May 30, 2017 08:51 UTC
  • Ramadhani, mwezi wa ibada na toba

Bismillahir Rahmanir Rahim Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuhu na karibuni kujiunga nami katika makala hii maalumu niliyokundalieni kwa mnasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atutakabalie saumu na ibada zetu katika mwezi huu mtukufu.

Tuko katika msimu wa rehema na kuteremka baraka za Mwenyezi Mungu. Tunamshukuru Mola kwa kutupatia taufiki ya kuishi katika wakati kama huu uliojaa nuru. Tunamshukuru Mola kwa kutufikisha katika mwezi huu na kuweza kumtii na kumnyenyekea. Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni ishara ya ukarimu wa Mwenyezi Mungu. Mwezi huu ni kama maji ya uhai ambayo hukidhi kiu kali. Wapenzi wasikilizaji tuko katika mwezi ambao Mtume Muhammad SAW alisema hivi kuuhusu: ‘Unakuja katika nyoyo kwa baraka na maghfira na kwa siku kadhaa kutua katika nyoyo za waumini wenye hamu....'Jambo la kwanza ambalo tunapaswa kufanya kuhusiana na mwezi wa Ramadhani, ni kufahamu kwa njia sahihi kuhusu malengo na falsafa ya mwezi huu.Muumini anapaswa kudiriki sababu ya kuwepo saumu na ni kwa nini amefaradhishiwa ibada hiyo. Kila wakati ulipowadia mwezi Mtukufu wa Ramadhani Imam Sajjad AS alikuwa akimuomba Mwenyezi Mungu ampe maarifa ya kuujua mwezi huu kwa kusema: ‘Ewe Mola! Sala na salamu zimfikie Mohammad na Kizazi Chake, nijaalie niweze kutambua fadhila za mwezi wa Ramadhani na kulinda heshima yake." Anas Bin Malik anasema: "Wakati mwezi wa Ramadhani ulipokuwa ukiwadia, Mtume SAW alisema: "Subhan'Allah! Tizama unaenda kuukaribisha mwezi upi na utakuletea kitu gani." Imam Ali AS alimuuliza Mtume SAW hivi, ‘Amali bora zaidi katika Mwezi huu ni ipi?' Mtume Mtukufu alijibu kwa kusema: ‘Kazi bora zaidi ni kujizuia na yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu.'

 

Hii ina maana kuwa mwanaadamu ajizuie kufanya mambo yote yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu.Kama unavyojua, mafundisho matukufu ya Kiislamu ni mjumuiko wa sheria muhimu katika uhai wa mwanaadamu. Mafundisho ya Kiislamu humuokoa mwanaadamu kutoka mtego wa matamanio ya kinafsi na kinyama. Hii ni kwa sababu maadamu nafsi ya mwanaadamu imetumbukia katika mtego wa shahawati na matamanio ya kinafsi hawezi kamwe kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Uislamu unawataka wafuasi wa dini hii tukufu kujitahidi kuelekea katika ucha Mungu. Saumu ni moja kati ya ibada zenye kumjenga mwanaadamu katika Uislamu na ibada hii ina faida nyingi sana. Moja ya faida za saumu ni kuimarisha maarifa na ujuzi katika moyo wa mwanaadamu.Saumu hasa saumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni jambo ambalo huondoa shahawati za kishetani na mahala pake kuchukuliwa na taqwa pamoja na kutii maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Kuvunjwa shahawati za kishetani katika nafsi ya mwanaadamu hupelekea kuibuka nuru na mwangaza katika batini na dhahiri ya mwanaadamu.Katika kivuli cha usafi na utakasifu utokanao na saumu, mwenye kufunga hajizuii tu kula na kunywa katika wakati ulioainishwa, bali pia viungo vyake vya mwili kama vile macho, miguu na ulimi hujizuia na yale yaliyoharamishwa. Kwa njia hii mwenye kufunga huweza kufikia daraja ya juu ya taqwa kiasi kwamba hujiepusha na hata dhambi za kifikra na hivyo kufikia kilele cha ibada. Imam Ali AS vile vile anaashiria kiwango hicho cha taqwa kwa kusema: ‘Saumu au kujiepusha na madhambi ya kimawazo ni saumu ya juu zaidi kulikosaumu ya tumbo ya kujizuia kula na kunywa.' (Ghurar al Hikam Uk.203) Maana ya maneno hayo ya Imam Ali ni kuwa katika saumu tusitosheke tu na kujizuia kula na kunywa bali tujitahidi pia tufikie natija ya kimaanawi.

Waislamu nchini Tanzania

 

Marhum Mullah Husseingholi Hamedani ni mmoja kati ya maulamaa mashuhuri wa Iran na alibobea sana katika masuala ya kutakasa nafsi na malezi. Inasemekana kuwa alipokuwa akifundisha, hotuba zake ziliwaathiri sana wanafunzi wake. Wanaomjua wanasema alikuwa na imani na irada thabiti katika kufuata njia ya Mwenyezi Mungu.Siku moja mwanazuoni huyu mkubwa wa akhlaqi aliulizwa ni kazi gani mtu afanye ili kujirekebisha kinafsi na kupata maarifa? Alijibu kwa kusema: "Hakuna kazi bora zaidi kuliko kusujudu kwa muda mrefu na ukiwa katika hali hiyo soma sehemu ya aya ya 87 ya Suratul Anbiya isemayo:لا إِلَهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَکَ إِنِّی کُنتُ مِنَ الظَّالِمِینَ Hapana mungu isipokuwa Wewe Subhanaka Uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.

Imenukuliwa kuwa, wanafunzi wake walitekeleza muongozo wake huo na kupata baraka nyingi.Baraka za kusujudu ni maarufu kwa watendao amali hii. Athari za kusujudu hubainika hasa iwapo sijda itakuwa ni yenye kudumu kwa muda mrefu na kutekelezwa kwa uzingatiaji. Imenukuliwa kuwa kulikuwa na kijana mmoja aliyempenda sana Mtume SAW. Mahaba hayo yalikuwa makubwa kiasi kwamba kijana huyo alikuwa akimtembelea Bwana Mtume kila siku kabla ya kuendelea na shughuli zake maishani. Lakini kulikuwa na jambo lililokuwa likimsumbua sana. Siku moja alifika mbele ya Mtume SAW na kumwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, daraja na hadhi yako ni ya juu sana. Najua kuwa hautakuwa nami daima duniani. Wakati huo ukifika sijui nivumilie vipi kuwa mbali nawe?Mapenzi ya kijana huyo kwa Mtume SAW yalikuwa yamejawa Ikhlasi kiasi kwamba Allah SWT alimtuma Jibril amfahamishe Mtume SAW kuwa kijana huyo atakuwa naye peponi. Hapo Mtume SAW kwa maneno yaliyojaa ukarimu na mahaba alimsemesha kijana huyo kwa kusema: ‘Ewe Kijana! Je, unataka kunisaidia? Yule kijana kwa furaha akasema Naam, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niambie ni vipi nikusaidie? Mtume alijibu kwa kusema: ‘Kwa istighfara na sijda ndefu.'Wapenzi wasikilizaji kwa kauli hiyo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ndio tunafikia mwisho wa makala yetu hii kwa leo. Tunamuomba Mola atutakabalie saumu na ibada zetu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.Wasalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags