Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (20)
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi.
Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 20 ya mfululizo huu.
Tukiendelea na mazungumzo yetu kuhusu Haki za Kimaumbile, kwa kimombo Natural Laws, ni kwamba mjadala kuhusu haki za kimaumbile umekuwa na miinuko na miteremko mingi katika zama tofauti; na baadhi ya wakati umeambatana na hatua za kufurutu mpaka. Lakini kwa ujumla tunaweza kusema kuwa kabla ya zama za Mvuvumko mkubwa wa Sanaa na Maarifa zinazojulikana kitaalamu kama Renaissance, mitazamo ya kutetea haki za kimaumbile za mtu haikuwa na mgongano na suala la wajibu wa kidini na mamlaka ya utawala wa Mwenyezi Mungu. Kwa mfano Marcus Tullius Cicero, mwananadharia na mzungumzaji mahiri wa Kirumi wa zama za BC, yaani kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masih, yeye anazielezea hivi haki za kimaumbile:”Ni sharia jumuishi ya ulimwengu mzima, isiyobadilika, ya milele na inayofahamika na akili timamu. Hakuna sharia kwa ajili ya Rome na Athens au kwa ajili ya sasa na mustakabali; bali kuna sharia moja tu, yenye itibari, ya milele na isiyoweza kubadilishwa kwa ajili ya mataifa yote na zama zote. Hakuna mtawala juu yetu sote ghairi ya Mwenyezi Mungu”, mwisho wa kumnukuu. Nadharia ya asili ya haki za kimaumbile ilisimama juu ya msingi huu, kwamba watu, wakiwa ni viumbe wa ulimwengu wa maumbile na wa Mwenyezi Mungu wanapaswa waendeshe maisha yao na kuratibu jamii yao kulingana na amri na kanuni za maumbile na za Mwenyezi Mungu.
Lakini katika zama za Mvuvumko mkubwa wa Sanaa na Maarifa, haki za kimaumbile nazo pia zikaingia katika awamu ya kupewa sura ya kisekulari. Hugo Grotius, ambaye anajulikana kama mwasisi wa Sharia za Kimataifa (International Laws) anasema:”Haki za kimaumbile zingeweza kupatikana hata kama kungekuwa hakuna Mungu”. Kwa hakika aina hii ya mtazamo kuhusu haki za kimaumbile ilizitoa haki hizo kwenye mduara wa kidini na kuziingiza kwenye mduara wa mawazo ya kibinadamu. Japokuwa kidhahiri, maneno hayo ya Hugo Grotius yana sura ya kilahidi, lakini yeye mwenyewe Grotius alikuwa mtu wa dini; na madhumuni ya maneno yake hayo yalikuwa ni kutilia mkazo na kusisitiza kuwa kanuni za ulimwengu wa uumbaji ni kitu thabiti, cha kuaminika na cha kimantiki. Lakini kwa vyovyote vile mtazamo wa aina hii ulikuwa ndio mwanzo wa kuzipa sura ya kisekulari haki za kimaumbile na kuikana nafasi ya dini katika suala hilo.
Leo hii, baada ya kujitokeza fikra za mielekeo ya Usasa, kwa kitaalamu Modernity na ya ukanaji umutlaki wa mambo kuwa heri tupu au shari tupu yaani Relativism, na kutawala mitazamo hiyo katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu, kila kitu chenye hata harufu ya uthabiti na kudumu kimekuwa kikitiliwa shaka na kuwekewa alama ya kuuliza. Haki za kimaumbile pia, kwa kuwa zimekuwa zikielezewa kwa msingi wa sharia thabiti na zisizobadilika za maumbile na fitra ya mwanadamu, nazo pia hazijatolewa nje ya kaida hiyo. Kwa hivyo haki za utungaji na upangaji zimehuishwa na kupewa uhai tena mkabala na haki za kifitra na kimaumbile. Watetezi wa sasa wa haki za kimaumbile wameziwekea mipaka kadhaa haki hizo; na hata kuna wakati wamezifunga na kuzibana kwenye haki moja tu ya kimaumbile kama haki sawa ya uhuru wa mtu binafsi. Lakini pamoja na ubanaji na uwekaji mipaka wote huo haki za kimaumbile zingali zinahesabiwa kuwa ni maudhui muhimu katika Sayansi ya Siasa na akhlaki.
