Feb 28, 2020 01:18 UTC
  • Ijumaa tarehe 28 Februari 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 4 Rajab 1441 Hijria sawa na Februari 28 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 498 iliyopita, ilianza harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Sweden dhidi ya utawala wa Christiane wa Pili, mtawala wa Denmark ambaye alizikalia kwa mabavu Sweden na Norway. Kiongozi wa harakati hiyo alikuwa Gustav Vasa. Hatimaye kwa msaada wa wakulima, wananchi na wafuasi wa Uprotestanti, Vasa alifanikiwa kuikomboa nchi hiyo kutoka mikononi mwa mtawala Christiane wa Denmark. Baada ya mapinduzi hayo, Gustav Vasa akawa kiongozi wa Sweden. Silsila ya utawala wa Vasa ulioendelea kwa karibu karne tatu, iliondolewa madarakani mwaka 1818 na Marshall Baptiste Bernadotte, mmoja wa makamanda wa jeshi la Ufaransa.

Gustav Vasa

Siku kama ya leo miaka 487 iliyopita, alizaliwa Michel de Montaigne, mtaalamu wa falsafa wa Ufaransa. Akiwa kijana mwenye umri wa miaka 13, Montaigne alijiunga na chuo kikuu cha Toulouse na kusomea taaluma la sheria. Baada ya masomo yake alianza kufanya kazi za mahakama huku akifanya utafiti juu ya falsafa. Montaigne ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Makala’ chenye juzuu tatu kinachozungumzia masuala mbalimbali. Michel de Montaigne alifariki dunia mwaka 1592.

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita sawa na tarehe 28 Februari 1922, nchi kongwe ya Misri ilipata uhuru. Misri ilikombolewa na Waislamu miaka 20 baada ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu. Mwaka 969 nchi hiyo ilidhibitiwa na kutawaliwa na silsila ya wafalme wa Fatimiyya hadi mwaka 1172 ambapo utawala huo ulipinduliwa na Maayyubi. Baada ya hapo Misri ilidhibitiwa na tawala tofauti. Waingereza walianza kuwa na ushawishi huko Misri katika miongo ya mwishoni mwa karne ya 19. Hata hivyo wananchi wa Misri walikabiliana na ukoloni wa Uingereza na mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia hapo mwaka 1914 Uingereza iliitangaza Misri kuwa chini ya himaya yake. Wananchi wa Misri walidumisha mapambano ya uhuru baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kuilazimisha Uingereza kuutambua rasmi uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1922.

Bendera ya Misri

Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Muhsin Amin al Amili, alimu na mwanafasihi mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1284 Hijria katika eneo la Jabal Amili nchini Lebanon na kupata elimu ya msingi ya Kiislamu nchini humo. Ayatullah Sayyid Amin alielekea Najaf nchini Iraq akiwa na umri wa miaka 24 kwa shabaha ya kukamilisha elimu ya juu na kupata elimu kwa maulamaa wakubwa wa mji huo. Baadaye alielekea Syria na kutoa huduma kubwa za kufundisha Uislamu. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi muhimu zaidi kikiwa kile cha A'yanul Shia chenye juzuu kumi. Katika kitabu hicho Sayyid Muhsin al Amin amearifisha vinara wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia hususan maimamu watoharifu katika kizazi cha Bwana Mtume (saw) na mchango wao katika kuimarisha ustaarabu wa Kiislamu. Kitabu kingine cha msomi huyo ni Kashful Irtiyab fii Atba'I Muhammad bin Abdul Wahhab kinachofichua na kukosoa itikadi za kundi potofu la Kiwahabi.

Ayatullah Sayyid Muhsin Amin al Amili

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 28 Februari 1986, aliuawa Olof Palme Waziri Mkuu wa zamani wa Sweden baada ya kufyatuliwa risasi tumboni kwenye shambulio lililofanyika barabarani katikati mwa Stockholm, mji mkuu wa nchi hiyo. Katika shambulio hilo, Bi. Lisberth mke wa Olof pia alijeruhiwa mgongoni.

Olof Palme

Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita inayosadifiana na 28 Februari 1991, George Bush "baba" alitangaza usitishaji vita vya Ghuba ya Uajemi vilivyoendelea kwa muda wa siku 40. Mgogoro huo ulianza mwezi Agosti 1990 baada ya majeshi ya Iraq kushambulia ghafla sehemu ya ardhi ya Kuwait na kuikalia kwa mabavu. Ndege za kijeshi za Marekani, Uingereza na Ufaransa zilianza kuyashambulia majeshi ya Iraq baada ya utawala wa Saddam Hussein kukataa amri ya kuyaondoa majeshi yake nchini Kuwait.

 

Tags