Aug 24, 2021 02:41 UTC
  • Jumanne tarehe 24 Agosti mwaka 2021

Leo ni Jumanne tarehe tarehe 15 Muharram 1443 Hijria sawa na tarehe 24 Agosti 2021.

Siku kama ya leo miaka 1090 iliyopita, yaani tarehe 15 Muharram mwaka 353 Hijiria, alifariki dunia Ibn Sakan mwanazuoni na mpokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijiria. Ibn Sakan alizaliwa mwaka 294 Hijiria huko mjini Baghdad, Iraq ambapo alisafiri katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Ibn Sakan alikusanya hadithi nyingi katika miji ya nchi kama Uzbekistan, Tajikistan, Kazakhstan Kyrgyzstan (Transoxiana), Khorasan, Iraq, Sham na Misri na mwishowe akaweka makazi yake nchini Misri. Mpokezi huyo wa hadithi ameacha athari nyingi na mojawapo ni kitabu cha historia kinachohusu maswahaba wa Mtume SAW, kinachoitwa Al Huruf fi Al -Swahaba.

Katika siku kama ya leo, miaka 854 iliyopita, sawa na tarehe 15 Muharram mwaka 589, alizaliwa Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq. Ibn Twaus alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia mjini Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "al Luhuuf" ambacho ndani yake alizungumzia kwa namna bora zaidi matukio ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya vita vya Karbala. Kitabu kingine mashuhuri cha mwanazuoni huyo ni "Al Iqbal". Ibni Twaus alifariki dunia mwaka 664 akiwa na umri wa miaka 75.

Saayyid Ibn Taus

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, yalianza mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas. Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad (saw) wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Mi'iraj na kwa sababu hiyo eneo hilo likawa na umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano hayo ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao taratibu walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina kwa kuungwa mkono na Uingereza, walianzisha harakati dhidi ya Waislamu. Siku hiyo Wapalestina wenye hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni hao maghasibu. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina.

Miaka 43 iliyopita katika siku kama hii ya leo Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu aliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Shah. Shahidi Andarzgu alianza harakati za mapambano akiwa na umri wa miaka 19 na kufahamiana kwa karibu shahidi Nawab Safawi, kiongozi wa kundi la Waislamu wanamapinduzi. Baada ya hapo Shahid Andarzgu alijiunga na harakati ya Muutalifeye Eslami na alikuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Shah, Hussein Ali Mansour. Shahid Andarzgu aliendesha mapambano ya siri dhidi ya utawala wa Shah kwa kipindi cha miaka 13 na hatimaye aliawa shahidi shahidi na vibaraka wa Shah katika siku kama hii ya leo katika mapambano ya silaha.

Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu

Na siku kama leo miaka 30 iliyopita, Ukraine ilipata uhuru toka kwa Umoja wa Kisovieti. Russia ilianza kuikalia kwa mabavu Ukraine ambayo wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland, katikati mwa karne ya 17 Miladia. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo iliunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ikajipatia uhuru wake.