Alkhamisi tarehe 17 Septemba 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 28 Muharram 1442 Hijria sawa na Septemba 17 mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 786 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, mji wa Baghdad uliokuwa makao makuu ya watawala wa Kiabbasi ulitekwa na Hulagu Khan Mongol baada ya kuuawa Mustaasim aliyekuwa mtawala wa mwisho wa utawala wa Bani Abbas. Mauaji ya mtawala huyo yalihitimisha utawala wa kizazi hicho uliotawala sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kislamu kwa kipindi cha miaka 500. Hulagu Khan Mongol hakusita kufanya mauaji na jinai za aina mbalimbali katika uvamizi wake wa nchi mbalimbali, na baada ya kuteka baadhi ya maeneo ya Iran na kuua watu kwa umati katika maeneo ya mijini na vijijini, aliushambulia mji wa Baghdad na kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya maelfu ya wakazi wake. Vilevile aliharibu na kuvunja nyumba na majengo muhimu ya mji wa Baghdad.

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, aliaga dunia Emil Ludwig mwandika wasifu wa Kijerumani. Alizaliwa 1881 katika mji wa Breslau nchini Ujerumani ambao leo hii ni sehemu ya ardhi ya Poland. Alipata umashuhuri katika nusu ya pili ya karne ya 19 baada ya kuandika wasifu wa Otto Van Bismarck Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, kiongozi wa zamani wa Russia Joseph Stalin, Beethoven na rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Ludwig alikuwa mwandishi wa habari aliyepata nafasi ya kufanya mahojiano na watawala waliokuwa na satua na ushawishi mkubwa katika kipindi hicho kama Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchil na Joseph Stalin.

Tarehe 17 Septemba miaka 59 iliyopita aliuawa waziri mkuu wa zamaji wa Uturuki, Adnan Menderes. Alizaliwa mwaka 1899 na kupata elimu katika taaluma ya sheria. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa bado kijana na alishika hatamu za uongozi nchini Uturuki kama waziri mkuu mwaka 1950. Menderes ambaye alikuwa akifuata siasa za sera za kimarekani, alituma vikosi vya jeshi kushambulia Wakurdi wa nchi hiyo, suala ambalo liliwakasirisha sana wasomi na wanafikra wengi nchini Uturuki. Mwaka 1957 alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Uturuki na kukandamiza maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakipinga utawala wake na kudai marekebisho ya kisiasa. Mwaka 1960 Adnan Menderes aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kufikishwa mahakamani ambapo alihukumiwa kifo kwa kupatikana na hatia ya kuua wanafunzi wa vyuo vikuu, kukiuka katiba ya nchi na kuwa na mahusiano haramu. Usiku wa kutekelezwa hukumu ya kifo, Menderes alifanya jaribio la kujiua lakini madaktari waliwahi kuokoa maisha yake. Hatimaye tarehe 17 Septemba, Adnan Menderes alinyongwa akiwa na umri wa miaka 62.

Na miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Shahrivar mwaka 1367 Hijria Shamsia, aliaga dunia, Ustadh Muhammad Hussein Shahriyar mshairi mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa mjini Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran na baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari katika Chuo cha Dar al-Funun mjini Tehran alijiunga na chuo cha tiba. Hata hivyo baada ya miaka michache aliacha masomo na kurejea katika kijiji alichozaliwa. Ustadh Shahariyar alitoa mashairi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 23. Sambamba na kushadidi harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini, Shahriyar aliungana na wimbi hilo kwa kutumia mashairi yake. Vilevile alikuwa mashuhuri sana kwa kumpenda Mtume wa Ahlubaiti zake na mapenzi hayo yalidhihiri katika tungo na mashairi yake.
