Ijumaa tarehe 20 Agosti 2021
Leo jni Ijumaa tarehe 11 Muharram 1443 Hijria sawa na tarehe 20 Agosti mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, yaani tarehe 11 Muharram mwaka 61 Hijiria, msafara wa mateka wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (saw), baada ya tukio chungu la mauaji ya siku ya Ashura, ulianza safari ya kelekea Sham, yalikokuwa makao makuu ya utawala wa dhalimu wa Yazidi bin Muawiya. Baada ya majeshi ya Yazidi yaliyokuwa yakiongozwa na Omar bin Sa’ad kumuua shahidi Imam Hussein (as) na masahaba wake, majeshi hayo ambayo hayakuwa na chembe ya ubinadamu moyoni, yalianza kupora vitu vya thamani vya msafara wa watu wa familia ya Mtume (saw). Askari hao sanjari na kuchoma moto mahema ya Imam Hussein (as) na watu wake, waliwanyang’anya pia wanawake mapambo yao na kila walichokuwa nacho. Jioni ya siku kama ya leo msafara wa familia ya Imam Hussein uliokuwa ukiongozwa na Imam Sajjad (as) na Bibi Zainab (as), ulielekea Kufa na baadaye Sham.

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita Marekani ilikiri kwamba ilifanya makosa kuishambulia ndege ya abiria ya Iran hapo tarehe 3 Julai mwaka 1988. Siku hiyo ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege ya Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani, USS Vincennes, ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu 298 waliokuwemo. Shambulio hilo lilionyesha wazi unyama wa serikali ya Marekani na ukatili wake hata kwa wanawake na watoto wadogo waliokuwemo ndani ya ndege hiyo. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa.

Miaka 29 iliyopita, Estonia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru. Estonia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Estonia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii.

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, yaani Agosti 20 mwaka 1998 Marekani ilizishambulia kwa makombora ya masafa marefu nchi za Sudan na Afghanistan. Serikali ya Washington ilidai kwamba, watu walioshiriki katika kulipua kwa mabomu balozi za Marekani mjini Dar es Salaam, Tanzania na Nairobi, Kenya wiki mbili kabla, walikuwa na uhusiano na nchi hizo. Washington pia ilidai kuwa ilikishambulia kwa mabomu kiwanda cha kuzalisha madawa cha ash-Shifaa nchini Sudan kwa sababu eti kilikuwa kikitengeneza mada za kemikali. Hata hivyo weledi wa masuala ya kisiasa walisema kwamba, sababu ya Marekani kufanya mashambulio ya mabomu dhidi ya Sudan na Afghanistan ilikuwa ni kujaribu kufunika fedheha ya kimaadili iliyokuwa ikimkabili Rais wa nchi hiyo Bill Clinton. Kwa sababu hiyo mashambulizi hayo yaliamsha hasira za fikra za walio wengi na serikali nyingi duniani dhidi ya siasa za kutumia mabavu na kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani.