May 11, 2020 00:21 UTC
  • Jumatatu, 11 Mei, 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 17 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 11 Mei 2020 Miladia..

Siku kama ya miaka 1442 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia Mtume Mtukufu Muhammad SAW alisafiri kutoka Makka hadi Baitul Muqaddas na kupaa mbinguni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Aya ya kwanza ya Sura ya al Isra inatoa maelezo kuhusu muujiza huo mkubwa ikisema. "Ametakasika aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara zetu. Hakika yeye ni mwenye kusikia na mwenye kuona." Kwa kuzingatia aya hiyo na hadithi za Mtume Muhammad SAW, wakati mtukufu huyo alipokuwa katika safari ya Miiraji alionyeshwa siri nyingi za Mwenyezi Mungu SW, viumbe vyake Jalali na hatima ya wanadamu katika ulimwengu wa Akhera. Tukio hilo ni miongoni mwa miujiza mikubwa ya Mtume Muhammad SAW na linadhihirisha nafasi ya juu ya mtukufu huyo. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, vita vya Badr, moja kati ya vita maarufu vya Mtume Muhammad SAW, vilitokea katika eneo lililoko kati ya Makka na Madina. Badr ni jina la kisima kilichoko umbali wa kilomita 120 kusini magharibi mwa mji wa Madina, ambako kulipiganwa vita vya kwanza kati ya Waislamu na washirikina. Vita vya Badr vilitokea huku washirikina wakiwa na wapiganaji wengi waliokaribia 920 na jeshi la Kiislamu likiwa na wapiganaji 313 na silaha chache. Hata hivyo imani thabiti ya Waislamu iliwafanya washinde vita hivyo. ***

Vita vya Badr

 

Miaka 324 iliyopita sawa na tarehe 11 Mei mwaka 1696 Miladia, alifariki dunia mwandishi na mwanafikra wa Kifaransa, Jean de La Bruyère. De la Bruyère alizaliwa mwaka 1645 Miladia, na kuwa wakili baada ya kutabahari katika elimu ya sheria. Hata hivyo baadaye aliachana na kazi ya uwakili na akaanza kufanya kazi serikalini, huku akijifunza masuala ya maadili na tafakuri ya mwanadamu katika zama zake. Mwandishi huyo wa Kifaransa ameandika vitabu vingi vinavyohusu utamaduni, mila na mienendo ya mwanadamu. Kadhalika ametoa mchango mkubwa katika uga wa fasihi ya Kifaransa. ***

Jean de La Bruyère

 

Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita,  alizaliwa Ethel Lilian Voynich mwandishi wa Ki-Ireland. Akiwa na umri wa miaka 21, Bi Lilian alielekea Russia na kusoma fasihi ya lugha ya Kirusi. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanza taratibu kuwa na shauku na fani ya uandishi na fasihi ya lugha. Bi Ethel Lilian aliaga dunia mwaka 1960. ***

Ethel Lilian Voynich

 

Katika siku kama ya leo miaka 153iliyopita, sawa na tarehe 11 mwezi Mei mwaka 1867 Miladia, iliundwa nchi ya magharibi mwa bara Ulaya ya Luxembourg. Awali Luxembourg ilifahamika kama Lutxenbourg katika karne ya 10 hadi 15, ikiwa sehemu ya Utawala wa Roma. Hadi katikati ya karne ya 19, nchi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na serikali na watawala wa madola yaliyokuwa na nguvu na ushawishi wakati huo Ulaya. Luxembourg ambayo imezungukwa na Ubelgiji, Ufaransa na Ujerumani, ilitangazwa kuwa nchi huru katika Kongamano la London lililofanyika Mei 11 mwaka 1867 katika mji huo mkuu wa Uingereza na kuanza kutambulika kimataifa. ***

Luxembourg

 

Miaka 115 iliyopita katika siku kama ya leo, Salvador Felipe Dali, mchoraji na mchongaji wa sanamu za mawe na mtaalamu wa sanaa ya maandishi au Graphic Arts wa Kihispania alizaliwa. Alianza kuonyesha kipaji chake katika sanaa ya uchoraji akiwa kijana mdogo na kwa muda mfupi tu akawa mashuhuri kimataifa. Salvador Felipe Dali alikuwa na kipaji cha aina yake na ubunifu katika taaluma hizo na ndiye anayehesabiwa nchini Uhispania kuwa mwasisi wa uchoraji wa kisasa. Mwanasanaa huyo stadi aliaga dunia mwaka 1989. ***

Salvador Felipe Dali,

 

Katika siku kama ya leo miaka 85 iliyopita,  kituo cha kwanza cha kurushia matangazo ya televisheni kwa jina la Nipkow kilianza kazi rasmi katika mji wa Berlin huko Ujerumani, hatua ambayo iliwawezesha watu kuanza kutumia runinga au televisheni. Kituo hicho kilipewa jina la Nipkow kwa shabaha ya kumuenzi Paul Gottlieb Nipkow ambaye alikuwa miongoni mwa wavumbuzi asili wa televisheni. Nipkow alivumbua njia ya kubadili picha na kuwa mawimbi na kisha kuyarejesha mawimbi hayo katika sura ya picha. ***

Paul Gottlieb Nipkow

 

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, vikosi vya pamoja vya Uingereza na Ufaransa viliingia nchini Ubelgiji kwa shabaha ya kuiunga mkono nchi hiyo iliyokuwa imevamiwa na Ujerumani ya Kinazi. Kuitetea Ubelgiji ni jambo lililokuwa limetiliwa mkazo katika mkataba baina ya Uingereza na Ufaransa. Licha ya Uingereza na Ufaransa kuwa pamoja, jeshi la Ujerumani ya Kinazi si tu kwamba, lilitoa pigo kwa jeshi la Ubelgiji, bali lilivishinda pia vikosi vya Ufaransa na Uingereza na kudhibiti maeneo yote ya ardhi ya Ubelgiji.***

Vita vya Pili vya Dunia

 

Miaka 50 iliyopita na kwa mujibu wa azimio nambari 278 la Umoja wa Mataifa nchi ya Bahrain ilitengwa na ardhi ya Iran. Kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo ndogo iliyo katika Ghuba ya Uajemi ilikuwa katika utawala wa Iran na baada ya kubuniwa utawala wa Kiislamu ikawa inadhibitiwa na makhalifa wa Kiislamu. Mwanzoni mwa karne ya 7 Hijiria kwa mara nyingine tena nchi hiyo iliunganishwa na Iran na baada ya hapo ikawa chini ya himaya ya Uingereza. Licha ya hayo Iran iliendelea kudai udhibiti na utawala wake kwa Bahrain na kulalamikia vikali hatua ya Uingereza ya kuitawala nchi hiyo.***

Bahrain

 

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, yaani tarehe 22, Ordibehesht, mwaka 1364 Hijria Shamsia, makumi ya watu waliuawa shahidi na kujeruhiwa kutokana na shambulizi la bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la Munafiqiin (MKO) mjini Tehran. Mripuko huo mbali na kusababisha uharibifu mkubwa, uliteketeza kikamilifu jengo moja la ghorofa mbili na karakana ya ufumaji nguo katika barabara ya Naser Khosro na kuua watu 9 na kujeruhi wengine 45.  Mauaji hayo ya kinyama kwa mara nyingine tena yaliidhihirishia dunia jinai za k  utisha za kundi la kigaidi la MKO, lenye kuungwa mkono na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni. ***

Mlipuko wa bomu katika barabara ya Naser Khosro

 

Tags