Nov 24, 2020 02:25 UTC
  • Jumanne tarehe 24 Novemba 2020

Leo ni Jumanne tarehe 8 Mfunguo Saba rRabiuthani 1442 Hijria sawa na Novemba 24 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1210 iliyopita alizaliwa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Madina. Imam Askari alilazimishwa na watawala wa Bani Abbas kwenda uhamishoni huko Samurra akiwa pamoja na baba yake na kufaidika na elimu ya Imam Hadi kwa kipindi cha miaka 13. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha karibu miaka sita baada ya kuuawa shahidi baba yake. Sehemu ya umri wake wa miaka 28 iliishia katika jela za watawala madhalimu wa Bani Abbas au akiwa uhamishoni na chini ya udhibiti wa watawala hao. Hata hivyo mtukufu huyo hakuacha kueneza maarifa sahihi ya Uislamu na kulea kizazi cha wanazuoni hodari.

Katika siku kama ya leo miaka 1085 iliyopita yaani mwaka 357 Hijria, aliaga dunia Abu Firas al-Hamdani malenga na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Mbali na kuandika mashairi, Abu Firas al-Hamdani alikuwa mpiganaji na miongoni mwa watu wa karibu kwa Seif ad-Dawlah mtawala wa Halab na alikuwa miongoni mwa makamanda wake.

Abu Firas al-Hamdani

Siku kama ya leo miaka 388 iliyopita, alizaliwa Baruch de Spinoza mwanafalsafa na mtaalamu wa elimu jamii wa Uholanzi. Spinoza alisoma kwa bidii na kukwea daraja za kielimu. Hata hivyo ukosoaji wake wa dini ya Kiyahudi ulimfanya akabiliwe na chuki na uhasama wa maulama wa dini hiyo. Njia na fikra za kifalsafa za Spinoza zilikaribiana na itikadi za kisufi. Msomi huyo wa elimu ya falsafa wa Uholanzi ameandika pia vitabu kadhaa kama The Philosophy of Spinoza na The Road to Inner Freedom. Baruch de Spinoza alifariki dunia mwaka 1677.

Baruch de Spinoza

Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita, Michael Faraday mwanafizikia stadi wa Kiingereza aligundua mkondo wa umeme unaojulikana kitaalamu kama ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Faraday alizaliwa mwaka 1791 na awali alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza vitabu. Ni kipindi hicho ndipo taratibu alipoanza kusoma vitabu mbalimbai na kuanza kuvutiwa na masuala ya kielimu. Miaka michache baadaye akawa msaidizi wa maabara. Akiwa katika maabara hiyo Faraday alifanya utafiti mwingi kuhusiana na jinsi ya kutengeneza balbu za umeme. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.

Michael Faraday

Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mkubwa wa Ufaransa, Henri Toulouse Lautrec. Familia ya Lautrec ilikuwa ya kipato cha wastani na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi ya kimaisha, Lautrec alitokea kuwa miongoni mwa wasanii mashuhuri na hodari wa Ufaransa kutokana na kipawa chake kikubwa. Msanii huyo alifariki dunia mwaka 1901.

enri Toulouse Lautrec

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 Muhammad Hadi Farzaneh, maarufu kwa jina la Hakim Farzaneh, mtaalamu mkubwa wa elimu ya theolojia na falsafa. Hakim Farzaneh alizaliwa mwaka 1302 Hijiria katika moja ya maeneo ya mji wa Isfahan. Alisoma elimu ya msingi eneo alikozaliwa na kisha kuelekea mjini Isfahan kwa ajili ya kuendelea na masomo yake ambapo alipata kusomea elimu mbalimbali muhimu hususan theolojia na falsafa. Aliweza kuinukia kielimu na kuwa msomi mkubwa kiasi kwamba mwishoni mwa umri wake alikuwa miongoni mwa wataalamu wa taaluma hizo. Baadaye alirejea katika mji alikozaliwa na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji hadi alipofariki dunia.

Muhammad Hadi Farzaneh,

Miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 4 Azar 1345 Hijria Shamsia, alifariki dunia mhadhiri wa chuo kikuu Jabbar Baghche Ban baada ya kutumia muda wake mwingi katika kuwahudumia kwa moyo mkunjufu viziwi wa Iran. Mnamo mwaka 1302 Hijria Shamsia, Baghche Ban alianzisha kituo cha kuwafunza na kuwalea watoto viziwi katika mji wa Tabriz, ulioko kaskazini magharibi mwa Iran na huo ndio uliokuwa mwanzo wa jitihada za muda mrefu za mhadhiri huyo za kuwafundisha watoto viziwi. Aliwafundisha watoto hao kusoma na kuandika kwa kugundua mbinu mpya za kujifunza alfabeti ambayo inatumika siku hizi. Baghche Ban pia mwaka 1313 Hijiria Shamsia alianzisha shule ya kwanza ya wanafunzi viziwi nchini Iran.

Jabbar Baghche Ban

Na siku kama ya leo miaka 7 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi 6 zinazounda kundi la 5+1 zilitia saini makubaliano ya muda ya nyuklia mjini Geneva huko Uswisi. Kutiwa saini makubaliano hayo kulitayarisha uwanja mzuri na kufungua njia ya mazungumzo zaidi kati ya Iran na nchi hizo sita ambazo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Russia, China na Ujerumani kwa ajili ya kutia saini makubaliano kamili ya nyuklia na kuondoa hitilafu kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia hapa nchini, na mwishowe kufutwa vikwazo vya kidhalimu vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

 

Tags