodwood mwezi Agosti. Mellah amekabidhiwa zawadi yake katika ofisi cha News UK mjini London katika sherehe iliyofanyika Alkhamisi. Khadijah Mellah aliye na umri wa miaka 18 anasema anafuraha kubwa kuwa ameweza kutoa taswira chanya ya mwanamke Muislamu mwenye kuvaa Hijabu nchini Uingereza. Aidha amesema kumekuwepo na taswira potovu nchini humo kuhusu wanawake Waislamu kuwa hawatoki nje ya nyumba na kufanya kazi za kawaida.
Mbali na hayo, klabu ya Arsenal imefanya maamuzi magumu ya kumpiga kalamu nyekundu kocha wake Unai Emery kwa kuliyumbisha jahazi ya Gunners. Emery amefukuzwa kazi baada ya kuinoa Arsenal kwa takribani miezi 18. Usimamizi wa Wabeba Bunduki hao wa Londo ulifikia maamuzi hayo baada ya kupoteza katika mchezo wa UEFA Europa League wakiwa katika uwanja wao wa Emirates ambapo walitandikwa mabao 2-1 dhidi ya Frankfurt. Freddie Ljungberg ndio atakuwa kocha wa muda wakati huu uongozi wa Arsenal ukiwa unatafuta mbadala wake. Haya yanajiri siku chache baada ya klabu ya Tottenham Hotspurs chini ya mwenyekiti wao Daniel Levy imetangaza kuingia mkataba wa miaka mitatu na Jose Mourinho wa kuifundisha timu hiyo ambayo msimu huu imekuwa ikisuasua. Mourinho alipewa jukumu hilo saa chache baada ya Hotspurs kutangaza kumfuta kazi rasmi aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Mauricio Pochettino. Shoka hilo la timuatimua halikuachia hapo. Kocha wa klabu ya Watford Quique Sanchez Flores ametimuliwa kazini siku 85 tu baada ya kutua ugani Vicarage Road. Mhispania huyo alichukuwa wadhifa wa Javia Garcia baada ya Hornets kushiriki mechi nne za ligi bila kuandikisha ushindi wowote. Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 54 alifaulu kupata ushindi mmoja pekee katika mechi kumi za Ligi Kuu
Na tukiwa bado katika suala hilo la timuatimua, klabu ya Simba ya Tanzania imetangaza rasmi kuachana na kocha wake mkuu Patrick Aussems kwa kile walichodai kuwa ameshindwa kufikia malengo. Moja kati ya sababu zilizopelekea kumfuta kazi Aussems ni pamoja na kushindwa kufikia malengo ya kucheza hatua ya Makundi ya michuano ya CAF Champions League msimu 2019/2020. Barua ya kumtimua Aussems iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Senzo Mbatha imesema mchakato wa kutafuta kocha mkuu mpya utaanza mara moja. Aidha bodi imemteua kocha msaidizi Dennis Kitambia kukaimu nafasi ya Aussems. Haya yanajiri siku chache baada ya kuondolewa kwa kocha mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera na nafasi yake kukaimiwa na Boniface Mkwasa. Wakati huohuo, kocha wa klabu ya Mbeya City ya Tanzania ameamua kubwaga manyanga pia. Juma Mwambusi ameandika barua ya kujiuzulu kuifundisha timu hiyo kutokana na mwenendo mbovu wa matokeo kwenye mechi za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara. Katika kikao chake kilichofanyika Jumamosi pamoja na Bodi ya Timu ya Mbeya City, bodi hiyo imeridhia ombi la kocha huyo kujiuzulu. Hivi karibuni Mwambusi alijiwa juu na mashabiki wa klabu hiyo wakimtuhumu kuwa ana upendeleo, wakati timu hiyo ilipochezea kichapo kutoka Singida United.
Na Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Gianni Inafantino amesema shirikisho hilo lingependa kuona bara la Afrika linaanzisha ligi ya kikanda ya timu 20. Amesema Fifa inataka ligi hiyo mpya iambatane na uboreshaji wa viwanja kuwa vya kisasa katika kila nchi mwanachama wa Umoja wa Afrika. Aliyasema hayo akiwa ziarani nchini Kongo, alikoalikwa kushiriki hafla ya kuadhimisha miaka 80 tangu klabu ya TP Mazembe iasisiwe. Amesema "Ligi hii inaweza kuleta mapato ya zaidi ya dola milioni 200 na kuwa moja ya ligi kumi bora duniani."
………………………TAMATI……….….…..