Sep 02, 2021 07:11 UTC
  • Mchakato wa Chanjo ya COVID-19 ya Iran, Coviran Barekat

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknoloaji nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Kituo cha Habari cha Kitengo cha Utekelezaji wa Maagizo ya Imam Khomeini (M.A) kimetangaza kuwa, dozi milioni 8 za chanjo ya corona ya Coviran Barekat zimezalishwa hapa nchini. Kituo hicho kimeripoti kuwa, hadi kufikia Agosti 30 jumla ya dozi milioni nane za chanjo ya corona ya Coviran Barekat zimezalishwa hapa nchini. Kimeongeza kuwa, idadi ya chanjo zilizokabidhiwa kwa Wizara ya Afya na Tiba ya Iran hadi kufikia jana Jumatatu ni karibu milioni nne na laki mbili; na kwamba chanjo zilizosalia zinaendelea kupitia mchakato wa kukaguliwa na kutazamwa ubora wake. 

Chanjo hiyo ya UVIKO-19 iliyotengenezwa na watafiti wa Kiirani ilianza kufanyiwa majaribio kwa wanadamu siku ya Jumanne 29 Disemba mwaka jana ambapo watu waliojitolea walidungwa chanjo hiyo. 

Mchakato wa kusajili chanjo ya kuzuia ugonjwa wa COVID-19 iliyoundwa hapa nchini Iran ya COVIran Barekat katika Shirika la Afya Duniani (WHO) tayari umeanza.

Kuzinduliwa chanjo COVIran Barekat kunaiweka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika orodha ya nchi sita tu duniani zinazotengeneza chanjo za Corona. Tayari nchi 12 zikiwemo za Ulaya, Asia na Amerika ya Latini zimewasilisha maombi ya kutaka kuagiza chanjo ya COVIran Barekat.

Iran iko mbioni kuunda chanjo kadhaa za COVID-19, ambapo mbali na  chanjo ya hiyo COVIran Barekat, chanjo zingine ambazo zimepiga hatua nzuri katika majaribio ni pamoja na Razi Cov Pars, Noora,  Fakhra na chanjo ya pamoja ya Taasisi ya Chanjo ya Finlay ya Cuba na Taasisi ya Chanjo ya Pasteur ya Iran.

Mtanzania abuni mtungi wa oxijeni

George Nyahende, raia wa Tanzania amebuni na kutengeneza mashine ya oksijeni ambayo ina sifa za kipekee ambazo anasema zinatokana na mazingira hususani ya vijiji vya Tanzania.

Kupitia katika mahojiano na Kituo cha habari UNIC Dar es Salaam Tanzania, Nyahende ambaye ameipatia mashine yake hiyo jina lake Nyahende, ameeleza kinagaubaga namna alivyolifikia wazo hilo kwamba ni kutokana na kushuhudia kifo kilichotokana na nyoka.

Nyahende anasema, “kilichonisukuma ni kwamba wakati fulani nilitembelea sehemu fulani inaitwa Longido, Arusha. Kule kuna mama mmoja aligongwa na nyoka aina ya koboko au Black Mamba, sumu yake huwa inaathiri mfumo wa kupumua. Sasa baada ya muda alifariki na nilipoulizia wataalamu pale wakasema amefariki kwa sababu hawakuwa na mashine za kusaidia kupumua. Na nilipoangalia huko kijijini kulikuwa hakuna umeme wala nini, nikajua kama huyo ni mmoja ina maana kuna tatizo kubwa katika nchi nzima ndipo nilipoingiwa na wazo kwamba nijaribu kutengeneza hizo mashine lakini ambazo zitakuwa na uwezo wa kutumika hata kwenye sehemu hizo ambazo hazina nishati ya umeme.”

Mhandisi huyu anaeleza kuwa mashine anazozitengeneza zina uwezo wa kufanya kazi hata bila kutegemea mitungi ya gesi iliyobeba oksijeni kwani, “ni mashine rahisi ambazo zinaweza zikatumika katika mazingira yoyote na nimelenga zaidi vijijini kwa hiyo zinaweza zikatumia umeme wa nishati ya kawaida, umeme wa jua, au betri ya gari moja kwa moja au betri za redio zile nane za kawaida zinaweza zikaendesha hii mashine. Na inaweza ikatumia mifumo miwili ya hewa, ile ya Oksijeni iliyoko kwenye mitungi au hii hewa tunayovuta sisi, inaweza kubadilishwa ikachujwa na ikatumia kwa mgonjwa.”

