Ulimwengu wa Michezo, Oktoba 5
Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....
Persepolis yatinga fainali ya AFC Champions League
Klabu ya Persepolis ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetinga fainali ya ligi ya kieneo kwa kuigaragaza klabu ya al-Nassr ya Saudi Arabia mabao 5-3. Katika mchuano huo wa Jumamosi wa Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia (AFC Champions League) uliopigwa katika Uwanja wa Jasim Bin Hamad nchini Qatar, timu mbili hizo zilikabana koo, ambapo dakika 90 za ada na 30 za nyongeza hazikutosha kumtoa mshindi. Timu hizo mbili zililazimika kuingia katika mikwaju ya penati baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Al-Nassr ya Saudia walikuwa wa kwanza kucheka nyavu, lakini panga pangua na tikitaka za Wekundu wa Tehran zilizaa matunda na wakafanikiwa kusawazisha mambo katika dakika ya 43, kupitia bao la Mehdi Abdi. Persepolis waliingia uwanjani bila ari, masaa machache baada ya Kamati ya Niadhamu na Maadili ya Shirikisho la Soka Asia (AFC) kumpiga marufuku ya miezi sita mchezaji nyota wa klabu hiyo, Issa Alekasir kwa kile kilichotajwa kuwa utovu wa nidhamu wakati wa kushangilia bao katika mchuano wa robofainali siku ya Jumatano. Licha ya mazonge na masaibu hayo, lakini hatimaye Persepolis walipata ushindi kupitia mikwaju ya penati na kutinga fainali.

Klabu hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sasa inatazamiwa kuisakata ngoma fainali mnamo Disemba 13 mwaka huu. Hapa jijini Tehran, ushindi huo ulisimamisha shughuli zote na kusababisha msongamano mkubwa wa magarai kwa masaa kadhaa, huku Wairani wakishangilia ushindi ho muhimu kwa nderemo, vifijo na hoi.
Kwengineko, mkufunzi wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaita kambini wachezaji 23 kwa ajili ya maandalizi ya michuano miwili ya kirafiki. Dragan Skocic anaandaa kikosi cha kukichezesha katika mechi za kufunzu Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar. Mechi hizi zilipaswa kuchezwa mwaka huu lakini zikaakhirishwa hadi mwakani kutokana na janga la corona. Vijana 23 walioitwa kambini na Scocic wanapasha misuli moto kwa ajili ya kuvaana na Uzbekistan Oktoba 8, na Mali siku tano baadaye. Machui wa Persian wanatazamiwa kuchuana na Wauzbeki mjini Tashkent, huku mechi yao na Mali ikitazamiwa kupigwa mjini Antalya nchini Uturuki Oktoba 13.
Riadha: Kosgei ahifadhi Taji la London Marathon
Mwanariadha nguli wa Kenya Eliud Kipchoge siku ya Jumapili alitolewa tonge mdomoni baada ya kushindwa kuhifadhi taji la mbio za London Marathon. Muethiopia Shura Kitata aliomuonyesha kivumbi Kipchoge katika mbio hizo za kilomita 42.2 kwa upande wa wanaume. Kitata mwenye umri wa miaka 24 alithibitisha uwezo wake baada ya kushinda mbio hizo kwa muda wa saa 2:05.21, huo ukiwa ushindi wake mkubwa katika riadha. Mkenya Vincent Kipchumba alishika nafasi ya pili, sekunde moja tu nyuma ya Kitata, huku nafasi ya tatu ikimuendea Muethiopia Sisai Lemma sekunde tatu nyuma ya Kipchumba. Bingwa mtetezi za mbio hizo Eliud Kipchoge alipigiwa upatu kuibuka mshindi, hasa baada ya Kenenisa Bekele kujiondoa siku ya Ijumaa kufuatia jeraha. Hata hivyo bingwa huyo alimaliza katika nafasi ya nane. Binafsi anasisitiza kuwa, kilichosababisha ashindwe ni vitu viwili, sikio uziba kuziba baada ya kukimbia kilomita 25, na maumivu kwenye sehemu za nyonga.

