Feb 21, 2020 13:25 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu Kurejea Imam tarehe 12 Bahman 1357 Shamsia, sawa na Februari Mosi 1979 (1)

Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika mfululizo huu wa vipindi kadhaa tulivyokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran.

Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa mfululizo huu ambao tutakuwa nao kila siku hadi yatakapofikia kileleni maadhimisho hayo yaani hadi tarehe 11 Februari. Katika kipindi cha leo tuutazungumzia kurejea nchini Iran Imam Khomeini (MA) kutokea uhamishoni hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Asubuhi ya tarehe 12 Bahman 1357 Hijiria Shamsia sawa na Februari Mosi, 1979 Miladia, wananchi wa  walikuwa katika shamrashamra iliotawaliwa na matumaini tele. Imam Khomeini (MA) Kiongozi wao mtukufu anayependwa licha ya kuwepo vitisho vingi na ukwamishaji mambo wa utawala wa Shah, alikuwa akisubiriwa kwa hamu kuwasili nchini hapa kwa ndege ya shirika la ndege la Ufaransa. Kiongozi huyo wa wananchi na wa kiroho ambaye alikuwa ametengwa mbali na wananchi wake wa Iran kwa kipindi cha miaka 14, sasa alikuwa anarejea na ushindi kwa wananchi. Baada ya Mfalme Shah kibaraka wa madola ya Magharibi kukimbia nchi hapo tarehe 26 Dei 1357 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 16 Januari 1979, Imam Khomeini alitangaza uamuzi wake wa kurejea nchini.

Rubani wa ndege iliyomleta Imam Khomeini akiwa amemshika mkono akimsaidia kushuka ndege hiyo Februari Mosi 1979

Uamuzi huo wa kishujaa na wa hatari pia uliwatia wasi wasi mkubwa wapenzi na wapinzani wa mtukufu huyo. Wananchi wa Iran na licha ya kwamba walikuwa wamefanya subira ya muda mrefu ya kumgonjea kiongozi wao huyo, pia walikuwa na wasi wasi kwamba vibaraka wa utawala wa kitwaghuti watamsababishia madhara katika safari yake hiyo ya kurejea nchini. Kwa upande mwingine nao utawala wa Shah na waungaji mkono wake wa Kimarekani na Wamagharibi walikuwa wanajua kwamba kurejea Imam Khomeini nchini Iran kutazidisha moto wa harakati za kimapinduzi na hatimaye kufikiwa Ushindi wa Mapinduzi hayo ya Kiislamu ya wananchi. Katika uwanja huo baada ya imam kuazimia kurejea nchini, kulianza harakati nyingi za kuzuia safari yake hiyo ya kihistoria. Mkabala wake wanamapinduzi miongoni mwa wananchi walitumia uwezo wao wote kwa ajili ya kuzishinda njama hizo za maadui ili kufanikisha mtukufu huyo anawasili nchini hapa kwa amani.

**********

Harakati ya kwanza na muhimu iliyofanywa na wananchi Waislamu wa Iran siku tatu baada ya Shah kukimbia nchi, ilikuwa ni kufanya maandamano katika marasimu ya Arubaini ya Imam Hussein (as). Siku hiyo mamilioni ya Wairan walifanya maandamano makubwa katika miji tofauti ya Iran wakisisitizia udharura wa kurejea kiongozi wao mpendwa (Imam Khomeini MA.) Tukio hilo muhimu lililofanyika siku ya Arubaini ya Imam Hussein lilionyesha kwamba raia wa nchi hii bado wanashikamana na harakati ya mwamko wa Imam Hussein (as) kwa ajili ya kufikia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika uwanja huo maafisa wa utawala wa Shah chini ya uongozi wa Robert Huyser, mjumbe maalumu wa kijeshi wa Marekani nchini Iran, walitoa pendekezo la kuzuia safari ya Imam Khomeini kuwasili Iran, ikiwemo kupindisha mwelekeo wa ndege iliyombeba mtukufu huyo ambapo badala ya ndege hiyo kutakiwa kutua mjini Tehran, walitaka itue katika uwanja wa ndege mwingine. Licha ya uamuzi huo, Imam aliatangaza tarehe sita Bahman yaani sawa na tarehe 26 Januari 1979, kuwa siku atakayorejea nchini.

Imam Khomeini kabla ya kuanza safari kuelekea Iran

Ni wakati huo ndipo mabaki ya viongozi wa utawala wa Shah wakiongozwa na Shapour Bakhtiar, wakatangaza kuwa viwanja vyote vya Iran vitafungwa na hakuna ndege itayoruhusiwa kutua siku hiyo. Hatua hiyo ya serikali iliibua hasira kali za wananchi. Kufuatia tangazo hilo ndipo kukaibuka maandamano, migomo na machafuko makubwa nchini, sambamba na askari wengi kujiunga na wananchi hata ndani ya safu ya viongozi wa ngazi ya juu wa kijeshi. Katika ujumbe alioutuma kwa wananchi Imam Khomeini alisisitza kuwa siku chache zijazo atafika Iran na kwa kuwa wanajeshi wako pamoja na wananchi wakipambana na ukoloni na udikteta, watafikia ushindi kamili wa mapinduzi. Katika tarehe sawa na aliyofariki dunia Mtume Muhammad (saw) wananchi wa Iran sambamba na kufanya maandamano makubwa na ya hamasa katika miji tofauti ya Iran, walitangaza pia azma yao ya kuendeleza mapinduzi na hatimaye kurejea nchini kiongozi wao. Hata hivyo vibaraka wa Shah pia walitumia nguvu kubwa kuwakandamiza wananchi na kupelekea maelfu ya raia kuuawa shahidi wakiwemo wanawake wanamapinduzi.