Nyahede ambaye ni mkazi wa Arusha kaskazini mwa Tanzania, anasema kwa kadri atakavyodhidi kupata ufdahili au uwekezaji zaidi, ataendelea kuuboresha uvumbuzi wake huo, ili uende kusaidia watu kuanzia hospital hadi majumbani kwani ni mashine ambazo zinaweza kutumiwa katika mazingira yoyote hata kwa ngazi ya familia.

Homa ya Hepatitis 

Katika kila sekunde 30 mtu mmoja anafariki dunia kutokana na ugonjwa wa homa ya ini, au Hepatitis, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO katika taarifa zake kuelekea siku ya kimataifa ya ugonjwa huo hatari lakini ambao bado umma haujawa na taarifa za kutosha kuhusu hatari zake.

Ujumbe wa mwaka huu wa siku hiyo ya homa ya ini duniani inayoadhimishwa kila tarehe 28 ya mwezi Julai ni “homa ya ini haiwezi kusubiri” ikiwa ni katika kuchagiza kuhusu umuhimu wa juhudi za haraka kwa ajili ya kutokomeza homa ya ini kuwa tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.

WHO inasema licha ya uwepo wa ugonjwa wa Corona au COVID-19,  lazima kuwepo na juhudi za makusudi za kukabiliana na magonjwa mengine ikiwemo homa ya ini ambao ni  ugonjwa unaoambukiza.

Aina za homa ya ini kuwa ni A, B, C, D na E, hata hivyo  aina zinazotambulika zaidi na hatari zaidi ni B na C yaani Hepatitis B na Hepatis C. Iwapo mgonjwa hatopatiwa tiba ya haraka dhidi ya aina hizi mbili anaweza kupoteza maisha. Hizi mbili njia zake za maambukizi zinafanana na zinaweza kuenea hata kwa mtoto ambaye yuko tumboni mwa mama yake ndio maana tunapatia  umuhimu zaidi.

Hata hivyo kuna njia za kinga na tiba. Ikiwemo chanjo dhidi ya homa ya ini na wagonjwa wanapona. Kuzuia ni pamoja na kuhakikisha hakuna kutumia sindano baada ya kutumika mara moja.

Polio barani Afrika

Na Nchi za Afrika zimeahidi kuangamiza aina zote zilizobaki za ugonjwa wa kupooza au polio sambamba na kuchukua hatua za kuelekea kutokomeza kabisa virusi vya ugonjwa huo. Ahadi hizo zimetolewa kwenye kikao maalumu kuhusu polio kilichofanyika kandoni mwa mkutano wa kamati ya 70 ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya Afrika. Wakati kanda ya Afrika ilithibitishwa kuwa bila ugonjwa wa polio mwaka mmoja uliopita kufuatia miaka minne bila kuwa na mgonjwa yeyote, milipuko ya virusi vya polio inayotokana na chanjo (cVDPV) inaendelea kuenea. cVDPV hutokea katika jamii ambapo watoto hawajapata chanjo ya kutosha ya polio.  Visa vya polio viliongezeka mwaka jana kwa sababu ya uvurugaji wa kampeni za chanjo ya polio uliosababishwa na janga la corona au COVID-19. 

Chanjo ya polio

WHO inasema idadi ya wagonjwa iliongezeka mwaka jana moja ya sababu kubwa ikiwa ni kufurugwa kwa kampeni za chanjo dhidi ya polio kulikosababishwa na janga la corona au COVID-19.

Nchi katika mkutano huo zimejadili jinsi zitakavyoanza kutekeleza mkakati mpya wa kutokomeza polio duniani (GPEI) 2022-2026, ambao ulizinduliwa mnamo  mwezi Juni ili kukomesha ueneaji wa CVDPV. 

Tangu Julai 2020, karibu watoto milioni 100 wa Kiafrika wamepewa chanjo dhidi ya polio.  Tangu mwaka 2018, nchi 23 katika eneo hilo zimepata milipuko ya polio na zaidi ya nusu ya visa 1071 vya cVDPV vilirekodiwa barani Afrika.