Jan 13, 2020 07:20 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Januari 13

Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....

Jamii ya wanamichezo wa Iran yamuomboleza Soleimani

Wanamichezo mbalimbali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanaendelea kumuomboleza na kumuenzi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa mapema mwezi huu katika shambulio la kigaidi la Marekani nchini Iraq. Wanariadha, wanamileka, wanasoka, wanataekwondo na makarateka wa Iran miongoni mwa wanamichezo wengine wamelaani vikali jinai hiyo ya kutisha ya Marekani kwa kauli za moja kwa moja na walizozituma na kuchapisha kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii. Aidha taasisi za michezo za Iran ikiwemo Wizara ya Michezo na Vijana na Kamati ya Taifa ya Olimpiki zimetuma salamu zao za rambirambi kufuatia mauaji hayo yaliyofanywa na Marekani nchini Iraq. Alireza Jahanbakhsh, mchezaji nyota wa timu ya taifa ya soka ya Iran na anayechezea pia klabu ya Brigton ya Uingereza sambamba na kuelezea masikitiko yake kuhusu ukatili huo ameandika: "Sielewi kwa nini mtandao wa kijamii wa Instagram unafuta machapisho yanayohusu mtu aliyepigana kulinda mipaka ya nchi na taifa. Sielewi kabisa."

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC

 

Akthari ya wanamichezo mashuhuri hapa nchini waliweka picha za Soleimani zilizoambatana na jumbe za kutoa mkono wa pole na kumuenzi Jenerali Soleimani, aliyeuawa kwa makombora ya Marekani usiku wa kuamkia Ijumaa ya Januari 3, akiwa nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo.

Iran yatinga Olimpiki 2020

Timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka huu 2020 jijini Tokyo Japan, baada ya kuifanyia China mauaji ya kimbari siku ya Jumapili. Timu hiyo ya voliboli ya wanaume wa Iran inaingia kwenye michezo ya Olimpki ikiwa timu bora zaidi ya Asia. Katika mchezo huo wa Jumapili, Iran iliwasagasaga Wachina kwa seti 3-0 za (25-14, 25-22, 25-14) na kuibuka kidedea. Huu ulikuwa mchezo wa marudiano baina ya miamba hiyo ya voliboli barani Asia haswa kuzingatia kuwa, siku ya Alkhamisi, Iran ilikuwa imeichabanga China alama 3-0 katika mchezo wa Kundi A.

Timu ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Mohammad Mousavi wa Iran ndiye aliyeng'ara zaidi kwenye mchuano huo kwa kufunga pointi 16 ambazo ni za juu zaidi, akifuatiwa na Mchina Chuan Jiang aliyefunga alama 13. Nahodha wa timu hiyo ya Iran, Milad Abadipour anasema ingawaje mchezo wenyewe ulikuwa mgumu, lakini wanafuraha kubwa kwa kuibuka na ushindi huo mnono hatimaye.

Mbali na mwenyeji Japan, Iran, Argentina, Brazil, Italia, Poland, Ufaransa, Marekani na Tunisia tayari zimejikatia tiketi za kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020. Iran iliibuka ya tano katika michezo iliyopita ya Olimpiki jijini Rio nchini Brazil.

Voliboli: Malkia wa Kenya watinga Olimpiki

Timu ya taifa ya voliboli ya Kenya kwa upande wa wanawake, Malkia Strikers, imejikatia tiketi ya kuingia kwenye mashindano ya Olimpiki mwaka huu yatakayofanyika mjini Tokyo, Japan. Malkia Strikers walipata mpenyo huo baada ya kuitafuna Nigeria walipokutana katika mashindano ya mataifa ya Afrika ya kufuzu Olimpiki katika mechi iliyochezwa Yaoundé, Cameroon. Malkia walianza kwa kishindo baada ya kuinyuka Nigeria 25-15 kwenye seti ya kwanza, raundi ya pili wakawapepeta 25-21 na kisha kuwamalizia na 25-21. Sasa timu hiyo itashiriki Olimpiki tena baada ya miaka 16 kwani mara ya mwisho kushiriki ilikuwa mwaka 2004 nchini Ugiriki. Na je, Kenya ipo tayari kwa Michezo ya Olimpiki jijini Tokyo mwka huu? Sharon Chepchumba, ni mshambuliaji wa safu ya kushoto wa timu hiyo ya wanawake wa Kenya.

Mbio za kusaka tiketi za kutinga Michezo ya Olimpiki Japan 

 

Kwengineko, timu mbili za mpira wa wavu wa ufukweni za Rwanda kwa upande wa akina dada zimejihakikishia tiketi ya kuingia raundi ya pili kwenye michuano ya kucheza Olimpiki ya Tokyo 2020 kufuatia ushindi dhidi ya Kenya na Uganda. Rwanda iliwakilishwa na timu mbili katika michuano hiyo ya siku tatu ya Sub-Zone 5 iliyofanyika Dar es Salaam, Tanzania. Baada ya raundi hiyo ya kwanza kukamilika, raundi ya pili itafanyika mwezi ujao. Timu zitakazofanya vizuri kwenye raundi ya pili zitafuzu kucheza michuano ya mabingwa ya Afrika itakayofanyika Juni mwaka huu.