**********

Katika uwanja huo wanazuoni wakubwa wa kidini walilalamikia hatua ya serikali ya kufunga uwanja wa ndege ambapo walifanya mgomo katika msikiti wa Chuo Kikuu cha mjini Tehran. Mgomo huo uliungwa mkono na maafisa wengi wa jeshi kama ambavyo maulama wa miji mingine pia walitekeleza hatua kama hiyo kwa kufanya mgomo misikitini na maeneo ya umma. Mashinikizo hayo yaliifanya serikali kulazimika kurejea nyuma na kutangaza kuwa sasa Imam Khomeini anaweza kutua Iran kupitia uwanja wa ndege wa Tehran. Bila kuchelewa kamati ya mapokezi ya kumlaki Imam ambayo ilikuwa imeundwa tangu awali, ilitangaza tarehe 12 Bahman kuwa siku rasmi ya kurejea mtukufu huyo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku hiyo. Siku moja kabla ya tarehe hiyo akthari ya raia wa Iran kutoka miji tofauti waliwasili mjini Tehran kwa ajili ya maandalizi ya mapokezi hayo ya kihistoria. Njia zote kuanzia uwanja wa ndege wa Mehr Abad wa mjini Tehran hadi katika makaburi ya Behesht Zahraa (as), eneo walipozikwa maelfu ya mashahidi wa mapinduzi ya Kiislamu, zilikuwa zimepambwa kwa maua. Ni wakati huo ambapo Imam Khomeini alitoa shukurani kwa Ufaransa kutokana na kumpa hifadhi kwa kipindi chote alichokuwa huko. Akiwa pamoja na idadi kadhaa ya wafuasi wake akaingia ndani ya ndege kuelekea Iran. Katika hali ambayo watu wote walijawa na wasi wasi na khofu, ni imam pekee ambaye alikuwa na utulivu wa nafsi. Mtukufu huyo akiwa na utulivu uliotokana na imani yake ya hali ya juu ya kumtegemea Mwenyezi Mungu akaanza safari kuelekea katika nchi yake asilia ambapo pia alipata kusali swala za usiku na alfajiri ndani ya ndege kwa ikhlasi na unyenyekevu wa hali ya juu.

***********

Katika uwanja wa ndege wa Mehr Abad kulikuwa na vifijo na nderemo ambapo baadhi ya wananchi walikuwa na khofu na wasi wasi huku wengine wakimsubiria kiongozi wao aweze kuwasili na kumlaki kwa furaha. Hatimaye ndege iliyombeba Imam Khomeini ikafanikiwa kutua salama na bila ya tatizo lolote sawa na saa tatu na nusu asubuhi katika siku ya tarehe 12 Bahman 1357 Hijiria Shamsia sawa na Februari Mosi 1979. Maelfu ya wananchi walipanga safu kuanzia uwanja wa ndege hadi makaburi ya Behesht Zahra (as) kwa ajili ya kumuona kipenzi chao huyo. Akiwa eneo hilo Imam Khomeini alitoa hotuba fupi akiwashukuru wananchi wote wa Iran sambamba na kuwasisitiza juu ya umoja na mshikamano. Aidha alisema kuwa kumfurusha Shah nje ya nchi ilikuwa ni hatua ya kwanza ya Ushindi wa Mapinduzi na kwamba hatua ya pili ilikuwa ni kuwatimua vibaraka na kukatwa vyanzo vyote vya utawala wa Shah nchini Iran.

Maenlfu ya Wairan waliofika kumlaki kiongozi wao

Ndugu wasikilizaji hivi sasa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yametimiza miongo minne tangu yalipopata ushindi wake. Katika kipindi hicho kuna matunda mengi na ya kila namna yaliyopatikana kutokana na Mapinduzi hayo matukufu na matunda ya juu kabisa ni kukata kikamilifu utegemezi wa taifa la Iran kwa mabeberu katika upande wa kisiasa na kiutamaduni. Aidha mapinduzi hayo yameliletea taifa la Iran maendeleo ya kiuchumi, uhuru unaokwenda sambamba na kujali watu majukumu yao, kujiamini na kupata nguvu fikra ya kupigania ukombozi na uadilifu. Hata hivyo Mapinduzi ya Kiislamu tangu yalipopata ushindi hadi kwenye kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Saddam huko Iraq na baada ya vita hivyo, yamekuwa yakikabiliwa na njama za kila namna za kijeshi na kisiasa kutoka kwa maadui, lakini pamoja na yote hayo, taifa la Iran halijatetereka hata kidogo na badala yake limefanikiwa kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kwa kutegemea uwezo wake wa ndani na kufanikiwa kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya mawimbi na mashambulizi ya kila upande ya maadui.

Na kufikia hapa muda wa kipindi chetu cha Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran sehemu ya kwanza, ndio umefikia tamati. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, kwaherini.

 

Tags