Wakati huohuo, mwanariadha nyota wa Kenya, Brigid Kosgei kwa upande wake alifanikiwa kuhifadhi taji lake la London Marathon kwa upande wa wanawake. Kosgei alikamilisha mbio hizo kwa muda wa saa 2:18:01, mbele ya mshindani wake Mmarekani Sarah Hall aliyekimbia kwa muda wa saa 2:22:01. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Bingwa wa Dunia upande wa wanawake Ruth Chepngetich kutoka Kenya aliyeshinda kwa muda wa saa 2:22:05. Awali mbio za London Marathon zilipaswa zifanyike mwezi Aprili, lakini ziliahirishwa hadi mwezi Oktoba kufuatia janga la virusi vya corona. Janga hilo pia limesababisha mashindano mengine muhimu duniani kuahirishwa mfano ikiwa ni Michezo ya Olimpiki ya Tokyo.
Dondoo za Hapa na pale
Mshambuliaji matata wa Bayern Munich ya Ujerumani, Robert Lewandowski, 32, ndiye ametawazwa Mwanasoka Bora wa Mwaka 2019-20 katika tuzo zilizotolewa na Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) Alkhamisi ya Oktoba Mosi. Lewandowski ambaye ni nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Poland, aliwapiku kipa Manuel Neuer wa Bayern na kiungo wa Manchester City, Kevin de Bruyne. Mkufunzi Hansi Flick wa Bayern alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka baada ya kumpiga kumbo Julian Nagelsmann wa RB Leipzig na Jurgen Klopp aliyeongoza Liverpool kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa msimu wa 2019-20 baada ya miaka 30. De Bruyne, 29, alitawazwa Kiungo Bora wa Mwaka katika UEFA na kuvunja ukiritimba wa Bayern kwenye tuzo hizo kwa upande wa wanaume mwaka huu. Joshua Kimmich, 25, wa Bayern alituzwa Beki Bora wa Mwaka wa 2019-20. Naye Mannuel Neuer, 34, ambaye pia ni mlinda-lango wa timu ya taifa ya Ujerumani, alitawazwa Kipa Bora wa Mwaka baada ya kutofungwa bao katika jumla ya mechi sita za UEFA. Umahiri wa Neuer langoni pa Bayern ulisaidia waajiri wake kupiga Paris St-Germain (PSG) ya Ufaransa 1-0 kwenye fainali ya UEFA mnamo Agosti 23, 2020 jijini Lisbon Ureno.

Mbali na hayo, mshambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane amekutwa na maambukizi ya virusi vya corona na tayari amejitenga dhidi ya wachezaji wenzake. Taarifa hizo zinajiri baada ya siku tatu zilizopita, kiungo mpya wa timu hiyo Thiago Alcantara kukutwa na maambukizi ya virusi hivyo. Taarifa iliyotolewa kupitia Tovuti ya klabu hiyo inaeleza “Kama ilivyo kwa Thiago tutaendelea kufuata miongozo yote, Mane atajitenga kwa kipindi cha siku kadhaa kitakachohitajika.”
Na uongozi wa klabu ya Yanga ya Tanzania imempiga kalabu nyekundu kocha wake mkuu. Licha ya klabu hiyo kupata ushindi wa magoli 3-0 wikendi hii dhidi ya Coastal Union, lakini uongozi wake umetangaza kumfuta kazi kocha wao mkuu Zlatko Krmpotic raia wa Serbia. Zlatko hadi anatumuliwa Yanga SC alikuwa ameiongoza timu hiyo katika michezo 5 na ameshinda mechi nne na sare moja, sare mchezo mmoja, lakini ushindi wake wa Jumapili ndio mnono wa kwanza wa zaidi ya goli.
Masaibu ya klabu hiyo ambayo inasika rekodi ya kutimua makocha hayakuishia hapo, taarifa kutoka Bodi ya Ligi Tanzania mnamo Ijumaa ya Oktoba 2 kuhusu matukio mbalimbali ambayo yamefanyiwa maamuzi baada ya Kamati ya Kusimamia Ligi Kuu Bara kupitia matukio mbalimbali. Miongoni mwa waliopewa adhabu ni pamoja na mashabiki wa Klabu ya Yanga ambao waliwapiga mashabiki wa Simba na kuwachania jezi kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Adhabu waliyopewa ni pamoja na faini na kufungiwa kuingia uwanjani kwa muda wa miezi 12.
………………………TAMATI…..…………..