Baadhi ya wanafikra walioathiriwa na nadharia ya Kimagharibi ya haki za kimaumbile wamedai kuwa Uislamu ni dini ya utekelezaji wajibu tu na inapuuza haki za watu. Madai haya yanatolewa kutokana na kutokuwa na uelewa na ufahamu wa mafundisho ya Uislamu. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, ulimwengu wa uumbaji una ghaya na lengo lake kuu; na unawaongoza viumbe kuelekea kwenye ukamilifu unaowastahiki. Kufikia kwenye ukamilifu kunategemea vipawa maalumu vya kila kiumbe. Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu vipawa tofauti; na kwa mtazamo wa Uislamu vipawa hivyo maalumu vya mwanadamu ndiyo msingi wa “haki za kimaumbile”. Shahidi Murtadha Mutahhari, anaeleza hivi kuhusiana na suala hilo:”Kwa mtazamo wetu, haki za kimaumbile na kifitra zimeanzia pale mfumo wa uumbaji, -kwa uono wa wazi na kwa kuzingatia lengo-, unapowaongoza viumbe kuelekea kwenye ukamilifu ambao umefichika kwenye vipawa vilivyomo ndani ya nafsi zao. Kila kipawa cha kimaumbile ni msingi wa kufikia “haki moja ya kimaumbile” na kinahesabiwa kuwa ni kielelezo kimoja cha kimaumbile kwa ajili ya haki hiyo. Kwa mfano mtoto wa mwanadamu ana haki ya kusoma na kwenda skuli, lakini mtoto wa kondoo hana haki hiyo. Kwa nini? Kwa sababu kipawa cha kusoma na kuwa mjuzi kimo ndani ya nafsi ya mwanadamu, lakini hakiko kwa kondoo”.
Kwa hivyo kwa mujibu wa Uislamu, “haki za kimaumbile” si jambo la kupangwa na kubuniwa, kwamba ziwe zimetungwa na kundi moja la wanasiasa au wanafalsafa na kupitishwa na kundi jengine la watu. Kwa maneno mengine, haki za kimaumbile si jambo la kupangwa ambalo mwanadamu anaweza kuwa nalo bila ya kujali na kuzingatia asili ya uumbaji. Ni suala la kifitra na kimaumbile ambalo ametunukiwa mwanadamu na Muumba wa ulimwengu ili kumuongoza kuelekea kwenye uokovu na umaanawi kulingana na uumbwaji wenye lengo maalumu wa kiumbe huyo.
Ni kuanzia hapa ndipo inapodhihirika na kubainika tofauti iliyopo baina ya mtazamo wa Kimagharibi na wa Kiislamu katika kutoa tafsiri ya misingi na chimbuko la haki za kimaumbile. Watetezi wengi wa haki za kimaumbile na za binadamu huko Magharibi hutaja hamu, matashi na ghariza tu za mwanadamu kama chimbuko na msingi wa haki hizo. Katika maandiko ya Kimagharibi ya haki za kimaumbile za mwanadamu haizungumziwi kabisa nafasi ya akili katika kuyadhibiti matashi ya kinafsi na kihayawani ya kiumbe huyo na pia katika utukukaji na kufikia ukamilifu anaostahiki. Lakini chimbuko la haki za kimaumbile na za binadamu katika Uislamu ni utu wa mwanadamu mwenyewe, ambaye ana lengo maalumu; na lengo lenyewe ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
Katika mtazamo wa Kimagharibi, kwa kuwa “wajibu” unayabana matashi na ghariza za nafsi ya mtu, unachukuliwa kuwa unapingana na haki za kimaumbile. Lakini katika mtazamo wa dini, kwa kuwa “wajibu” unamsogeza na kumkurubisha mwanadamu kwenye ghaya na lengo kuu la maisha yake, na kwa kuwa unaendana na vipawa vya kiutu, unachukuliwa kuwa ni sawa kabisa na “haki ya kiutu”. Haki za kimaumbile za mtu zinatokana na utu wake, si kiwiliwili na nafsi yake ya kihayawani. Na kwa kuwa mwanadamu ana ghaya na lengo kuu inapasa tuziratibu haki zote za kiutu kulingana na lengo lake aali. Kwa msingi huu, haki za kiutu, zinahusiana na utu wa mtu, na kila jambo ambalo linamuinua mtu na kumfikisha kwenye ukamilifu, jambo hilo litaitwa “haki za binadamu”. Kinyume chake, kile kinachozuia utukukaji na ukuaji wa utu wa mtu, sio tu si haki za binadamu, bali ni kitu kinachopasa kukemewa na kulaumiwa vikali kwa kusababisha madhara kwa haki za binadamu.
Katika mtazamo wa kimantiki na kidini, haki za kimaumbile ni haki ya aina yoyote inayowezesha kuchanua kipawa cha mwanadamu na kudhamini saada ya kweli ya kiumbe huyo. Kwa kuwa wajibu na faradhi za kidini ni mambo yenye taathira chanya kwa saada halisi na ya kweli ya mwanadamu nazo pia zinahesabika kuwa miongoni mwa haki za binadamu, japokuwa kidhahiri na kwa mtazamo wa kijuujuu zinawekea mpaka baadhi ya uhuru wa mtu binafsi.
Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshallah katika sehemu nyengine ya kipindi hiki. Nakuageni na kukutakieni heri na fanaka maishani…/