Aug 31, 2020 03:14 UTC
  • Jumatatu tarehe 31 Agosti mwaka 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 11 Mfunguo Nne Muharram mwaka 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 31 Agosti mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita, yaani tarehe 11 Muharram mwaka 61 Hijiria, msafara wa mateka wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (saw), baada ya tukio chungu la mauaji ya siku ya Ashura, ulianza safari ya kelekea Sham, yalikokuwa makao makuu ya utawala wa dhalimu wa Yazidi bin Muawiya. Baada ya majeshi ya Yazidi yaliyokuwa yakiongozwa na Omar bin Sa’ad kumuua shahidi Imam Hussein (as) na masahaba wake, majeshi hayo ambayo hayakuwa na chembe ya ubinadamu moyoni, yalianza kupora vitu vya thamani vya msafara wa watu wa familia ya Mtume (saw). Askari hao sanjari na kuchoma moto mahema ya Imam Hussein (as) na watu wake, waliwanyang’anya pia wanawake mapambo yao na kila walichokuwa nacho. Jioni ya siku kama ya leo msafara wa familia ya Imam Hussein uliokuwa ukiongozwa na Imam Sajjad (as) na Bibi Zainab (as), ulielekea Kufa na baadaye Sham.

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, nchi ya Malaysia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Wananchi wa Malaysia walianza kuingia taratibu katika dini ya Uislamu katika karne ya 13 Miladia. Ushawishi wa nchi za Ulaya ulianza kuenea nchini humo mwanzoni mwa karne ya 16 sambamba na kuwasili nchini humo baharia wa Kireno, Albuquerque. Uholanzi iliidhibiti nchi hiyo katika karne ya 17 na kuanza kuikoloni. Mwaka 1824 nchi za Uholanzi na Uingereza zilifikia makubaliano ambapo Waingereza waliichukua Malaysia na Waholanzi wakachukua Indonesia. Waingereza waliendelea kuikolonia Malaysia hadi nchi hiyo ilipopata uhuru katika siku kama ya leo.

Bendera ya Malaysia

Miaka 53 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani. Alizaliwa tarehe 17 Juanuari mwaka 1891 huko Kiev nchini Ukraine. Ilya ambaye anatambuliwa kuwa mkosoaji, mwandishi wa tamthilia, riwaya na hadithi alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Ulaya hususan Uhispania. Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 na miongoni mwa vitabu hivyo ni kile cha "tufani" na "kuanguka kwa Paris".

Ilya Ehrenburg

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Imamu Mussa Sadr, mwanazuoni na msomi mashuhuri wa Lebanon alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa safarini nchini Libya. Alizaliwa mnamo mwaka 1928 katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya kuhitimu masomo yake alielekea Lebanon. Baada ya kuwasili nchini humo, Imamu Mussa Sadr alichukua hatua kubwa za kuboresha maisha ya Walebanoni waliokuwa katika hali mbaya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Mwanazuoni huyo pia alikuwa muungaji mkono wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina na aliasisi Harakati ya Wanyonge kwa ajili ya kutetea haki za Waislamu wa Lebanon. Hadi sasa juhudi mbalimbali za kutaka kufahamu hatima ya Imamu Mussa Sadr bado hazijazaa matunda.

Imamu Mussa Sadr

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita karibu Waislamu 1,000 wa Iraq waliokuwa katika shughuli ya maombolezo kwenye mji mtakatifu wa Kadhimain waliuawa. Siku hiyo karibu Waislamu milioni moja wa madhehebu ya Shia walikuwa katika maombolezo ya kukumbuka siku ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Mussa al-Kadhim (as). Milipuko kadhaa ya mabomu iliyotokea katika eneo la maombolezo hayo iliwatia hofu waombolezaji hao ambao walianza kukimbia huko na kule na baadhi yao kuanguka chini na kukanyagwa hadi kufa. Baadhi ya wahanga wa tukio hilo pia walianguka kutoka kwenye daraja maarufu la Aimma lililoko katika mji huo wa Kadhimain.

Kadhimain

 

Tags