Jumatano tarehe 21 Julai 2021
Leo ni Jumatano tarehe 10 Mfunguo Tatu Dhulhija 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Julai 2021.
Leo tarehe 10 Dhilhaj ni sikukuu ya Idul Adh'ha, moja ya sikukuu kubwa za Kiislamu. Katika siku hii mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu waliokwenda Makka, huchinja mnyama kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mola wao na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii Mtukufu Ibrahim (as). Mwenyezi Mungu aliijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumwamuru amchinje mwanawe kipenzi Ismail (as). Licha ya mashaka ya utekelezwaji wa amri hiyo, Nabii Ibrahimu (as) aliandaa mazingira ya kutekeleza amri hiyo na kumlaza chini mwanaye na kuanza kuikata shingo yake lakini kisu kilikataa kuchinja. Hapo ndipo alipoambiwa na Mwenyezi Mungu kuwa amefaulu mtihani huo na akamtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanaye Ismail. Tukio hili lenye ibra na mafunzo tele linawapa wanadamu somo la kujitoa mhanga, kujisabilia kwa ajili ya Allah, kushinda matamanio na matakwa ya nafsi na kusalimu amri mbele ya amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii kubwa.

Siku kama ya leo miaka 142 iliyopita John Boyd Dunlop raia wa Uingereza, alikuwa mvumbuzi wa kwanza wa gurudumu. Dunlop alifikia hatua ya kuvumbua gurudumu la magari baada ya utafiti wa miaka kadhaa. Alifariki dunia 1921.

Katika siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, yaani sawa na tarehe 21 Julai mwaka 1899, alizaliwa mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Kwa muda fulani Hemingway alikuwa mwandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka kwa wepesi. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Hemingway alipendelea sana kuwinda na alitumia muda mwingi katika shughuki hiyo. Alifariki dunia tarehe pili Julai 1961 baada ya kujipiga risasi na bunduki yake mwenyewe ya kuwindia, wakati akiisafisha. Hivyo, mkasa wa kifo cha baba yake ukawa umejirudia kwake baada ya kupita miaka 23. Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni pamoja na kitabu cha "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na "For Whom The Bell Tolls".

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, kulifanyika maandamano makubwa mjini Tehran na kwenye miji mingine ya Iran baada ya Dakta Musaddiq kujiuzulu cheo cha Waziri Mkuu. Wakati huo Ayatullah Kashani alitoa taarifa ya maneno makali baada ya Dakta Musaddiq aliyekuwa Waziri Mkuu kujizulu na Shah kumteuwa Ahmad Qavam mashuhuri kwa jina la Ghavam Sultaneh kuwa Waziri Mkuu. Ayatullah Kashani alitoa taarifa hiyo akilalamikia vikali agizo la Shah la kumteuwa Ghavam kushika wadhifa huo. Ahmad Qavam ambaye alikuwa na uhusiano na wakoloni na kibaraka wa utawala wa kibeberu wa wakati huo, muda mfupi baada ya kuwa Waziri Mkuu, alianzisha njama za kutenganisha dini na siasa na kuendesha propaganda dhidi ya Ayatullah Kashani na wanaharakati wa Kiislamu nchini Iran.

Katika siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 21 Julai 1954 ulitiwa saini mkataba wa kuacha vita kati ya Ufaransa na Vietnam na kukomesha ukoloni wa Ufaransa huko India na China mwishoni mwa mkutano wa Geneva. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya kuanguka ngome imara ya Wafaransa iliyojulikana kwa jina la Dien Bien Phu nchini Vietnam Mei mwaka 1954. Makubaliano ya mkutano wa kimataifa wa Geneva, yalihudhuriwa na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka Ufaransa, Marekani, Uingereza, China, Vietnam na Urusi ya zamani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vikosi vya kigeni vilipaswa kuondoka Vietnam, lakini Marekani kinyume na makubaliano ya Geneva, ikaamua kutuma majeshi katika eneo hilo kwa lengo la kuzuia kuungana maeneo mawili ya Vietnam ya kaskazini na ya kusini.

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, meli ya kwanza ya biashara ya nyuklia iliyopewa jina la NS Savannah iliwekwa majini huko Marekani. Baada ya kugunduliwa atomu na wasomi kutambua nguvu kubwa na nishati ya atomiki ilijitokeza fikra ya kutumia nishati hiyo katika masuala mbalimabali. Hata hivyo inasikitisha kwamba, nishati hiyo ilitumiwa kwa mara ya kwanza kielimu katika kutengeneza mabomu ya nyuklia. Suala hilo lilichochea mashindano ya kutengeneza silaha na mabomu ya nyuklia kati ya madola makubwa duniani na kuiweka dunia katika ncha ya vita vya nyuklia. Meli ya NS Savannah ilikuwa matokeo ya jitihada za wasomi za kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani na katika siku kama hii ya leo yaani tarehe 21 Julai mwaka 1958 meli hiyo ya kibiashara iliyokuwa ikitumia nishati hiyo iliwekwa majini na kuanza kufanya kazi. NS Savannah ilikuwa meli ya kwanza iliyotumia nishati ya nyuklia kuvuka habari ya Atlantic.

Na tarehe 10 Dhulhija miaka 6 iliyopita katika sikukuu ya Idil Adh'ha ardhi tukufu ya Mina huko Saudi Arabia ilikuwa machinjio ya maelfu ya mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kutokana na azembe wa maafisa na wasimamizi wa Hija wa Saudia. Siku hiyo ilishuhudia tukio baya zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 3 asubuhi wakati baadhi ya mahujaji walipokuwa wakielekea eneo la Jamarat kumpiga mawe Shetani. Ghafla maafisa wa Saudi Arabia walifunga barabara za kuelekea eneo hilo na kukatokeo msongamano mkubwa kupita kiasi wa maelfu ya mahujaji, suala lililosababisha vifo vya zaidi ya mahujaji elfu 7 kutoka nchi mbalimbali duniani. Mahujaji 464 wa Iran pia waliaga dunia katika tukio hilo ambazo lilidhihirisha tena uzembe na kutokuwa na uwezo wa kusimamia vyema ibada ya Hija wa serikali ya Saudia.
