Jumanne tarehe Pili Juni 2020
Leo ni Jumanne tarehe 10 Shawwal 1441 Hijria sawa na tarehe Pili Juni 2010.
Siku kama ya leo miaka 1113 iliyopita alifariki dunia Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Muqlah, mwandishi, mwanakaligrafia na mvumbuzi wa hati tofauti za uchoraji. Alizaliwa Baghdad na kujifunza masomo ya dini kwa wasomi mashuhuri wa mji huo. Ibn Muqlah aliingia katika idara ya vyombo vya mahakama katika utawala wa Bani Abbas akiwa kijana. Hata hivyo muda mfupi na kutokana na upinzani wake mkali dhidi ya utawala na mienendo iliyokuwa kinyume na dini ya watawala wake, msomi huyo alikamatwa na kufungwa jela. Hatimaye na kutokana na amri ya mtawala wa wakati huo, watumishi wa utawala walimkata ulimi na mikono msomi huyo na kisha kumuua shahidi. Miongoni mwa vitabu vya Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi ni pamoja na 'Risaalat fi Ilmil-Khat wal-Qalam' na 'Risalatun fi Mizaanil-Khat.'

Miaka 138 iliyopita katika siku kama leo, alifariki dunia Giuseppe Garibaldi kamanda mzalendo na kiongozi wa harakati ya umoja wa Italia. Wakati wa ujana wake alifanya kazi mbalimbali na mwishowe alijiunga na jeshi. Baadaye alichaguliwa kuwa kamanda wa wanaharakati wa kupigania uhuru wa Italia na alifanya jitihada kubwa za kuimarisha umoja nchini humo. Kwa sababu hiyo alijulikana katika historia ya Italia kama shujaa wa taifa.

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, mnamo tarehe Pili Juni mwaka 1942 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Mjerumani Marshal Erwin Rommel maarufu kwa jina la Mbwa Mwitu wa Jangwani, alianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Uingereza katika maeneo ya kaskazini mwa Afrika. Kabla ya mashambulizi hayo, Waingereza walikuwa wamefanya hujuma nchini Libya na kuitwaa nchi hiyo kutoka mikononi mwa jeshi la Wajerumani wa Kinazi. Hata hivyo mashambulizi ya jeshi la Erwin Rommel ambayo yalidumu kwa kipindi cha mwezi mmoja yaliwawezesha wanajeshi wake kuidhibiti tena Libya na eneo la al Alamein lililoko kaskazini mwa Misri na karibu na bandari muhimu ya Alexandria. Wajerumani walikaribia kuutwaa mfereji wa kistratijia wa Suez lakini mwezi Novemba mwaka 1942 Waingereza wakafanya mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Erwin Rommel na hatimaye kulishinda.
Na katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, Imam Khomeini (M.A), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba kali ya kihistoria dhidi ya utawala wa kitwaguti wa Iran, kwa mnasaba wa Ashura ya Imam Husseini (A.S). Imam Khomeini alitoa hotuba hiyo mbele ya hadhara kubwa ya wananchi na wanazuoni katika Madrasa ya Faidhiya katika mji mtakatifu wa Qum hapa nchini, licha ya vizuizi na vitisho vya utawala wa Shah. Imam alikosoa vikali usaliti wa utawala wa Shah na vibaraka wake na kukosoa hiyana ya utawala huo dhidi ya wananchi Waislamu wa Iran. Sehemu ya hotuba ya Imam Khomeini ilisema hivi kama ninavyomnukuu: "Watu hao wanapinga Uislamu na wanazuoni na wana nia ya kuutokomeza. Enyi wananchi, dini yetu ya Kiislamu na nchi yetu viko hatarini na tuna wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Iran," mwisho wa kunukuu.
