Jumatatu Disemba 14 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 14 Desemba 2020 Miladia.
Miaka 804 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Damascus. Alizaliwa mwaka 560 Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka, Halab (Aleppo) na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".
Siku kama ya leo miaka 215 iliyopita, sawa na 14 Disemba 1805, iligunduliwa nishati ya joto ya makaa ya mawe na George Branclon, mhunzi kutoka Uingereza. Kabla ya hapo, makaa ya mawe yalikuwa yakitumiwa kama mojawapo ya vifaa vya kujengea nyumba. Shehena ya kwanza ya madini ya makaa ya mawe yaliyotumiwa katika nishati ya joto, ilipatikana katika bandari Plymouth nchini Uingereza.
Miaka 109 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1911, baada ya juhudi na jitihada za miaka mingi, hatimaye Ncha ya Kusini yaani South Pole ilivumbuliwa na kwa mara ya kwanza na wavumbuzi kadhaa waliwasili katika eneo hilo. Katika siku hii, Roald Amundsen baharia mashuhuri wa Kinorway aliyekuwa akishindana na Robert Falcon Scott wa Uingereza ili kuifikia ncha hiyo ya kusini, aliibuka mshindi na kuitundika bendera ya Norway katika ncha hiyo. Robert Falcon Scott akiwa na wenzake walikumbana na theluji kali wakati wanarejea na kupoteza maisha yao.
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1981 Bunge la utawala haramu wa Israel 'Knesset' liliiunganisha rasmi miinuko ya Golan ya huko Syria na ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Hatua hiyo ilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa nchi za Kiislamu, Kiarabu pamoja na jamii ya kimataifa. Utawala dhalimu wa Israel uliikalia kwa mabavu miinuko hiyo ya Golan ya Syria katika vita baina yake na Waarabu mwaka 1967.
Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Dayton Peace Agreement" yaani Makubaliano ya Amani ya Dayton" yalithibitishwa kwa mara ya mwisho katika kikao kilichofanyika mjini Paris, Ufaransa. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa ni kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa dhidi yao na Waserbia.