Jun 30, 2020 02:34 UTC
  • Jumanne tarehe 30 Juni mwaka 2020

Leo ni Jumanne tarehe 8 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Juni 30 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1093 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Ibn Zubair, mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa wakati huo. Katika ujana wake Ibn Zubair alisoma kwa baba yake elimu muhimu tofauti za wakati huo. Baada ya baba yake kufariki dunia aliutumia utajiri wa baba yake huyo katika njia ya kutafuta elimu, kuasisi maktaba na kuwasaidia wanafunzi wa kidini waliokuwa na hali ngumu ya kimaisha. Mbali na uhodari mkubwa katika uandishi, Ibn Zubair alikuwa na kipawa pia cha kuandika upya baadhi ya vitabu vya wasomi wengine na kuvieneza.

Siku kama ya leo miaka 1062 iliyopita, alifariki dunia Abu Hamid Swaghani, mtaalamu wa nujumu na hesabati wa Iran. Abu Hamid alizaliwa mjini Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran, na baadaye kuhamia mjini Baghdad Iraq. Msomi huyo alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika uga wa elimu ya nujumu na hisabati wa zama zake sanjari na kuasisi kituo cha unajimu mjini Baghdad. Msomi huyo ameacha vitabu vingi katika fani ya nujumu.

Siku kama ya leo miaka 1056 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Ali bin Omar Dar-Qutni, mwandishi na mtaalamu wa sheria za Kiislamu. Dar-Qutni alifanya safari nchini Misri na Sham na kuweza kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo. Aidha msomi huyo alikuwa hodari pia katika tafsiri ya Qur’an Tukufu, fiq’hi, mashairi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya ‘as-Sunan’, ‘Sunan Daru Qutni’ na ‘al-Mukhtalif wal-Mu’talif.’

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire ya zamani) ilijitangazia uhuru na Joseph Kasavubu akawa rais wa nchi hiyo, huku Patrice Lumumba akiwa Waziri Mkuu. Kongo ilikoloniwa na Ubelgiji. Mapambano ya kudai uhuru yaliyoongozwa na Patrice Lumumba yalishika kasi katika miaka ya mwisho ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia na kupelekea nchi hiyo kujipatia uhuru wake. Hata hivyo baada ya Kongo kupata uhuru zilianza harakati nyingi za uasi zilizokuwa zikiungwa mkono na Ubelgiji. Katika upande mwingine kulishadidi mapigano kati ya Lumumba na Musa Chumbe kiongozi aliyekuwa akiungwa mkono na Ubelgiji. Hatimaye mnamo mwaka 1965 Jenerali Mobutu Sese Seko aliyeungwa mkono na Marekani alifanya mapinduzi ya kijeshi na kutwaa madaraka ya nchi hiyo ambapo badaye alianza kuwakandamiza wananchi masikini wa Kongo.

Bendera ya Congo

Miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Omar Hassan Ahmad Al Bashir wa Sudan aliongoza mapinduzi ya kijeshi na kuuangusha utawala wa Swadiq Al Mahdi bila ya umwagaji damu. Utawala huo ulikuwa ukikabiliwa na matatizo mbalimbali ya ndani. Baada ya mapinduzi hayo Omar Hassan Al Bashir kwa kushirikiana na Hassan Al Turabi alianzisha chama cha Kongress ya Kitaifa huku yeye akiwa mwenyekiti wa chama hicho na rais wa nchi. Baada ya Al Bashir kutwaa urais alijitahidi kujitenga na siasa za Marekani, hatua ambayo iliipelekea serikali ya Washington kuichukia Khartoum.na kuanzisha hatua za kiaduai dhidi ya serikali ya Al Bashir. Miongoni mwa hatua za kiadui zilizochukuliwa na Marekani dhidi ya Sudan ni kuwaunga mkono waasi wa Kusini mwa Sudan ambapo mwaka 2011 eneo hilo la kusini lilijitenga na Sudan na kujitangazia uhuru wake. Hata hivyo al Bashir alibadilisha mielekeo yake na kuwa tegemezi kwa utawala mwa kifalme wa Saudi Arabia. Utawala wa al Bashir ulitafunwa na ufisadi, utumiaji mbaya wa madaraka, hali mbaya ya uchuumi na kufuata kibubusa sera za Saudi Arabia katika vita vya Yemen. Mambo haya yaliwakasirisha Wasudani walioanzisha harakati ya upinzani dhidi ya al Bashir na hatimaye tarehe 11 Aprili mwaka 2019 kiongozi huyo alilazimika kung'atuka madarakani na kutiwa nguvuni kwa tuhuma za ufisadi na utakatishaji wa fedha chafu. Omar al Bashir anatumikia adhabu ya kifungo.

Omar al Bashir

Na katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, mfumo wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ulihitimishwa. Kuanzia mwaka 1948, wazungu walio wachache nchini Afrika Kusini walianza kutekeleza siasa za kibaguzi dhidi ya wazalendo weusi. Kwa mujibu wa siasa hizo, wazungu waliokuwa wakiunda asilimia 20 tu ya wananchi wa Afrika Kusini walihesabiwa kuwa jamii bora zaidi na iliyokuwa na nafasi muhimu katika uendeshaji wa masuala ya nchi hiyo. Sheria za kibaguzi kama vile za kupiga marufuku watu weusi kuoana na watu weupe na vilevile kushiriki katika harakati za kisiasa ni baadhi tu ya sheria za kibaguzi zilizotekelezwa na makaburu nchini Afrika Kusini. Siasa hizo ziliwakasirisha mno walimwengu na nchi nyingi duniani kukata uhusiano na utawala huo.

Shujaa wa ukombozi wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela

 

Tags