Soka Wanawake; Tanzania yaichakaza Burundi

Timu ya Taifa ya Soka ya Wanawake ya Tanzania ya wachezaji wenye chini ya miaka 17 Jumapili ya Januari 12 iliigaragaza Burundi magoli 5-1 kwenye mchezo wa kuwania kufuzu tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa Wanawake. Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mshambuliaji wa Tanzania Asha Masaka alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Burundi. Mlinda mlango wao, Amissa Inarukundo alijikuta akiokoteshwa nyavuni mabao matatu ya hatrick Asha huku Joyce Meshack na Protasia Mbunda wakipachika bao moja moja na kukamilisha jumla ya mabao matano kwa vijana hao wa kike wa Tanzania. Bao pekee la kufuta machozi kwa Burundi lilipachikwa na Nadine Ndayishimiye kutokana na uzembe wa safu ya ulinzi wa timu ya Taifa ya Tanzania. Michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa Wanawake inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini India na mchezo wa marudio kati ya Tanzania na Burundi ukitarajiwa kufanyika Januari 25, Bujumbura.

Ni Sadio Mane 2019

Mwanasoka nyota wa Senegal Sadio Mane, ambaye pi ni winga machachari wa klabu ya Liverpool ya Ligi Kuu ya soka ya Uingereza EPL kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka 2019 wa Afrika. Mane alikabidhiwa tuzo hiyo ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) katika hafla iliyofanyika katika mji wa Hurgada nchini Misri. Tuzo hiyo pia ilikuwa ikiwaniwa na Muhammed Sallah wa Misri (Liverpool) na Riyad Mahrez raia wa Algeria anayekipiga Manchester City. Katika hotuba yake fupi, Mane ameishukuru familia yake, wakufunzi na wachezaji wenzake wa timu ya taifa na Liverpool bila kusahau Shirikisho la Soka Afrika. Mane (27) alikuwa na mchango mkubwa msimu uliopita kuiwezesha Liverpool kutwaa kombe la klabu bingwa barani Ulaya. Kadhalika aliiwezesha timu yake ya taifa ya Senegal kumaliza nafasi ya pili katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Sadio Mane akisujudu baada ya kufunga bao

 

Achraf Hakim wa Real Madrid aliyepo kwa mkopo Borussia Dortmund ndio mshindi wa tuzo ya mchezaji bora kijana. Golikipa wa zamani wa Togo, Kodjovi Obilale aliyestaafu soka 2010 akiwa na miaka 26 kufuatia kushambuliwa kwa basi la Togo nchini Angola na kupata ulemavu wa maisha, alipewa tuzo maalumu. Timu ya wanaume ya taifa ya Algeria ndio imeshinda tuzo ya timu bora ya taifa ya mwaka 2019. Algeria ndio waliibuka mabingwa wa AFCON 2019. Kocha wa Algeria aliyeipa timu yake ubingwa wa AFCON 2019 nchini Misri, Djamel Belmadi ametangazwa kocha bora wa Afrika kwa mwaka 2019. Timu ya taifa ya wanawake ya Cameroon ndio imeshinda tuzo ya timu bora ya taifa ya wanawake 2019.

Madrid watwaa Super Cup

Klabu ya Real Madrid imetwaa taji la Super Cup la Uhispania kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2017. Hii ni baada ya Madrid kuisasambua Atletico Madrid mabao 4-1 katika mikwaju ya penati, baada ya muda wa kawaida na ziada kumalizika wakiwa na sare tasa. Mechi hiyo ya aina yake ilipigwa Jumapili katika Uwanja wa Mfalme Abdullah mjini Jeddah nchini Saudi Arabia. Waliocheka na nyavu na kuifanya Madrid inayonolewa na Zinedine Zidane iibuke kidedea ni Dani Carvajal, Rodrygo, Luka Modric na Sergio Ramos.

Suhula za mchezo wa tenisi

 

Na kwa kutamatisha, mchezaji nyota wa tenisi duniani Novak Djokovic amemcharaza Rafael Nadal katika fainali ya Kombe la ATP na kutwaa tuzo hiyo. Katika mchezo huo wa Jumapili mjini Sydney, Djokovic ambaye ni raia wa Serbia hakumpa nafasi ya kupumua hasimu wake wa Uhispania Rafael Nadal ambaye alilazimika kukubali kuchakazwa kwa seti 6-2 na 7-6.

Nadal alionyeshwa kivumbi hicho Jumapili usiku licha ya kuwa ni mchezaji tenisi nambari moja duniani hivi sasa.

……………………TAMATI………………